Tobiti 2

Tobiti 2

TOBITI KIPOFU

1Hata nilipofika tena nyumbani kwangu, na kurudishiwa mke wangu Ana na mwanangu Tobia, kwenye sikukuu ya Pentekoste, iliyo siku takatifu ya majuma saba, niliandaliwa chakula kizuri, nikakaa kitako nile.[#Kut 23:16]

2Ndipo nilipoona nyama tele, nikamwambia mwanangu, Nenda ukamlete mtu maskini yeyote utakayemwona miongoni mwa ndugu zetu amkumbukaye BWANA. Haya! Nakungojea.

3Akarudi, akasema, Baba, kuna mtu mmoja wa taifa letu amenyongwa; akatupwa sokoni.

4Mara, kabla sijadiriki kuonja chakula chochote, niliondoka kwa haraka, nikaenda nikamchukua, nikampeleka katika chumba hata kuchwa kwa jua.

5Kisha nikarudi nikaoga, nikala chakula changu kwa msiba,[#Hes 19:11-13]

6huku nikiukumbuka ule unabii wa Amosi, kusema,[#Amo 8:10]

Nitageuza sikukuu zenu kuwa maombolezo,

Na nyimbo zenu zote kuwa vilio.

Tobiti apofuka macho

7Kwa hiyo nikalia; na jua lilipokwisha kuchwa, nilikwenda nikachimba kaburi, nikamzika.

8Lakini jirani zangu walinidhihaki, wakasema Mtu huyu bado haogopi kuuawa kwa sababu ya tendo hilo; ingawa alikimbia; na kumbe! Anazika maiti tena.

9Usiku ule ule nilirudi mazikoni, nikalala kwenye ukuta wa kiwanja changu, maana nimenajisika; na uso wangu haukufunikwa.

10Wala sikujua kama wamo videge katika ukuta, na macho yangu yalikuwa wazi. Hivyo videge wakateremsha mavi ya moto ndani ya macho yangu; vikatokea vyamba vyeupe katika macho yangu. Nikaenda kwa matabibu wasiweze kunisaidia. Walakini Akiakaro alinilisha hata alipohamia Elimayo.

Anafanyakazi ya usokotaji

11Basi mke wangu Ana alikuwa akifanya kazi ya kusokota vyumbani mwa wanawake, naye alipomaliza kazi huzipeleka kwao wenyewe.

12Wao wakamlipa mshahara; tena wakampa na zawadi ya mwana-mbuzi.

13Na yule mwana-mbuzi alipokuwamo nyumbani mwangu alianza kulia. Kwa hiyo nikamwuliza mke wangu, Huyu mwana-mbuzi ametoka wapi? Je! Hukumwiba? Uwarudishie wenyewe, maana si halali kula kilichoibiwa.

14Naye akanijibu, Aa, ni zawadi yangu niliyopewa faida zaidi ya mshahara wangu. Lakini mimi sikumsadiki; nikamwagiza awarudishie wenyewe; nikamwonea haya. Akarudisha maneno, Je! Wewe, ziko wapi basi sadaka zako na matendo yako ya haki? Tazama ati! Umefahamika wewe na kazi zako zote.

Swahili Revised Union Version Bible © Bible Society of Kenya, and Bible Society of Tanzania, 2005.
Published by: Bible Society of Kenya