The chat will start when you send the first message.
1NAWASIHI wazee walio kwenu, mimi niliye mzee, mwenzi wao, na shahidi wa mateso ya Kristo, na mshirika wa utukufu utakaofunuliwa baadae;
2lichungeni kundi la Kristo lililo kwenu, na kulisimamia, si kwa kulazimishwa, bali kwa khiari; si kwa kutaka fedha ya aibu, bali kwa moyo;
3wala si kama wajifanyao mabwana juu ya mitaa yao, bali kwa kujifanya mfano kwa lile kundi.
4Na mchungaji mkuu atakapodhihirishwa, mtaipokea taji ya utukufu, ile isiyokauka.
5Vivyo hivyo ninyi vijana, watiini wazee. Naam, ninyi nyote jifungeni unyenyekevu kama mshipi, mpate kukhudumiana; kwa sababu Mungu hushindana na wenye kiburi, huwapa wanyenyekevu neema.
6Bassi nyenyekeeni chini ya mkono wa Mungu ulio hodari, awakweze kwa wakati wake;
7mkimtwika yeye taabu zenu zote, kwa maana yeye hujishughulisha sana katika mambo yenu.
8Erevukeni, kesheni; kwa kuwa mshitaki wenu Shetani, kama simba angurumae, huzungukazunguka, akitafuta mtu amle;
9mpingeni, mkiwa imara katika imani, mkijua ya kuwa mateso yaleyale yanatimizwa kwa ndugu zenu walioko duniani.
10Na Mungu wa neema yote, aliyewaita kuingia utukufu wake wa milele katika Kristo, mkiisha kuteswa kwa muda kidogo, yeye mwenyewe atawatengeneza, atawathubutisha, atawatia nguvu.
11Uweza una yeye hatta milele na milele. Amin.
12Kwa mkono wa Silwano, ndugu mwaminifu kama nionavyo, nimewaandikieni kwa maneno machache, nikionya na kushuhudia ya kuwa hii ndiyo neema ya kweli va Mungu. Simameni imara katika hiyo.
13Bibi mteule, mwenzi wenu aliye katika Babeli, awasalimu, na Marko mwanangu.
14Salimianeni kwa busu la upendo. Amani na iwe kwenu nyote, katika Kristo Yesu. Amin.