The chat will start when you send the first message.
1KILLA nafsi itumikie mamlaka makuu; kwa maana hapana mamlaka yasiyotoka kwa Mungu: na mamlaka yaliyopo yameamriwa na Mungu.
2Hivyo amwasiye mwenye mamlaka ashindana na agizo la Mungu; nao washindanao watajipatia hukumu.
3Kwa maana watawalao hawatii watu khofu kwa ajili ya matendo mema, bali kwa ajili ya matendo mabaya. Bassi, wataka usimwogope mwenye mamlaka?
4Fanya mema, utapata sifa kwake; kwa kuwa yeye ni mtumishi wa Mungu kwako kwa ajili ya mema. Lakini ufanyapo mabaya, ogopa; kwa maana hauchukui upanga burre: ni mtumishi wa Mungu, amlipizae kisasi mtenda mabaya kwa ajili ya ghadhabu.
5Kwa hiyo lazima kutumika, si kwa sababu ya ghadhabu tu, illa na kwa sababu ya dhamiri.
6Kwa sababu hiyo tena mwatoa kodi; kwa kuwa wao ni watumishi wa Mungu, wakidumu katika kazi hiyohiyo.
7Wapeni wote haki zao; mtu wa kodi, kodi; mtu wa ushuru, ushuru: astahiliye khofu, khofu; astahiliye heshima, heshima.
8Msiwiwe na mtu cho chote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendae mtu mwenzake ameitimiza sharia.
9Maana ile, Usizini, Usiue, Usiibe, Usishududu uwongo, Usitamani; na ikiwapo amri nyingine yo yote, inajumlishwa katika neno hili, ya kwamba, Mpende jirani wako kama nafsi yako.
10Peudo halimfanyizii jirani neno baya; bassi pendo ndio utimilifu wa sharia.
11Na hayo, tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia: kwa maana sasa wokofu u karibu yetu kuliko tulipoamini.
12Usiku unakwisha, mchana umekaribia; bassi tuyavue matendo ya giza, tuzivae silaha za nuru.
13Kama ilivyokhusika na mchana tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufasiki na uasharati, si kwa ugomvi na wivu.
14Bali mvaeni Bwana Yesu, wala msitafakari mahitaji ya mwili, nisije mkawasha tamaa zake.