1 Wathesalonike 2

1 Wathesalonike 2

Kazi ya Paulo Thesalonike

1Ndugu zangu, mnafahamu kuwa safari yetu kuja kwenu ilikuwa yenye nguvu.

2Lakini kabla ya kuja kwenu, watu wa Filipi walitutenda vibaya kwa kututukana matusi mengi na kutusababishia mateso. Mnafahamu yote kuhusu hilo. Na kisha tulipokuja kwenu, watu wengi huko walitupinga. Tuliwaeleza ninyi Habari Njema za Mungu lakini ni kwa sababu Mungu alitupa ujasiri tulio hitaji.

3Hatukuwa na kitu cha kupata faida kwa kuwaomba ninyi muiamini Habari Njema. Hatukuwa tunataka kuwafanya wajinga wala kuwadanganya.

4Hapana, tulifanya hivyo kwa sababu Mungu ndiye aliyetuagiza kazi hii. Na hii ilikuwa baada ya yeye kutupima na kuona ya kuwa tunaweza kuaminiwa kuifanya. Hivyo tunapoongea, tunajaribu tu kumpendeza Mungu, na sio wanadamu. Yeye tu ndiye awezaye kuona kilichomo ndani yetu.

5Mnafahamu kuwa hatukujaribu kuwarubuni kwa kusema mambo mazuri juu yenu. Hatukuwa tunatafuta jinsi ya kuzichukua pesa zenu. Hatukutumia maneno ama matendo kuficha tamaa yetu. Mungu anajua ya kuwa huu ni ukweli.

6Hatukuwa tukitafuta sifa toka kwa watu ama kutoka kwenu au kwa mtu yeyote.

7Tulipokuwa pamoja nanyi, kama mitume wa Kristo tulikuwa na uwezo wa kutumia mamlaka yetu kuleta madai ya nguvu kwenu. Lakini tulikuwa wapole kwenu. Tulikuwa kama vile mkunga anavyowahudumia watoto wake wadogo.[#2:7 Nakala nyingi za Kiyunani zina “Lakini tulikuwa watoto”.]

8Ilikuwa ni upendo wetu mkuu sana kwenu uliotufanya tuwashirikishe Habari Njema za Mungu. Zaidi ya hayo yote tulifurahi kuwashirikisha ninyi nafsi zetu wenyewe. Hiyo inadhihirisha ni kwa kiwango gani tuliwapenda.

9Ndugu zangu, ninajua kuwa mnakumbuka jinsi tulivyofanya kazi kwa bidii. Tulifanya kazi usiku na mchana ili tujitegemee, pasipo kumwelemea mtu yeyote wakati tukifanya kazi ya kuhubiri Habari Njema za Mungu.

10Tulipokuwa pamoja nanyi enyi mnaoamimi, tulikuwa safi, wa kweli, na wasio na kosa lolote kwa namna tulivyoishi maisha matakatifu. Mnafahamu, kama vile Mungu anavyotenda, kuwa jambo hili ni la kweli.

11Mnafahamu jinsi tulivyo mtendea kila mmoja wenu kama vile baba anavyowatendea wanaye.

12Tuliwatia moyo, tuliwafariji, na tuliwaambia kuishi maisha mema kwa Mungu. Yeye anawaita muwe sehemu ya maisha mema mbele za Mungu.

13Pia, tunamshukuru Mungu pasipo kuacha kwa sababu ya namna mlivyoupokea ujumbe wake. Ingawa tuliuleta kwenu, mliupokea si kama ujumbe unaotoka kwa wanadamu, bali kama ujumbe wa Mungu. Kweli hakika ni ujumbe kutoka kwa Mungu, unaofanya kazi kwenu ninyi mnao uamini.

14Kaka na dada zangu katika Bwana, mmeufuata mfano wa makanisa ya Mungu yaliyoko Uyahudi yaliyo mali ya Kristo Yesu. Nina maana ya kuwa ninyi mlitendewa vibaya na watu wa kwenu, namna ile ile walioamini wa Kiyahudi walivyotendewa vibaya na Wayahudi wenzao.[#2:14 Ni nchi ya kiyahudi ambako Yesu aliishi na kufundisha, pia ndipo mahali ambapo kanisa lilianzia.]

15Wayahudi wengine pia walimuua Bwana Yesu na manabii. Na walitulazimisha sisi kuondoka katika mji lenu. Hawampendezi Mungu, na wako kinyume na watu wengine wote.

16Na wanajaribu kutuzuia tusizungumze na wasio Wayahudi. Wanapofanya hivi wanawazuia watu wasio Wayahudi kuokoka. Na hivyo wanaendelea kuziongeza dhambi zao hata kujaza kipimo. Sasa wakati umefika kwa wao kuadhibiwa na hasira ya Mungu.

Shauku ya Paulo kuwa tembelea tena

17Kaka na dada zangu, tulikuwa kama yatima, tulitengwa nanyi kwa muda. Lakini hata kama hatukuwa pamoja nanyi, mawazo yetu yalikuwa bado yangali nanyi. Tulitamani sana kuwaona, na tulijitahidi sana kulitimiza hilo.

18Ndiyo, tulitamani kuja kwenu. Mimi, Paulo, nilijaribu zaidi ya mara moja kuja kwenu, lakini Shetani alituzuia.

19Ninyi ni tumaini letu, furaha yetu, na taji yetu tutakayojivunia wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu.

20Mnatuletea heshima na furaha.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International