Wafilipi 4

Wafilipi 4

Maagizo ya Mwisho

1Kaka na dada zangu wapenzi, ninawapenda na ninataka kuwaona. Mnanifurahisha na ninajivuna kwa sababu yenu. Endeleeni kuwa imara kumfuata Bwana kama nilivyowaambia.

2Ninawasihi Euodia na Sintike, ninyi nyote wawili ni wa Bwana, hivyo muwe na mtazamo mmoja.

3Kwa ajili ya hili ninamwomba rafiki yangu aliyetumika pamoja nami kwa uaminifu: Wasaidieni wanawake hawa. Waliwahubiri watu Habari Njema kwa bidii kama watendaji wenzangu tukiwa pamoja na Klementi na wengine waliofanya kazi pamoja nami. Majina yao yameandikwa katika kitabu cha uzima.[#4:3 Kitabu cha Mungu chenye majina ya wateule wake. Tazama Ufu 3:5; 21:27.]

4Furahini katika Bwana daima. Ninasema tena, furahini.

5Kila mtu auone wema na uvumilivu wenu. Bwana yu karibu kuja.

6Msisumbuke kitu chochote, lakini salini na kumwomba Mungu kwa mahitaji yenu. Mshukuruni Mungu wakati mnapomwomba yale mnayohitaji.

7Na kwa kuwa ninyi ni milki ya Kristo Yesu, amani ya Mungu itailinda mioyo na mawazo yenu isipate wasiwasi. Amani yake inaweza kutenda haya zaidi ya akili za kibinadamu.[#4:7 Yaani, “Inazidi (ni bora kuliko) akili zote”. Hii inaweza kumaanisha pia kuwa “Ni zaidi ya uelewa wote.”]

8Na sasa, mwisho kabisa, kaka na dada zangu, fikirini kuhusu yale yaliyo ya kweli, ya kuheshimiwa, ya haki, yaliyo safi, yenye kupendeza, na yanayosemwa vema.

9Yatendeni yale mliyojifunza na kupokea kutoka kwangu, niliyowaambia na yale mliyoyaona nikitenda. Na Mungu atoaye amani atakuwa pamoja nanyi.

Paulo Apokea Zawadi Kwa Furaha

10Nimefurahi sana katika Bwana kwa sababu mmeonesha tena kuwa mnanijali. Mmeendelea kujali juu yangu, lakini haikuwepo njia ya kuonesha hili.

11Ninawaambia hili, si kwa sababu ninahitaji msaada kutoka kwa yeyote. Nimejifunza kuridhika na kile nilichonacho na chochote kinachotokea.

12Ninajua namna ya kuishi ninapokuwa na vichache na ninapokuwa na vingi. Nimejifunza siri ya kuishi katika hali zote, ninapokuwa na vyakula vingi au ninapokuwa na njaa, ninapokuwa na vingi zaidi ya ninavyohitaji au ninapokuwa sina kitu.

13Kristo ndiye anayenitia nguvu kuyakabili mazingira yote katika maisha.

14Lakini mlifanya vyema mliposhiriki nami katika kipindi changu kigumu.

15Enyi watu wa Filipi kumbukeni nilipokuja mara ya kwanza kuwahubiri Habari Njema watu wa Makedonia. Nilipoondoka huko, ninyi ndiyo kanisa pekee ambalo lilishirikiana nami katika uhusiano ulioendelea wa kutoa na kupokea.

16Ukweli ni kuwa hata nilipokuwa Thesalonike, zaidi ya mara moja mlinitumia kila kitu nilichohitaji.

17Si kwamba natafuta msaada wa kifedha kutoka kwenu. Bali ninataka ninyi mpokee manufaa yanayozidi kukua yanayotokana na kutoa.

18Nina kila kitu ninachohitaji. Nina zaidi ya hata ninavyohitaji kwa sababu Epafrodito ameniletea kila kitu mlichompa aniletee. Zawadi zenu ni kama sadaka yenye harufu nzuri inayotolewa kwa Mungu. Ni sadaka anayoikubali, na inampendeza.

19Mungu wangu atatumia utajiri wake wenye utukufu kuwapa ninyi kila kitu mnachohitaji kupitia Kristo Yesu.

20Utukufu kwa Mungu na Baba yetu milele na milele. Amina.

21Wasalimuni watakatifu wote wa Mungu walio wake Kristo Yesu. Wale walio katika familia ya Mungu walio pamoja nami wanawasalimu.

22Na watu wote wa Mungu walio hapa wanawasalimu, hasa wale walio katika utumishi wa Kaisari.

23Neema ya Bwana Yesu Kristo iwe pamoja na utu wenu wa ndani.

Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi Toleo la Awali © 2017 Bible League International
Published by: Bible League International