Mhubiri 1

Mhubiri 1

Maisha ni bure kabisa

1Yafuatayo ni maneno ya Mhubiri mwana wa Daudi, aliyekuwa mfalme huko Yerusalemu.[#1:1 Kiebrania: Kohelethi.]

2Bure kabisa, bure kabisa,

nakuambia mimi Mhubiri!

Kila kitu ni bure kabisa!

3Binadamu hufaidi nini

kwa jasho lake lote hapa duniani?

4Kizazi chapita na kingine chaja,

lakini dunia yadumu daima.

5Jua lachomoza na kutua;

laharakisha kwenda machweoni.

6Upepo wavuma kusini,

wazunguka hadi kaskazini.

Wavuma na kuvuma tena,

warudia mzunguko wake daima.

7Mito yote hutiririkia baharini,

lakini bahari kamwe haijai;

huko ambako mito hutiririkia

ndiko huko inakotoka tena.

8Mambo yote husababisha uchovu,

uchovu mkubwa usioelezeka.

Jicho halichoki kuona,

wala sikio kusikia.

9Yaliyokuwako ndio yatakayokuwako,

yaliyotendeka ndio yatakayotendeka;

duniani hakuna jambo jipya.

10Watu husema, “Tazama jambo jipya,”

kumbe lilikwisha kuwako zama za kale.

11Hakuna mtu anayekumbuka ya zamani

wala atakayekumbuka yatakayotukia baadaye.

Aliyoyaona Mhubiri

12Mimi Mhubiri, nilikuwa mfalme wa Israeli, huko Yerusalemu.

13Nilipania kuchunguza na kutafuta kwa hekima kila kitu kinachotukia duniani. Hiyo ni taabu kubwa ambayo Mungu amewapa wanadamu.

14Nimeyaona yote yanayofanywa duniani; yote ni bure: Ni sawa na kufukuza upepo!

15Kilichopindika hakiwezi kunyoshwa,

kisichokuwapo hakiwezi kuhesabiwa.

16Basi, nikatafakari nikisema, “Nimejipatia hekima nyingi zaidi kupita wote waliopata kutawala Yerusalemu kabla yangu. Naam, nina uzoefu wa hekima na maarifa.”

17Nilipania kubainisha kati ya hekima, wazimu na upumbavu. Lakini niligundua kwamba kufanya hivyo ni sawa na kufukuza upepo.

18Maana katika kuwa na hekima nyingi mna wasiwasi;

na aongezaye maarifa zaidi huongeza huzuni zaidi.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania