Isaya 17

Isaya 17

Mungu ataadhibu Ashuru na Israeli

1Kauli ya Mungu dhidi ya Damasko.[#17:1-3 Taz Yer 49:23-27; Amo 1:3-5; Zek 9:1]

“Damasko utakoma kuwa mji;

utakuwa rundo la magofu.

2Mitaa yake imeachwa mahame milele.

Itakuwa makao ya makundi ya wanyama,

wala hakuna mtu atakayewatisha.

3Ngome za kujihami za Efraimu zitatoweka,

na utawala wa Damasko utakwisha.

Waashuru ambao watabaki hai,

watakuwa na fedheha kama wazawa wa Israeli.

Mimi Mwenyezi-Mungu wa majeshi nimenena.

Watakaosalia katika Israeli

4“Siku hiyo, fahari ya Yakobo itaporomoshwa,

na unono wake ataupoteza.

5Atakwisha kama shamba lililovunwa,

atafanyiwa kama mvunaji avunavyo nafaka,

atakuwa kama shamba lililovunwa bondeni Refaimu.

6Atabakiziwa wachache kama vile baada ya zeituni:

Zeituni mbili, tatu katika tawi la juu;

nne, tano katika matawi ya mti uzaao sana.

Mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli, nimenena.”

Mwisho wa kuabudu sanamu

7Siku hiyo, watu watamwangalia Muumba wao, na kuelekeza macho yao kwa huyo Mtakatifu wa Israeli.

8Hawatazielekea tena madhabahu ambazo ni kazi za mikono yao wenyewe, wala kuzitazamia tena kazi za mikono yao wenyewe, yaani sanamu za mungu Ashera na madhabahu za kufukizia ubani.

9Siku hiyo miji yao imara itaachwa mahame, kama miji ambayo Wahivi na Waamori waliihama walipokuwa wakiwakimbia wazawa wa Israeli. Kila kitu kitakuwa uharibifu.[#17:9 Kadiri ya Septuaginta; Kiebrania: Kama magofu ya msitu na kilele cha mlima.]

10Maana wewe Israeli umemsahau Mungu aliyekuokoa,

hukumkumbuka Mwamba wa usalama wako.

Kwa hiyo, hata mkipanda mimea ya Baali,

na kuiweka wakfu kwa mungu wa kigeni;

11hata mkiifanya ikue siku hiyohiyo mliyoipanda

na kuifanya ichanue asubuhi hiyohiyo,

mavuno yenu yatatoweka

siku hiyo ya balaa na maumivu yasiyoponyeka.

Mataifa adui yanashindwa

12Lo! Ngurumo ya watu wengi!

Wananguruma kama bahari.

Lo! Mlio wa watu wa mataifa!

Yanatoa mlio kama wa maji mengi.

13Mataifa yananguruma kama ngurumo ya maji mengi,

lakini Mungu atayakemea, nayo yatakimbilia mbali.

Yatafukuzwa kama makapi mlimani mbele ya upepo;

kama vumbi litimuliwalo na kimbunga.

14Wakati wa jioni yanaleta hofu kuu,

lakini kabla ya asubuhi yametoweka!

Hilo ndilo litakalowapata wanaonyakua mali yetu,

ndilo litakalowapata wanaotupora.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania