Isaya 31

Isaya 31

Misri haitaweza kusaidia

1Ole wao wale waendao Misri kuomba msaada,

ole wao wanaotegemea farasi,

wanaotegemea wingi wa magari yao ya vita,

na nguvu za askari wao wapandafarasi,

nao hawamtegemei Mtakatifu wa Israeli,

wala hawamwombi Mwenyezi-Mungu shauri!

2Mungu ni mwenye busara na huleta maangamizi.

Habadilishi tamko lake;

ila yuko tayari kuwakabili watu waovu

kadhalika na wasaidizi wa watendao mabaya.

3Wamisri ni binadamu tu wala si Mungu;

farasi wao nao ni wanyama tu, si roho.

Mwenyezi-Mungu akiunyosha mkono wake,

taifa linalotoa msaada litajikwaa,

na lile linalosaidiwa litaanguka;

yote mawili yataangamia pamoja.

Mungu ataulinda mji wa Yerusalemu

4Mwenyezi-Mungu aliniambia:

“Kama vile simba au mwanasimba angurumavyo

kuyakinga mawindo yake,

hata kundi la wachungaji likiitwa kumkabili,

yeye hatishiki kwa kelele zao,

wala hashtuki kwa sauti zao.

Ndivyo atakavyoshuka Mwenyezi-Mungu wa majeshi

kupigana juu ya mlima Siyoni na kilima chake.

5Kama ndege arukavyo juu ya viota vyake,

ndivyo Mwenyezi-Mungu atakavyoulinda Yerusalemu,

ataulinda na kuukomboa,

atauhifadhi na kuuokoa.

6Enyi Waisraeli,

mrudieni huyo mliyemsaliti vibaya.

7Wakati utafika ambapo nyote

mtavitupilia mbali vinyago vyenu

vya fedha na dhahabu ambavyo

mmejitengenezea kwa mikono yenu,

vikawakosesha.

8Hapo Waashuru watauawa kwa upanga,

lakini si kwa upanga wa binadamu;

naam, wataangamizwa kwa upanga

ambao ni zaidi ya ule wa binadamu.

Waashuru watakimbia

na vijana wao watafanyizwa kazi za kitumwa.

9Mfalme wao atatoroka kwa hofu,

na maofisa wao wataiacha bendera yao kwa woga.

Hayo ameyatamka Mwenyezi-Mungu

ambaye moto wake umo mjini Siyoni,

naam, tanuri lake limo mjini Yerusalemu.”

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania