Isaya 52

Isaya 52

Mungu ataikomboa Yerusalemu

1Amka! Amka![#52:1 Taz Ufu 21:2,27]

Jipe nguvu zako ewe mji wa Siyoni!

Jivike mavazi yako mazuri,

ewe Yerusalemu, mji mtakatifu.

Maana hawataingia tena kwako

watu wasiotahiriwa na walio najisi.

2Jikungute mavumbi, uinuke

ewe Yerusalemu uliyetekwa nyara!

Jifungue minyororo yako shingoni,

ewe binti Siyoni uliyechukuliwa mateka.

3Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Nyinyi mliuzwa utumwani bila malipo yoyote, na mtakombolewa bila kulipa hata senti moja.

4Tena mwanzoni nyinyi watu wangu mlikimbilia Misri mkakaa huko. Halafu baadaye Waashuru waliwakandamiza bila sababu yoyote.

5Katika hali ya sasa napata faida gani kuwaona watu wangu wamepelekwa utumwani? Hao wanaowatawala wanajitapa. Nalo jina langu laendelea kudharauliwa kila siku.[#52:5 Taz Rom 2:24]

6Kwa hiyo watu wangu watajua mimi ni nani; siku hiyo watajua kwamba ni mimi ninayesema: Niko!”

7Tazama inavyopendeza[#52:7 Taz Nah 1:15; Rom 10:15; Efe 6:15]

kumwona mjumbe akitokea mlimani,

ambaye anatangaza amani,

ambaye analeta habari njema,

na kutangaza ukombozi!

Anauambia mji wa Siyoni:

“Mungu wako anatawala!”

8Sikiliza sauti ya walinzi wako;

wanaimba pamoja kwa furaha,

maana wanaona kwa macho yao wenyewe,

kurudi kwa Mwenyezi-Mungu mjini Siyoni.

9Pazeni sauti za shangwe, enyi magofu ya Yerusalemu!

Mwenyezi-Mungu amewafariji watu wake,

ameukomboa mji wa Yerusalemu.

10Mwenyezi-Mungu ameonesha nguvu yake tukufu,

mbele ya mataifa yote.

Atawaokoa watu wake,

na ulimwengu wote utashuhudia.

11Ondokeni! Ondokeni! Tokeni hapa;[#52:11 Taz 2Kor 6:17]

msiguse kitu chochote najisi!

Ondokeni huku Babuloni!

Jitakaseni enyi mbebao vyombo vya Mwenyezi-Mungu.

12Safari hii hamtatoka kwa haraka,

wala hamtaondoka mbiombio!

Maana Mwenyezi-Mungu atawatangulieni,

Mungu wa Israeli atawalinda kutoka nyuma.

Mtumishi wa Mwenyezi-Mungu

13Mungu asema hivi:

“Mtumishi wangu atafanikiwa;

atatukuzwa na kupewa cheo,

atapata heshima kuu.

14Wengi waliomwona walishtuka,

kwa vile sura yake ilikuwa imeharibiwa;

hakuwa tena na umbo la kibinadamu!

15Lakini sasa ameyashangaza mataifa mengi.[#52:15 Taz Rom 15:21]

Wafalme wanaduwaa kwa sababu yake,

maana wataona mambo ambayo hawajapata kuambiwa,

na kufahamu mambo ambayo hawajapata kusikia.”

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania