The chat will start when you send the first message.
1Nani aliyeamini mambo tuliyosikia?[#53:1 Taz Yoh 12:38; Rom 10:16]
Nani aliyetambua kuwa mkono wa Mwenyezi-Mungu ulihusika?
2Maana, mbele yake Mwenyezi-Mungu,
mtumishi wake alikua kama mti mchanga,
kama mzizi katika nchi kavu.
Hakuwa na umbo wala sura ya kutupendeza,
wala hakuwa na uzuri wowote wa kutuvutia.
3Alidharauliwa na kukataliwa na watu,
alikuwa mtu wa uchungu na huzuni.
Alikuwa kama mtu kinyaa kwa watu;
alidharauliwa na tukamwona si kitu.
4Hata hivyo alivumilia majonzi yetu,[#53:4 Taz Mat 8:17]
na kubeba huzuni zetu.
Sisi tulifikiri amepata adhabu,
amepigwa na Mungu na kuteswa.
5Lakini alijeruhiwa kwa sababu ya dhambi zetu,[#53:5 Taz 1Pet 2:24]
aliumizwa kwa sababu ya maovu yetu.
Kwa kuadhibiwa kwake sisi tumepata uhai;
kwa kupigwa kwake sisi tumepona.
6Sisi sote tumepotea kama kondoo,[#53:6 Taz 1Pet 2:25]
kila mmoja wetu ameelekea njia yake.
Lakini Mwenyezi-Mungu alimtwika adhabu,
ambayo sisi wenyewe tuliistahili.
7Alidhulumiwa na kuteswa,[#53:7 Taz Ufu 5:6]
lakini alivumilia kwa unyenyekevu,
bila kutoa sauti hata kidogo.
Alikuwa kama mwanakondoo apelekwaye machinjoni,
kama kondoo akaavyo kimya anapokatwa manyoya.
Hakutoa sauti hata kidogo.
8Alidhulumiwa, akahukumiwa na kupelekwa kuuawa;
na hakuna mtu aliyejali yanayompata.
Alifukuzwa kutoka nchi ya walio hai,
kwa sababu ya makosa ya watu wangu.
9Walimzika pamoja na wahalifu;[#53:9 Taz 1Pet 2:22]
katika kifo aliwekwa pamoja na matajiri,
ingawa hakutenda ukatili wowote,
wala hakusema neno lolote la udanganyifu.
10Mwenyezi-Mungu alipenda kumwumiza
na kumweka katika huzuni.
Alijitoa mhanga kwa ajili ya kuondoa dhambi.
Mtumishi wa Mungu atakuwa na wazawa;
ataishi maisha marefu.
Yeye ndiye atakayetimiza mpango wa Mwenyezi-Mungu.
11Mungu asema:
“Baada ya kutaabika sana,
mtumishi wangu atafurahi.
Kwa kuwajibika kwake kikamilifu,
atatosheka na matokeo hayo.
Kwa maarifa yake mtumishi wangu mwadilifu
atawafanya wengi wawe waadilifu
Yeye atazibeba dhambi zao.
12Kwa hiyo, nitamweka katika cheo cha wakuu,
atagawa nyara pamoja na wenye nguvu;
kwa kuwa alijitolea mwenyewe kufa,
akawekwa katika kundi moja na wakosefu,
alizibeba dhambi za watu wengi,
akawaombea msamaha hao wakosefu.”