Isaya 54

Isaya 54

Upendo wa Mungu kwa Israeli

1Mwenyezi-Mungu asema hivi:

“Imba kwa shangwe ewe uliye tasa,

wewe ambaye hujapata kuzaa!

Paza sauti na kuimba kwa nguvu,

wewe usiyepata kujifungua mtoto.

Maana watoto wako wewe uliyeachwa

watakuwa wengi kuliko wa aliye na mume.

2Panua nafasi hemani mwako,

tandaza mapazia hapo unapoishi,

usijali gharama zake.

Zirefushe kamba zake,

na kuimarisha vigingi vyake;

3maana utapanuka kila upande;

wazawa wako watamiliki mataifa,

miji iliyokuwa mahame itajaa watu.

4Usiogope maana hutaaibishwa tena;

usifadhaike maana hutadharauliwa tena.

Utaisahau aibu ya ujana wako,

wala hutaikumbuka tena fedheha ya ujane wako.

5Muumba wako atakuwa mume wako;

Mwenyezi-Mungu wa majeshi, ndilo jina lake,

Mtakatifu wa Israeli ndiye Mkombozi wako;

yeye aitwa ‘Mungu wa ulimwengu wote’.

6“Yerusalemu, Mwenyezi-Mungu amekuita tena wewe

kama vile mke aliyeachwa na kuhuzunika,

mke aliyeolewa akiwa kijana akaachwa.

Mungu wako anasema:

7Nilikuacha kwa muda mfupi tu;

kwa huruma nyingi, nitakurudisha.

8Kwa hasira nyingi nilikuficha uso wangu kwa kitambo,

lakini kwa fadhili za milele nitakuonea huruma.

Mimi Mwenyezi-Mungu Mkombozi wako, nimesema.

9“Nitafanya kama nilivyofanya wakati wa Noa:[#54:9 Taz Mwa 9:8-17]

Wakati ule niliapa kwamba

sitaifunika tena ardhi kwa gharika.

Basi sasa naapa kwamba sitakukasirikia tena

wala sitakukemea tena.

10Milima yaweza kutoweka,

vilima vyaweza kuondolewa,

lakini fadhili zangu hazitakuondoka,

agano langu la amani halitaondolewa.

Mimi Mwenyezi-Mungu nikuhurumiaye nimesema.

Yerusalemu mpya

11“Ewe Yerusalemu uliyeteseka,[#54:11-12 Taz Ufu 12:18-21]

uliyetaabishwa na kukosa wa kukufariji!

Nitakujenga upya kwa mawe ya thamani,

misingi yako itakuwa ya johari ya rangi ya samawati.

12Minara yako nitaijenga kwa mawe ya akiki,

malango yako kwa almasi,

na ukuta wako kwa mawe ya thamani.

13“Watu wako watafunzwa nami Mwenyezi-Mungu,[#54:13 Taz Yoh 6:45]

wanao watapata ustawi mwingi.

14Utaimarika katika uadilifu,

utakuwa mbali na dhuluma,

nawe hutaogopa kitu;

utakuwa mbali na hofu,

maana haitakukaribia.

15Mtu yeyote akija kukushambulia,

hatakuwa ametumwa nami.

Yeyote atakayekushambulia,

ataangamia mbele yako.

16“Tazama, mimi ndiye niliyemuumba mhunzi,

afukutaye moto wa makaa na kufua silaha.

Ni mimi pia niliyemuumba mwangamizi anayeangamiza.

17Silaha zote zilizoundwa kukudhuru wewe

hazitafaa chochote kile.

Mtu akikushtaki mahakamani, utamshinda.

Hilo ndilo fungu nililowapangia watumishi wangu.

Hizo ndizo haki nilizowathibitishia.

Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania