Isaya 9

Isaya 9

Mtoto amezaliwa kwetu

1Lakini nchi ile iliyokuwa imekumbwa na huzuni haitabaki daima katika giza hilo kuu. Hapo awali Mungu alizifedhehesha nchi za Zebuluni na Naftali, lakini siku za usoni ataifanikisha sehemu hii ya baharini na nchi iliyo ngambo ya Yordani na hata Galilaya wanamoishi watu wa mataifa.[#9:1 Taz Mat 4:15]

2Watu waliotembea gizani[#9:2 Taz Mat 4:16; Luka 1:79]

wameona mwanga mkubwa.

Watu walioishi katika nchi ya giza kuu,

sasa mwanga umewaangazia.

3Wewe, ee Mungu, umelikuza taifa,

umeiongeza furaha yake.

Watu wanafurahi mbele yako,

wana furaha kama wakati wa mavuno,

kama wafurahivyo wanaogawana nyara.

4Maana nira nzito walizobeba,

nira walizokuwa wamefungwa,

na fimbo ya wanyapara wao,

umezivunjavunja kama wakati wa Wamidiani.

5Viatu vyote vya washambulizi vitani

na mavazi yote yenye madoa ya damu

yatateketezwa kama kuni za kuwasha moto.

6Maana mtoto amezaliwa kwa ajili yetu,

tumepewa mtoto wa kiume.

Naye atapewa mamlaka ya kutawala.

Ataitwa: “Mshauri wa Ajabu”.

“Mungu Mwenye Nguvu”,

“Baba wa Milele”,

“Mfalme wa Amani”.

7Utawala wake utastawi daima,[#9:7 Taz Luka 1:32-33]

amani ya ufalme wake haitakoma.

Atachukua wadhifa wa mfalme Daudi

na kutawala juu ya ufalme wake;

ataustawisha na kuuimarisha,

kwa haki na uadilifu,

tangu sasa na hata milele.

Hayo atayafanya Mwenyezi-Mungu wa majeshi.

Adhabu ya Waisraeli

8Mwenyezi-Mungu ametoa tamko dhidi ya Yakobo

nalo litampata Israeli.

9Watu wote watatambua,

ukoo wote wa Efraimu

na wakazi wa Samaria.

Kwa kiburi na majivuno wanasema:

10“Kuta za matofali zimeanguka

lakini sisi tutazijenga kwa mawe yaliyochongwa!

Nyumba za boriti za mikuyu zimeharibiwa

lakini mahali pake tutajenga za mierezi.”

11Basi, Mwenyezi-Mungu atawaletea wapinzani

na kuwachochea maadui zao.

12Waaramu upande wa mashariki,

Wafilisti upande wa magharibi,

wamepanua vinywa vyao kuimeza Israeli.

Hata hivyo, hasira yake haijatulia,

bado ameunyosha mkono wake.

13Ingawa aliwaadhibu watu,

hawakumrudia Mwenyezi-Mungu wa majeshi.

14Basi kwa muda wa siku moja tu,

Mwenyezi-Mungu atakata katika Israeli vichwa na mikia,

tawi la mtende na nyasi:

15Vichwa ndio wazee na waheshimiwa,

mikia ndio manabii wafundishao uongo.

16Wale wanaoongoza watu hawa wamewapotosha,

na hao wanaoongozwa nao wamepotoka.

17Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu hawahurumii vijana wao,[#9:17 Kufuatana na hati moja ya kale. Kiebrania: Hapendezwi.]

hana huruma juu ya yatima na wajane wao;

kwani hakuna hata mmoja amchaye Mungu,

kila mtu husema uongo.

Hata hivyo, hasira yake haijatulia,

bado ameunyosha mkono wake.

18Uovu huwaka kama moto

uteketezao mbigili na miiba;

huwaka kama moto msituni,

na kutoa moshi mzito upandao angani juu.

19Kwa ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu wa majeshi

nchi imechomwa moto,

na watu ni kama kuni za kuuwasha.

Hakuna mtu anayemhurumia ndugu yake;

20wananyanganya upande mmoja na hawatosheki;

wanakula upande mwingine lakini hawashibi.

Kila mmoja anamshambulia mwenzake.

21Manase dhidi ya Efraimu,

Efraimu dhidi ya Manase

na wote wawili dhidi ya Yuda.

Hata hivyo, hasira ya Mwenyezi-Mungu haijatulia,

bado ameunyosha mkono wake.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania