The chat will start when you send the first message.
1Kisha Yobu akajibu:
2“Aa! Jinsi gani ulivyomsaidia asiye na uwezo!
Jinsi gani ulivyomwokoa asiye na nguvu!
3Jinsi gani ulivyomshauri asiye na hekima,
na kumshirikisha ujuzi wako!
4Lakini umetamka hayo kwa ajili ya nani?
Nani aliyekusukuma kuongea hivyo?”
Bildadi akajibu:
5“Mizimu huko chini yatetemeka,
maji ya chini na wakazi wake yaogopa.
6Kuzimu kuko wazi kabisa mbele ya Mungu.
Abadoni haina kifuniko chochote.
7Mungu hutandaza kaskazini mahali patupu,
na hutundika dunia mahali pasipo na kitu,
8huyafunga maji mawinguni yawe mazito,
nayo mawingu hayapasuki kwa uzito wake.
9Huufunika uso wa mwezi
na kutandaza juu yake wingu.
10Amechora duara juu ya uso wa bahari,
penye mpaka kati ya mwanga na giza.
11Mungu akitoa sauti ya kukemea,
nguzo za mbingu hutetemeka na kustaajabu.
12Kwa nguvu zake aliituliza bahari;
kwa maarifa yake alimwangamiza dude Rahabu.
13Kwa pumzi yake aliisafisha anga;
mkono wake ulilichoma joka lirukalo.
14Yamkini haya ni machache tu ya matendo yake,
ni minongono tu tunayosikia juu yake.
Nani awezaye kujua ukuu wa nguvu yake?”