The chat will start when you send the first message.
1Mwenyezi-Mungu alimwambia Mose,
2“Waamuru watu wa Israeli wakuletee mafuta safi kwa ajili ya taa ili taa hiyo iendelee kuwaka daima.
3Aroni ataiweka taa hiyo ndani ya hema la mkutano, nje ya pazia la sanduku la maamuzi ili ipate kuwaka mbele yangu tangu usiku mpaka asubuhi. Hili ni sharti la kufuata milele katika vizazi vyenu.[#24:3 Au agano; Kiebrania: Edut.]
4Ataziweka hizo taa katika kinara cha taa cha dhahabu safi ziwake daima mbele ya Mwenyezi-Mungu.
5“Chukua unga laini, kilo kumi na mbili na kuoka mikate kumi na miwili.[#Taz Kut 25:30]
6Mikate hiyo itapangwa safu mbili juu ya meza ya dhahabu safi, kila safu mikate sita.
7Kila safu utaitia ubani safi ili iambatane na mikate hiyo, na kuwa sehemu ya sadaka ya kuteketezwa ya ukumbusho kwa Mwenyezi-Mungu.
8Kila siku ya Sabato Aroni ataipanga sawasawa katika safu mbele yangu mimi Mwenyezi-Mungu kwa niaba ya watu wa Israeli kama agano la milele.
9Aroni na wazawa wake peke yao ndio wanaoruhusiwa kula mikate hiyo kwani ni mitakatifu kabisa kwa sababu ni sehemu ya sadaka ninazotolewa mimi Mwenyezi-Mungu kwa moto. Hiyo ni haki yao milele.”[#Taz Mat 12:4; Marko 2:26; Luka 6:4]
10Siku moja kukatokea mzozo huko kambini kati ya Mwisraeli mmoja na kijana mmoja wa mama Mwisraeli aitwaye Shelomithi lakini baba Mmisri.
11Siku moja yule kijana ambaye mama yake aliitwa Shelomithi binti Dibri wa kabila la Dani, alilikufuru na kulilaani jina la Mungu. Basi watu walimpeleka kijana kwa Mose,
12wakamtia ndani mpaka hapo watakapofunuliwa matakwa ya Mwenyezi-Mungu.
13Basi, Mwenyezi-Mungu akamwambia Mose,
14“Mtoe kijana aliyekufuru nje ya kambi, na wale wote waliomsikia akikufuru waweke mikono yao juu ya kichwa chake, na jumuiya yote imuue kwa kumpiga mawe.
15Nawe uwaambie Waisraeli kwamba mtu yeyote atakayemlaani Mungu wake ni lazima awajibike kwa dhambi yake.
16Mtu yeyote awe ni mwenyeji au mgeni anayemkufuru Mwenyezi-Mungu, jumuiya nzima itamuua kwa kumpiga mawe.
17Mtu yeyote anayeua mtu mwingine ni lazima naye auawe.[#Taz Kut 21:12]
18Mtu yeyote anayeua mnyama ni lazima atoe fidia: Uhai kwa uhai.
19Mtu yeyote anayemwumiza jirani, ni lazima naye aumizwe kulingana na kiasi alichomwumiza jirani yake,[#Taz Kut 21:12]
20amemvunja mfupa naye atavunjwa mfupa, jicho kwa jicho, jino kwa jino. Kila mtu anayemwumiza mwenzake ni lazima naye aumizwe kulingana na tendo lake.[#Taz Kut 21:23-25; Kumb 19:21; Mat 5:38]
21Anayemuua mnyama ni lazima atoe fidia; lakini mtu yeyote akimuua mtu mwingine ni lazima naye auawe.
22Sheria hii yamhusu mgeni na mwenyeji. Mimi ndimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu.”[#Taz Hes 15:16]
23Basi, Mose akawaambia Waisraeli hayo yote. Wakampeleka yule mtu aliyemlaani Mwenyezi-Mungu nje ya kambi, wakamuua kwa kumpiga mawe. Ndivyo Waisraeli walivyofanya kama Mwenyezi-Mungu alivyomwamuru Mose.