Mika 2

Mika 2

Mika na wapinzani wake

1Ole wao wanaopanga kutenda maovu

wanaolala usiku wakiazimia uovu!

Mara tu kunapopambazuka,

wanayatekeleza kwani wanao uwezo.

2Hutamani mashamba na kuyatwaa;

wakitaka nyumba, wananyakua.

Huwadhulumu wenye nyumba na jamaa zao,

huwanyang'anya watu mali zao.

3Kwa hiyo, Mwenyezi-Mungu asema hivi:

“Ninapanga kuwaleteeni nyinyi maafa,

ambayo kamwe hamtaweza kuyakwepa.

Utakuwa wakati mbaya kwenu,

wala hamtaweza kwenda kwa maringo.

4Siku hiyo watu watawasimanga kwa wimbo,

watalia na kuomboleza kwa uchungu, wakisema:

‘Tumeangamia kabisa;

Mwenyezi-Mungu amechukua nchi yetu,

naam, ameiondoa mikononi mwetu.

Mashamba yetu amewagawia waliotuteka.’”

5Kwa hiyo hamtagawiwa sehemu yoyote ya ardhi

miongoni mwa watu wake Mwenyezi-Mungu.

Wapinzani wa nabii

6“Usituhubirie sisi.

Mambo kama hayo si ya kuhubiriwa.

Sisi hatutakumbwa na maafa!

7Je, yafaa kusema hivyo, wazawa wa Yakobo?

Je, Mwenyezi-Mungu ameacha uvumilivu wake?

Je, yeye hufanya mambo kama haya?”

Mika

Sivyo! Maneno yangu huwafaa watendao mambo mema.

8Lakini Mwenyezi-Mungu awaambia hivi:

“Nyinyi mnawavamia watu wangu kama adui.

Mnawanyang'anya mavazi yao watu watulivu;

watu wanaopita kwenda zao bila wasiwasi,

na wasio na fikira zozote za vita.

9Mnawafukuza wake za watu wangu

kutoka nyumba zao nzuri;

watoto wao mmewaondolea fahari yangu milele.

10Inukeni mwende zenu!

Hapa hamna tena pa kupumzika!

Kwa utovu wenu wa uaminifu

maangamizi makubwa yanawangojea!

11Kama mtu angetokea akatamka maneno matupu ya uongo

na kusema: ‘Nawatabirieni divai na pombe kwa wingi’,

mhubiri wa namna hiyo angependwa na watu hawa!

12“Lakini kweli nitawakusanya nyote enyi watu wa Yakobo,

naam, nitawakusanya enyi Waisraeli mliobaki,

niwalete pamoja kama kondoo katika zizi,

kama kundi kubwa la kondoo malishoni;

nanyi mtakuwa kundi la watu wengi.”

13Yule atakayetoboa njia atawatangulia,

nao watalivunja lango la mji na kutoka nje,

watapita na kutoka nje.

Mfalme wao atawatangulia;

Mwenyezi-Mungu mwenyewe atawatangulia.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania