Zaburi 112

Zaburi 112

Furaha ya mtu mwema

1Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Heri mtu anayemcha Mwenyezi-Mungu,

anayefurahia sana kutii amri zake.

2Wazawa wake watakuwa wenye nguvu nchini;

watoto wa wanyofu watapata baraka.

3Nyumbani kwake kutakuwa na mali nyingi;

uadilifu wake wadumu milele.

4Mtu mwema huangaziwa mwanga gizani;

mtu mwenye huruma, mpole na mwadilifu.

5Mtu mkarimu akopeshaye bila faida, hufanikiwa;

mtu afanyaye shughuli zake kwa kutumia haki.

6Mwadilifu hatashindwa kamwe,

huyo atakumbukwa milele.

7Hana haja ya kuogopa akipata habari mbaya;

ana moyo thabiti na humtegemea Mwenyezi-Mungu.

8Yuko imara moyoni, wala hataogopa;

naye atawaona maadui zake wanashindwa.

9Hutoa kwa ukarimu, huwapa maskini;[#Taz 2Kor 9:9]

uadilifu wake wadumu milele.

Nguvu yake inatukuzwa kwa heshima.

10Watu waovu huona hayo na kuudhika;

husaga meno kwa chuki na kutoweka,

matazamio ya mtu mbaya huishia patupu.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania