Zaburi 116

Zaburi 116

Shukrani kwa kuokolewa kifoni

1Nampenda Mwenyezi-Mungu,

kwa maana anisikia,

maana amesikia kilio cha ombi langu.

2Yeye amenitegea sikio,

hivyo nitamwomba muda wote niishio.

3Hatari ya kifo ilinizunguka,

vitisho vya kaburi vilinivamia;

nilijawa na mahangaiko na majonzi.

4Kisha nikamlilia Mwenyezi-Mungu:

“Ee Mwenyezi-Mungu, tafadhali unisalimishe!”

5Mwenyezi-Mungu amejaa wema na uaminifu;

Mungu wetu ni mwenye huruma.

6Mwenyezi-Mungu huwalinda wanyofu;

nilipokuwa nimekandamizwa aliniokoa.

7Uwe na utulivu mkuu, ee nafsi yangu,

maana Mwenyezi-Mungu amenitendea mema.

8Ameniokoa kifoni na kufuta machozi yangu;

akanilinda nisije nikaanguka.

9Nitatembea mbele yake Mwenyezi-Mungu,

katika nchi ya watu walio hai.

10Nilikuwa na imani hata niliposema:[#Taz 2Kor 4:13]

“Mimi nimetaabika mno.”

11Hata nilisema kwa hofu yangu:

“Binadamu wote hawaaminiki!”

12Nimrudishie nini Mwenyezi-Mungu,

kwa ukarimu wote alionitendea?

13Nitamtolea tambiko ya divai kwa kunikomboa,

nitaomba kwa jina lake Mwenyezi-Mungu.

14Nitamtimizia Mwenyezi-Mungu nadhiri zangu,

mbele ya watu wake wote.

15Kifo cha waaminifu wake Mwenyezi-Mungu

si jambo dogo mbele yake.

16Ee Mwenyezi-Mungu, mimi ni mtumishi wako;

ni mtumishi wako, mtoto wa mjakazi wako;

umenifungulia vifungo vyangu.

17Nitakutolea tambiko za shukrani,

na kukupa heshima zangu.

18Nitakutimizia ahadi zangu, ee Mwenyezi-Mungu

mbele ya watu wako wote,

19waliokusanyika hekaluni mwako,

katikati ya Yerusalemu.

Msifuni Mwenyezi-Mungu!

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania