Zaburi 57

Zaburi 57

Kuomba msaada

1Unihurumie, ee Mungu, unihurumie,

maana kwako nakimbilia usalama.

Kivulini mwa mabawa yako nitakimbilia usalama,

hata hapo dhoruba ya maangamizi itakapopita.

2Namlilia Mungu Mkuu,

Mungu anikamilishiaye nia yake.

3Atanipelekea msaada toka mbinguni na kuniokoa;

atawaaibisha hao wanaonishambulia.

Mungu atanionesha fadhili zake na uaminifu wake!

4Mimi nimezungukwa na maadui,

wenye uchu wa damu kama simba;

meno yao ni kama mikuki na mishale,

ndimi zao ni kama panga kali.

5Utukuzwe, ee Mungu, juu ya mbingu!

Utukufu wako uenee duniani kote!

6Maadui wamenitegea wavu waninase,

nami nasononeka kwa huzuni.

Wamenichimbia shimo njiani mwangu,

lakini wao wenyewe wametumbukia humo.

7Niko thabiti moyoni, ee Mungu,

naam, niko thabiti moyoni;

nitaimba na kukushangilia!

8Amka, ee nafsi yangu!

Amkeni, enyi kinubi na zeze!

Nitayaamsha mapambazuko!

9Ee Bwana, nitakushukuru kati ya mataifa;

nitakuimbia sifa kati ya mataifa.

10Fadhili zako zaenea hata juu ya mbingu,

uaminifu wako wafika hata mawinguni.

11Utukuzwe, ee Mungu, juu ya mbingu!

Utukufu wako uenee duniani kote!

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania