Isaya 16

Isaya 16

Moabu inaomba msaada kutoka Yerusalemu

1Pelekeni wanakondoo kwa mtawala wa nchi,

pelekeni kutoka Sela jangwani mpaka mlimani Siyoni.

2Kama ndege wanavyohangaika na kurukaruka,

wakiwa wamefukuzwa kutoka viota vyao,

ndivyo walivyo mabinti wa Moabu

kwenye vivuko vya Arnoni.

3Wamoabu wanawaambia watu wa Yuda,

“Tupeni mwongozo, tuamulieni.

Enezeni ulinzi wenu juu yetu,

kama vile usiku uenezavyo kivuli chake.

Tuficheni sisi wakimbizi;

msitusaliti sisi tuliofukuzwa.

4Wakimbizi wa Moabu waishi kwenu,

muwe kimbilio lao mbali na mwangamizi.”

Mdhalimu atakapokuwa ametoweka,

udhalimu utakapokuwa umekoma,

na wavamizi kutoweka nchini,

5utawala adili utazinduliwa katika maskani ya Daudi,

mtawala apendaye kutenda haki,

na mwepesi wa kufanya yaliyo sawa;

atatawala humo kwa uaminifu.

6Watu wa Yuda wanasema hivi:

“Tumesikia juu ya kiburi cha Moabu,

tunajua jinsi alivyojivuna mno;

tumesikia juu ya majivuno, kiburi na ufidhuli wake;

lakini majivuno yake hayo ni bure.”

7Sasa Wamoabu wanalia;

wote wanaomboleza juu ya nchi yao.

Ombolezeni kwa pigo hilo kubwa,

na juu ya maandazi ya zabibu za Kir-haresethi.

8Mashamba ya Heshboni yamefifia.

Kadhalika na zabibu za Sibma

ambazo ziliwalevya wakuu wa mataifa

zikafika Yazeri na kusambaa hata jangwani,

chipukizi zake zikafika hata ngambo ya bahari.

9Kwa hiyo ninalia pamoja na Yazeri

kwa ajili ya mizabibu ya Sibma.

Machozi yananitoka kwa ajili yenu,

enyi miji ya Heshboni na Eleale;

maana vigelegele vya mavuno ya matunda,

vigelegele vya mavuno ya nafaka vimetoweka.

10Furaha na shangwe zimetoweka katika shamba la rutuba.

Kwenye mizabibu hakuna kuimba tena,

wala kupiga vigelegele.

Hakuna tena kukamua zabibu shinikizoni,

sauti za furaha za mavuno zimekomeshwa.

11Hivyo, nafsi yangu yalilia Moabu kama kinubi,

na moyo wangu kwa ajili ya mji wa Kir-heresi.

12Watu wa Moabu wanapojitokeza kuabudu mungu wao,

wanapojichosha huko juu mahali pa ibada,

wanapokwenda mahali pao patakatifu kusali,

hawatakubaliwa.

13Hili ndilo jambo alilosema Mwenyezi-Mungu wakati uliopita kuhusu Moabu.

14Lakini sasa Mwenyezi-Mungu asema hivi: “Baada ya miaka mitatu kamili, ikihesabiwa kama mfanyakazi anavyohesabu siku zake, fahari ya Moabu itakwisha. Ingawa watu wake ni wengi, watakaobaki hai watakuwa wachache na wanyonge.”

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania