Isaya 26

Isaya 26

Wimbo wa ushindi

1Siku ile watu wataimba wimbo huu katika nchi ya Yuda:

Sisi tuna mji imara:

Mungu anatulinda kwa kuta na ngome.

2Fungueni malango ya mji,

taifa aminifu liingie;

taifa litendalo mambo ya haki.

3Ee Mungu, wawaweka katika amani walio thabiti,

wawaweka katika amani kwa kuwa wanakutegemea.

4Mtumaini Mwenyezi-Mungu siku zote

kwa maana yeye ni mwamba wa usalama milele.

5Amewaporomosha waliokaa pande za juu,

mji maarufu ameuangusha mpaka chini,

ameutupa mpaka mavumbini.

6Sasa mji huo unakanyagwakanyagwa

kwa miguu ya watu maskini na fukara.

7Njia ya watu wanyofu ni rahisi;

ewe Mungu mwadilifu, wasawazisha njia yao.

8Katika njia ya maamuzi yako

tunakungojea ee Mwenyezi-Mungu;

kulikumbuka jina lako ndiyo tamaa yetu.

9Moyo wangu wakutamani usiku kucha,

nafsi yangu yakutafuta kwa moyo.

Utakapoihukumu dunia,

watu wote ulimwenguni watajifunza haki.

10Lakini waovu hata wakipewa fadhili,

hawawezi kujifunza kutenda haki.

Hata katika nchi ya wanyofu,

wao bado wanatenda maovu,

wala hawajali ukuu wako wewe Mwenyezi-Mungu.

11Ee Mwenyezi-Mungu umeinua mkono kuwaadhibu,[#26:11 Taz Ebr 10:27]

lakini maadui zako hawauoni.

Waoneshe uwapendavyo watu wako nao wataaibika.

Moto wa hasira yako uwateketeze maadui zako!

12Wewe, ee Mwenyezi-Mungu, umetupatia amani;

umefanikisha shughuli zetu zote.

13Ee Mwenyezi-Mungu, Mungu wetu,

tulipata kutawaliwa na watu wengine na miungu yao,

lakini twakiri wewe pekee kuwa Mungu wetu.

14Watu hao wamekufa, wala hawataishi tena;

wamekuwa mizimu, wala hawatafufuka.

Maana wewe umewaadhibu na kuwaangamiza,

hakuna atakayeweza kuwakumbuka tena.

15Umelikuza taifa letu, ee Mwenyezi-Mungu,

naam, umelizidisha taifa letu.

Umeipanua mipaka yote ya nchi,

kwa hiyo wewe watukuka.

16Ee Mwenyezi-Mungu, walipotaabika walikutafuta,

walikuomba msaada ulipowaadhibu.

17Kama vile mama mjamzito anayejifungua

hulia na kugaagaa kwa uchungu,

ndivyo tulivyokuwa kwa sababu yako, ee Mwenyezi-Mungu.

18Sisi tulipata maumivu ya kujifungua

lakini tukajifungua tu upepo!

Hatukupata ushindi wowote kwa ajili ya nchi yetu,

hatukuweza kuongeza idadi ya watu katika nchi.

19Wafu wako wataishi tena,[#26:19 Taz Dan 12:2]

miili yao itafufuka.

Wanaolala mavumbini wataamka na kuimba kwa furaha!

Mungu atapeleka umande wake wa uhai,

nao walio kwa wafu watatoka hai.

Baada ya dhiki faraja

20Njoni watu wangu, ingieni majumbani mwenu,

mkajifungie humo ndani.

Jificheni kwa muda mfupi,

mpaka ifike ghadhabu ya Mwenyezi-Mungu.

21Maana Mwenyezi-Mungu aja kutoka kwake juu,

kutoka makao yake huko mbinguni;

kuwaadhibu wakazi wa dunia kwa uovu wao.

Nayo dunia haitaficha tena wale waliouawa,

ila itaufichua umwagaji damu wote.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania