Isaya 55

Isaya 55

Njoni hata kama hamna fedha

1“Haya! Kila mwenye kiu na aje kwenye maji![#55:1 Taz Ufu 21:6; 22:17]

Njoni, nyote hata msio na fedha;

nunueni ngano mkale,

nunueni divai na maziwa.

Bila fedha, bila gharama!

2Mbona mnatumia fedha yenu

kwa ajili ya kitu kisicho chakula?

Ya nini kutoa jasho lenu kwa kitu kisichoshibisha?

Nisikilizeni mimi kwa makini,

nanyi mtakula vilivyo bora,

na kufurahia vinono.

3“Tegeni sikio enyi watu wangu, mje kwangu;[#55:3 Taz Mate 13:34]

nisikilizeni, ili mpate kuishi.

Nami nitafanya nanyi agano la milele;

nitawapeni fadhili nilizomwahidi Daudi.

4Mimi nilimfanya kiongozi na kamanda wa mataifa

ili yeye anishuhudie kwa watu wa mataifa.

5Sasa utayaita mataifa usiyoyajua,

watu wa mataifa yasiyokutambua watakujia mbio,

kwa sababu yangu mimi Mwenyezi-Mungu, Mungu wako;

kwa sababu yangu mimi Mtakatifu wa Israeli

niliyekufanya wewe utukuke.”

6Mtafuteni Mwenyezi-Mungu wakati bado anapatikana,

mwombeni msaada wakati yupo bado karibu.

7Waovu na waache njia zao mbaya,

watu wabaya waachane na mawazo yao mabaya;

wamrudie Mwenyezi-Mungu apate kuwahurumia,

wamwendee Mungu wetu maana atawasamehe.

8Maana, Mwenyezi-Mungu asema hivi:

“Mawazo yangu si kama mawazo yenu,

wala njia zangu si kama njia zenu.

9Kama vile mbingu zilivyo mbali na dunia,

ndivyo njia zangu zilivyo mbali na zenu,

na mawazo yangu mbali na mawazo yenu.

10“Kama vile mvua na theluji ishukavyo toka mbinguni,[#55:10 Taz 2Kor 9:10]

wala hairudi huko bali huinywesha ardhi,

ikaifanya ichipue mimea ikakua,

ikampatia mpanzi mbegu na kuwapa watu chakula,

11vivyo hivyo na neno langu mimi:

Halitanirudia bila mafanikio,

bali litatekeleza matakwa yangu,

litafanikiwa lengo nililoliwekea.

12“Mtatoka Babuloni kwa furaha;

mtaongozwa mwende kwa amani.

Milima na vilima mbele yenu vitapaza sauti na kuimba,

na miti yote mashambani itawapigia makofi.

13Badala ya michongoma kutamea misonobari,

na badala ya mbigili kutamea mihadasi.

Hilo litakuwa jambo litakalowakumbusha watu

juu ya mambo niliyotenda mimi Mwenyezi-Mungu;

ishara ya milele ambayo haitafutwa.”

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania