Yudithi 2

Yudithi 2

Vita dhidi ya mataifa ya magharibi

1Mnamo mwaka wa kumi na nane wa utawala wake, siku ya ishirini na moja ya mwezi wa kwanza, mfalme Nebukadneza pamoja na washauri wake waliamua kutekeleza mpango wao wa kujilipiza kisasi nchi zote zilizokataa kumsaidia.

2Yeye aliwasimulia wakuu wake wa vikosi pamoja na maofisa wakuu jinsi nchi hizo zilivyomsaliti.

3Walikubaliana kuwa yeyote aliyemkataa mfalme Nebukadneza wakati wa vita hana budi auawe.

4Baada ya kuwaeleza mpango wake, mfalme Nebukadneza alimwita Holoferne, mkuu wake wa majeshi. Huyo alikuwa wa pili kwa cheo toka mfalme mwenyewe.

5Mfalme alitoa amri hii kwa Holoferne: “Mimi Nebukadneza, mfalme mkuu na mtawala wa dunia nzima, nakuamuru uchague wanajeshi wenye uzoefu wa vita kama ifuatavyo: Wanajeshi wa miguu 120,000, na wanajeshi wapandafarasi 12,000.

6Kisha nenda ukashambulie eneo lote la nchi zote za magharibi zilizokataa kunisaidia.

7Waambie kuwa hawana budi kuandaa udongo na maji, kwa kuwa nitawatokea katika hasira yangu na kuifunika nchi kwa miguu ya majeshi yangu, na kuwafanya mateka.

8Mabonde na kila kijito na mto nitavijaza maiti zao hadi majeneza yao yafurike kabisa.

9Nitawateka na kuwahamishia mpaka miisho ya dunia.

10“Bali wewe Holoferne, nakuagiza unitangulie na kuyateka maeneo yao yote kabla sijafika. Kama watajisalimisha kwako, yakupasa kuwakamata hadi nitakapofika kuwaadhibu.

11Lakini ikiwa watakuwa wakaidi, usiwaache hai. Waue na kuliteka eneo lao lote, na kuliweka chini ya mamlaka yako.

12Nimeapa kwa maisha yangu na kwa mamlaka ya ufalme wangu kuwa nitayatekeleza kwa mkono wangu mambo niliyoapa kuyafanya.

13Hivyo, wewe ni lazima utii amri zangu, pia lazima utekeleze kikamilifu maagizo yangu bila kuchelewa.”

Holoferne anafanya vita

14Basi, Holoferne alipomwacha mfalme, bila kuchelewa alikusanya makamanda, majenerali na maofisa wa jeshi la Ashuru.

15Akafanya kama bwana wake alivyomwagiza, akakusanya wanajeshi wa miguu 120,000, na wapandafarasi 12,000.

16Akawapanga katika vikosi tayari kwa vita.

17Akachukua idadi kubwa ya ngamia, punda na nyumbu ili kubeba vifaa. Pia alichukua kondoo, ng'ombe na mbuzi kwa ajili ya chakula.

18Kila mwanajeshi alipewa chakula cha kutosha pamoja na idadi kubwa ya dhahabu na fedha kutoka hazina ya kifalme.

19Kisha, Holoferne akaondoka na jeshi lake lote, wakimtangulia mfalme Nebukadneza. Magari ya farasi, wanajeshi wa miguu pamoja na wapandafarasi, likawa jeshi kubwa kiasi cha kulijaza eneo lote la magharibi.

20Kulikuwa na majeshi mengine yaliyokwenda pia. Wanajeshi walikuwa wengi mno kiasi cha kutohesabika; walikuwa wengi kama kundi la nzige au kama mchanga wa ardhi.[#2:20 Taz Amu 7:12; Yoe 2:2-11]

21Baada ya mwendo wa siku tatu kutoka mjini Ninewi, walizifikia mbuga zilizoko kandokando ya mji wa Bektilethi, karibu na milima iliyoko kaskazini ya Kilikia. Huko wakapiga kambi.

22Kutoka hapo Holoferne akasonga mbele kwenye eneo la milimani pamoja na jeshi lake lote, wanajeshi wa miguu, wapandafarasi na magari ya farasi.

23Akaziangamiza kabisa nchi za Libya na Lidia. Akawateka Warasisi na Waishmaeli wote waliokaa kandokando ya jangwa, kusini mwa nchi ya Wakeli.

24Holoferne alizidi kusonga mbele, akauvuka mto Eufrate na kupita katikati ya Mesopotamia, akiangamiza miji yenye ngome kandokando ya mto Abroni, hadi baharini.

25Akaliteka eneo la Kilikia, akimuua mtu yeyote aliyejaribu kumpinga. Akaendelea kusonga mbele hadi mipaka ya kusini ya nchi ya Yafethi, karibu na nchi ya Arabia.

26Akawashambulia ghafla Wamidiani, akazichoma hema zao na kuwateka kondoo wao.

27Holoferne akaenda kwenye sehemu tambarare zilizo jirani ya mji wa Damasko na kwa kuwa ulikuwa ni wakati wa mavuno ya ngano, akayatia moto mashamba yote, akawaua kondoo na ng'ombe wao, akapora mali za miji na maeneo yote ya jirani na kuwaangamiza vijana wote.

28Wakazi wa pwani ya bahari ya Mediteranea wakakumbwa na hofu kubwa, wakabaki wakitetemeka kwa hofu. Kila mtu aliyeishi katika miji ya Tiro, Sidoni, Suru, Osina, Azoto na Askaloni alitishika kwa woga mkuu.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania