Sira 11

Sira 11

1Ikiwa fukara ni mwenye hekima,

anayo sababu ya kujivuna,

tena ataketi pamoja na watu mashuhuri.

Usiamue kwa sura ya nje

2Usimsifu mtu kwa sura yake nzuri,

wala usimdharau mtu kwa sura yake.

3Nyuki ni miongoni mwa viumbe vidogo virukavyo,

lakini wanachotoa ni kitamu kuliko vitu vyote.

4Usijivune kwa sababu unavaa nguo maridadi,

wala kuvimba kichwa wakati unapopewa heshima.

Maana Bwana hufanya mambo ya ajabu,

mambo ambayo binadamu hawezi kuelewa.

5Wafalme wengi wamelazimika kuketi udongoni;

na mtu ambaye hakufikiriwa kabisa akavaa taji la kifalme.

6Watu mashuhuri wengi wameporomoshwa kabisa,

wakuu wengi wametiwa makuchani mwa wengine.

Uwe mwangalifu

7Usimlaumu mtu kabla ya kuchunguza,

fikiri kwanza halafu utoe lawama.

8Sikiliza kabla ya kujibu,

wala usimdakize mwingine anapoongea.

9Usiingilie jambo lisilokuhusu,

usijiingize katika ubishi wa wenye dhambi.

10Mwanangu, usishughulikie mambo mengi mno,

ukiongeza shughuli zako hutaepa kulaumiwa.

Hata ukijaribu kufuatia sana hutafika,

wala hutaweza kutoroka kwa kukimbilia mbali.

11Watu wengine hufanya kazi kwa bidii sana,

lakini mwishowe hujikuta bado wanatindikiwa.

12Wako na wengine ambao hawana bidii na huhitaji msaada,

hawana mali na wamejaa umaskini.

Lakini Bwana huwaangalia kwa wema na kuwainua;

13huwachangamsha na kuwafanya wawe na vitu,

hata watu wengine huwaona na kushangaa.

14Mema na mabaya, uhai na kifo,

umaskini na utajiri, vyote hutoka kwa Bwana. [

15Hekima, elimu na ujuzi wa Sheria hutoka kwa Bwana; upendo na kujua kutenda mema hutoka kwake;

16uhalifu na giza viliumbwa kwa ajili ya wenye dhambi; wanaopenda ubaya watazeeka katika ubaya.]

17Zawadi za Bwana ni hakika kwa wenye kumcha,

wema wake utakuwako daima kuwaongoza.

18Watu wengine huwa matajiri kwa bidii na nguvu,

lakini tuzo wanalopata ni hili:

19Ingawa wanasema: “Sasa naweza kustarehe,

na kufurahia faida niliyopata,”

hawajui itadumu muda gani;

watakufa na kuwaachia wengine utajiri wao.

20Wewe shikilia wajibu wako,

zeeka ukiwa kazini mwako.

21Usistaajabie kazi za wenye dhambi,

lakini mtumaini Bwana na fanya kazi yako.

Maana kwa Bwana ni jambo rahisi sana

kumtajirisha maskini mara moja.

22Wema watapokea baraka ya Mungu.

Mungu huwabariki mara moja.

23Usiseme, “Ninahitaji nini zaidi?

Nitapata nini wakati ujao?”

24Tena, usiseme, “Nina kila kitu cha kunitosheleza.

Ni maafa gani yatakayoweza kunipata?”

25Wakati wa fanaka mtu husahau matatizo;

na wakati wa matatizo hakuna akumbukaye fanaka.

26Maana, kwa Bwana ni jambo rahisi mtu anapokufa,

kumtuza kadiri ya matendo yake.

27Matatizo ya muda mfupi tu humsahaulisha mtu raha;

mtu hujulikana alivyo mwishoni mwa uhai wake.

28Usiseme fulani ana heri kabla hajafa,

maana ushahidi wote hutolewa baada ya kufa.

Uwe mwangalifu kuchagua marafiki

29Usikaribishe kila mtu nyumbani kwako;

maana mitego ya wajanja ni mingi.

30Mtu mwenye majivuno ni kama chombo cha kukutia hatarini,

kama jasusi, atachunguza udhaifu wako.

31Atageuza mambo mema yaonekane kuwa maovu,

na kuona kosa katika matendo mema kabisa.

32Cheche moja huwasha rundo la makaa,

na mwenye dhambi huvizia kumwaga damu.

33Jihadhari na mfidhuli na matendo yake ya ulaghai,

la sivyo atakuletea dosari ya kudumu.

34Mkaribishe nyumbani mtu mgeni naye atazusha mzozo;

atakufanya ufarakane na jamaa yako mwenyewe.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania