Sira 13

Sira 13

1Mtu yeyote agusaye lami atachafuka,

na anayeshirikiana na mwenye kiburi atakuwa kama yeye.

2Usikubali kubeba mzigo upitao nguvu zako,

usishirikiane na mwenye nguvu na tajiri kuliko wewe.

Chungu cha udongo chawezaje kushirikiana na birika la chuma?

Kama vikigongana hicho chungu ndicho kitakachovunjika.

3Tajiri humkosea mtu hata akadiriki kuongeza matusi juu.

Lakini maskini akikosa hulazimika kuomba msamaha.

4Tajiri atakunyonya kila anapopata faida kwako.

Lakini unapotaka akusaidie atakuacha hivihivi.

5Kama una kitu atakaa nawe;

atafyonza mali yako bila hata kujali.

6Anapokuhitaji atakudanganya,

atakuchekea na kukupa tumaini.

Atakuuliza kwa upole: “Unahitaji chochote?”

7Atakufanya uone haya kwa makaribisho yake ya chakula;

akiisha kukunyonya mara mbili tatu, atakucheka.

Kama ukimwona baadaye atajidai hakujui

na kukutikisia kichwa chake.

8Jichunge usije ukapotoshwa;

na kufedheheshwa kwa sherehe zako.

9Ukialikwa na mtu maarufu, uwe mtaratibu;

naye atakualika mara nyingi.

10Usijipeleke kwake kwa pupa,

la sivyo atakufukuza.

Lakini ukikaa mbali naye sana, atakusahau.

11Usijidai kuwa sawa naye,

wala usisadiki maneno yake mengi.

Maana atakupima kwa mazungumzo yake marefu,

na anapokucheka, atakuwa anakuchunguza.

12Mtu asiyeshika siri ni mtu mkatili.

Hatasita kukudhuru au kukutia gerezani.

13Tunza siri zako na uwe mwangalifu,

maana unatembea kwenye hatari. [

Ukisikia kitu unapolala amka!

14Mpende Bwana maisha yako yote na kumwomba akuokoe.]

15Kila kiumbe hupenda kiumbe cha aina yake,

kadhalika na binadamu humpenda binadamu mwenzake.

16Viumbe vyote hujumuika na aina zao,

kadhalika na mtu hujumuika na aliye kama yeye.

17Mbwamwitu na mwanakondoo wana ushirika gani?

Ni vigumu zaidi kushirikisha mwenye dhambi na mcha Mungu!

18Je, kuna amani yoyote kati ya fisi na mbwa?

Na je, kuna amani yoyote kati ya tajiri na fukara?

19Pundamwitu ni mawindo ya simba;

nao maskini ni malisho ya matajiri.

20Unyenyekevu ni chukizo kwa mtu mwenye kiburi,

vivyo hivyo maskini ni chukizo kwa mtu tajiri.

21Tajiri akitetereka hutegemezwa na rafikize.

Lakini maskini akianguka rafikize humsukumia mbali,

22Tajiri akikosea, wa kumsaidia ni wengi;

hata akisema maneno yasiyofaa, humtetea kuwa sawa.

Lakini maskini akitetereka watamkaripia,

hata kama akiongea kwa busara, hakuna anayemjali.

23Tajiri akiongea, wote hunyamaza,

huyasifu anayoongea hadi mawinguni.

Mtu maskini akiongea,

watu husema, “Ni nani huyu?”

Na akijikwaa, watamsukumiza chini.

24Utajiri ni mzuri kama hauhusiani na dhambi,

na umaskini ni mbaya kwa maoni ya wasiomcha Mungu.

25Hali ya mtu moyoni husababisha hali yake ya nje:

Iwe ya furaha au ya huzuni.

26Uso mkunjufu ni alama ya furaha moyoni,

utaonekana mwenye furaha hata nje.

Lakini kuvumbua methali kunahitaji kufikiri sana.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania