Sira 14

Sira 14

1Heri mtu asiyekosea kwa ulimi wake;

hahitaji kusikitika kuwa amekosa.

2Heri mtu ambaye dhamiri yake haimshtaki,

na ambaye hajakata tamaa.

Matumizi ya mali

3Si sawa kwa mtu mchoyo kuwa tajiri.

Utajiri una maana gani kwa mtu bahili?

4Mtu anayekusanya mali kwa kujinyima mwenyewe,

anawakusanyia watu wengine.

Hao wataiponda mali yake katika anasa.

5Aliye bahili kwake mwenyewe atakuwa mkarimu kwa nani,

kama hafurahii utajiri wake mwenyewe?

6Hakuna mtu bahili kuliko anayejichukia mwenyewe;

ndivyo ubaya wake unavyomlipa yeye mwenyewe.

7Hata kama akitenda wema, hutenda kwa ajali,

na mwishowe hujulisha hali yake duni.

8Mtu mwenye kijicho ni mwovu;

huangalia pembeni na kuwadharau watu.

9Jicho la mchoyo haliridhiki na kile alicho nacho,

na uchoyo huidhoofisha roho.

10Mtu mchoyo ni bahili wa chakula,

haweki chakula mezani pake.

11Mwanangu, tumia vitu vyako kukufurahisha uwezavyo,

na mtolee Bwana tambiko zitakiwazo.

12Kumbuka kwamba kifo hakitakawia,

na kwamba hujatangaziwa kauli ya kuzimu.

13Mtendee rafiki yako mema kabla hujafa;

uwe mkarimu na kumpa kadiri ya uwezo wako.

14Usijinyime siku moja ya furaha,

usiache sehemu yako ya furaha halali ikuponyoke.

15Siku moja utawaachia wengine matunda ya jasho lako;

yote uliyochuma kwa kazi ngumu yatagawanywa kwa kura.

16Wape wengine na kupokea kwao ujifurahishe moyo,

maana mtu hatazamii starehe huko kuzimu.

17Viumbe vyote hai huchakaa kama vazi,

maana kauli ya tangu zama ni: “Lazima mtakufa!”

18Kama vile majani katika mti uliotanda matawi:

Hupukutika yakaanguka na mengine huota,

ndivyo ilivyo kwa binadamu wenye mwili na damu:

Mmoja hufa na mwingine huzaliwa.

19Kila kilichotengenezwa huchakaa na kutoweka,

naye mtengenezaji hutoweka na kazi yake.

Furaha ya kuwa na Hekima

20Heri mtu anayetafakari juu ya Hekima

mtu anayefikiri kwa busara.

21Yule anayezifikiria njia za Hekima,

na kuwaza na kuwazua pia juu ya siri zake.

22Mtu amtafutaye Hekima kama vile mwindaji,

na kukaa kwenye njia zake kumngojea.

23Mwenye kuchungulia madirishani mwake,

na kusikiliza milangoni mwake.

24Mwenye makazi yake karibu na nyumba yake

na kufunga kigingi cha hema lake ukutani mwake.

25Mwenye kusimika hema lake karibu naye

na kukaa katika makao yake mazuri.

26Huweka watoto wake chini ya ulinzi wake,

na kupumzika chini ya matawi yake.

27Kwake atapata kivuli cha kumkinga na joto,

na kukaa katika fahari yake.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania