Sira 18

Sira 18

Ukuu wa Mungu

1Yeye aishiye milele aliumba ulimwengu wote.

2Bwana peke yake ndiye atendaye kwa uadilifu. [Na hakuna mwingine isipokuwa yeye.

3Huuongoza ulimwengu kwa kiganja cha mkono wake, na kila kitu hutii matakwa yake. Yeye ni mfalme wa vitu vyote, na nguvu zake hutenganisha kati ya kilicho kitakatifu na kilicho najisi.]

4Hajampa yeyote uwezo wa kutosha kutangaza kazi zake,

na wala hakuna mtu awezaye kuzichunguza.

5Nani anaweza kupima nguvu zake kuu?

Nani anaweza kuhesabu kikamilifu rehema zake?

6Haiwezekani kuzipunguza au kuziongeza.

Haiwezekani kuyaelewa maajabu ya Bwana.

7Binadamu anapofikia mwisho wa hayo

anajikuta kwamba ndio tu anaanza;

na akiacha, anabaki katika bumbuazi.

Mtu si kitu

8Mtu ni nini na anafaa nini?

Uzuri wake ni nini na ubaya wake ni nini?

9Mtu akiishi miaka 100,

ameishi maisha marefu.

10Lakini kama vile tone la maji kutoka baharini,

na kama chembe ya mchanga wa pwani,

ndivyo ilivyo hiyo miaka michache katika milele.

11Kwa hiyo Bwana huwavumilia watu

na kuwamiminia huruma zake.

12Yeye anaona na ajua kuwa mwisho wao ni mbaya

kwa hiyo huwajalia msamaha kwa wingi.

13Mtu humhurumia jirani yake tu,

lakini Bwana ana huruma kwa viumbe vyote hai.

Yeye huwaonya, huwafunza na kuwafundisha watu.

Huwarudisha kama mchungaji arudishapo kundi lake.

14Yeye huwarehemu wanaokubali nidhamu yake

na wanaotamani maamuzi yake.

Wema na kusaidia maskini

15Mwanangu, usichanganye matendo yako mema na lawama.

Unapomsaidia maskini usimhuzunishe kwa maneno yako.

16Je, umande si unaburudisha wakati wa joto kali?

Hivyo neno moja laweza kufaa kuliko zawadi.

17Neno jema lafaa kuliko zawadi,

mtu mkarimu anavyo vyote viwili.

18Mpumbavu ni mkatili na mwenye matusi.

Zawadi ya mtu mchoyo huzima macho.

19Jifunze kabla ya kusema.

Tunza afya yako kabla hujaugua.

20Jichunguze kabla ya hukumu

na siku ile itakapofika, utapata msamaha.

21Jinyenyekeshe kabla ya kupatwa na ugonjwa.

Unapokaribia kutenda dhambi, rudi.

22Usizuiliwe na chochote kutimiza nadhiri zako,

wala usingoje hadi kifo, usamehewe.

23Jitayarishe kabla ya kuweka nadhiri;

wala usiwe kama mtu anayemjaribu Bwana.

24Fikiri juu ya ghadhabu yake siku utakapokufa,

na wakati wa adhabu, atakapogeuzia mbali uso wake.

25Wakati wa fanaka, fikiria wakati wa njaa.

Wakati wa utajiri, fikiria umaskini na ufukara.

26Tangu asubuhi mpaka jioni, hali hubadilikabadilika.

Bwana aweza kugeuza haraka hali za viumbe vyote.

27Mwenye hekima ni mwangalifu katika kila kitu.

Anapokabiliwa na dhambi huchukua hadhari asikosee.

28Kila mwenye akili anajua hekima,

na humsifu yeyote anayeipata.

29Watu wanaoelewa misemo wanapata kuwa na hekima;

nao hububujika methali zifaazo.

Kujichunguza mwenyewe

30Usizifuate tamaa zako mbaya,

bali zuia uchu wako.

31Ukijiachia kufurahia tamaa mbaya,

utakuwa kitu cha kuchekwa na maadui zako.

32Usijitumbukize katika anasa kubwa,

usije ukafilisika kwa gharama zake.

33Usiwe muflisi kukopa fedha za karamu

wakati wewe huna chochote mfukoni.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania