Sira 20

Sira 20

Wakati wa kufaa kuongea

1Mtu anaweza kukaripiwa wakati usiofaa;

kuna ukimya ambao huonesha mtu ana hekima.

2Afadhali zaidi kumwonya mtu kuliko kukaa na hasira.

3Anayekiri kosa lake anajiepusha na balaa.

4Kama vile towashi anayetaka kumnajisi msichana

ndivyo alivyo mtu anayetaka kutekeleza maamuzi yake kwa nguvu.

5Kuna mtu ambaye akinyamaza anaonekana ana hekima;

hali mwingine huchukiwa kwa kuwa ni domo kaya mno.

6Mtu mwingine hunyamaza kwani hana la kusema;

na mwingine hunyamaza kwani anajua wakati wa kuongea.

7Mwenye hekima atanyamaza mpaka wakati ufaao;

Lakini domo kaya na mjinga huukosa wakati wa kufaa.

8Mtu wa maneno mengi mno, atachukiwa,

kadhalika na asiyewapa wengine nafasi ya kuongea.

9Mtu aweza kupata bahati njema katika taabu;

na bahati njema yaweza ikaishia katika hasara.

10Kuna zawadi isiyokuletea faida yoyote;

lakini zawadi nyingine huleta faida maradufu.

11Mara nyingine fahari huleta hasara.

Lakini wako wengine waliofaulu sana kutoka hali duni.

12Mtu hununua vitu vingi kwa bei ya chini,

kumbe hulipa mara saba zaidi ya bei yake.

13Mwenye hekima hufanya apendeke kwa maneno yake;

lakini uungwana wa wajinga ni bure tu.

14Zawadi ya mpumbavu, haitakufaa kitu,

maana anatazamia mengi kutoka kwako, si moja.

15Yeye hutoa kidogo na kupiga domo sana,

hufungua mdomo na kutangaza.

Leo hukopesha, kesho anakitaka.

Mtu kama huyo ni wa kuchukiza.

16Mpumbavu husema, “Sina rafiki.

Hakuna anayenishukuru kwa wema wangu.

Wanakula chakula changu na kunisema vibaya.”

17Naam! Ataendelea kuchekwa na wengi!

Mazungumzo yasiyofaa

18Afadhali kuteleza sakafuni kuliko kuteleza kwa ulimi;

maangamizi ya waovu yatakuja haraka.

19Mtu asiye na shukrani ni kama hadithi isiyo wakati wake,

na ambayo wajinga huirudiarudia.

20Methali ikitoka kwa mpumbavu hukataliwa,

maana haisemi wakati ulio wake.

21Mtu aweza kuzuiwa kutenda dhambi kwa umaskini wake,

kwa hiyo anapopumzika hatakuwa na la kujuta.

22Mtu aweza kupoteza maisha yake kwa kuona aibu,

au akayapoteza kuwaogopa watu.

23Mtu aweza kumwahidi rafiki kitu kwa aibu,

hata akamfanya kuwa adui bila sababu.

24Uongo ni doa baya sana kwa mtu;

uko daima mdomoni mwa mpumbavu.

25Afadhali mwizi kuliko mwenye tabia ya uongo;

lakini wote wawili wataangamia.

26Tabia ya kusema uongo huleta fedheha,

nayo itabaki daima na mwenye kusema uongo.

27Anayaongea kwa hekima, ataendelea vizuri;

mwenye busara atawapendeza wakuu.

28Anayelima ardhi atapata mavuno kwa wingi;

na anayewapendeza wakuu atajipatia haki.

29Bakshishi na zawadi hupofusha macho ya wenye hekima,

ni kizibo mdomoni cha kuwazuia wasikaripie ubaya.

30Hekima ya kuficha na hazina iliyofichika,

je, vina faida yoyote ile?

31Afadhali mtu afichaye upumbavu wake,

kuliko mtu afichaye hekima yake.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania