Sira 21

Sira 21

Dhambi

1Mwanangu, je, umetenda dhambi?

Usitende tena.

Lakini omba msamaha kwa yale uliyotenda.

2Ikimbie dhambi kama kumkimbia nyoka;

maana ukimsogelea nyoka utaumwa.

Meno ya dhambi ni kama ya simba.

Dhambi hufisha maisha ya watu.

3Uvunjaji sheria ni kama panga kali kuwili;

ukikujeruhi, mtu hawezi kutibiwa na kupona.

4Vitisho na ukatili huharibu utajiri;

nyumba ya mwenye kiburi itakuwa mahame.

5Dua la maskini husikika kwa Mungu,

na uamuzi wake Mungu huwasili haraka.

6Anayekataa kukosolewa anatembea katika dhambi,

lakini anayemcha Bwana atatubu moyoni mwake.

7Mtu hodari wa kusema hujulikana kwa mbali,

ukakosea, mwenye busara hutambua.

8Ajengaye nyumba yake kwa fedha ya wengine,

ni kama anayekusanya mawe ya kaburi lake.

9Mkutano wa waovu ni kama kamba ya kitani,

mwishoni mwao ni mwali wa moto mkali.

10Njia ya wenye dhambi imetengenezwa vizuri,

lakini mwisho wake ni kwenye shimo la kuzimu.

Hekima na upumbavu

11Yeyote ashikaye sheria huzitawala fikira zake;

hekima ni ukamilifu wa kumcha Bwana.

12Mtu asiye na akili hafundishiki.

Lakini kuna kuwa na akili ambako huongeza uchungu.

13Maarifa ya mwenye hekima yataongezeka kama mafuriko,

Na mawaidha yake kama chemchemi inayobubujika maji.

14Akili ya mpumbavu ni kama gudulia lililopasuka:

Kamwe haiwezi kushika maarifa.

15Mwenye maarifa akisikia neno la hekima

atalisifu na kuliongezea zaidi,

lakini mpotovu akilisikia hulidhihaki,

na kulitupa mbali kabisa.

16Mazungumzo ya mpumbavu ni kama mzigo safarini;

lakini furaha hupatikana katika maneno ya mwenye akili.

17Katika mkutano watu hutafuta mawazo ya mwenye busara;

nao huyatafakari maneno yake moyoni mwao.

18Kwa mpumbavu hekima ni kama nyumba iliyoanguka;

na maarifa ya mjinga ni maneno yasiyo na mpango.

19Kwa mpumbavu elimu ni kama pingu miguuni,

ni kama pingu kwenye mkono wa kulia.

20Mpumbavu hucheka kwa sauti,

hali mwenye busara hutabasamu tu.

21Kwa mwenye hekima elimu ni kama taji ya dhahabu;

ni kama kikuku kwenye mkono wa kulia.

22Mpumbavu huharakisha kuingia nyumbani kwa mtu;

lakini mwenye busara hungojea mlangoni kwa heshima.

23Mtu asiye na nidhamu huchungulia ndani,

lakini mwenye adabu zake hungoja nje.

24Ni utovu wa adabu kusikiliza mlangoni mwa watu,

kwa wenye busara kufanya hivyo ni aibu.

25Wafidhuli hupenda kurudia waliyosema wengine,[#21:25 hati moja tu ya tafsiri ya Kigiriki. Makala nyingine si dhahiri.]

lakini wenye busara maneno yao yana uzito.

26Wazo la wapumbavu liko mdomoni mwao,

lakini wanachosema wenye hekima hutoka akilini mwao.

27Mtu mbaya anapomlaani Shetani,

anajilaani yeye mwenyewe.

28Mteti huchafua nafsi yake mwenyewe;

naye huchukiwa na majirani zake.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania