Sira 24

Sira 24

Kuisifu Hekima

1Hekima anajisifu mwenyewe,

na kujitukuza miongoni mwa watu wake.

2Atajisifu kwenye kusanyiko la Mungu Mkuu,

atajisifu mbele ya jeshi lake na kusema,

3“Mimi nilitoka mdomoni mwake Mungu Mkuu,

na kuifunika dunia kama ukungu.

4Makao yangu yalikuwa mbinguni juu,

kiti changu cha enzi katika nguzo ya wingu.

5Peke yangu nilipita mzunguko wa mbingu,

nikatembea chini kabisa ahera.

6Juu ya mawimbi ya bahari duniani kote,

natawala kati ya watu wote na mataifa yote.

7Nilitafuta kwao wote mahali pa kupumzika,

nikatafuta ni eneo la nani ambako ningeishi.

8“Hapo huyo Muumba wa vitu vyote akanipa amri;

huyo aliyeniumba akanipangia mahali pa maskani yangu.

Aliniambia, ‘Fanya makao yako kwa Yakobo,

pokea sehemu yako kutoka kwa Israeli.’

9Tangu milele, mwanzoni kabisa aliniumba,

nami nitakuwako milele wala sitaacha kuwako.

10Nilimhudumia katika maskani yake takatifu,

na hivyo nikaimarika katika Siyoni.

11Alinipa pia pa kupumzikia katika mji wake mpendwa,

makao yangu yalikuwa mjini Yerusalemu.

12Niliweka mizizi yangu kati ya watu maarufu,

sehemu yangu kati ya watu walio wake Bwana.

13“Nilirefuka kama mwerezi wa Lebanoni,

nikawa kama msunobari kwenye vilele vya Hermoni.

14Nilirefuka kama mtende wa Engedi

na kama miwaridi huko Yeriko,

nikawa mzuri kama mzabibu shambani,

nikawa mrefu kama mparamuzi.

15Nilinukia harufu ya vikolezo kama mdalasini na mkakaya,

nikaeneza harufu nzuri kama manemane safi.

Harufu kama ya udi, hunukia ubani,

kama harufu nzuri ya ubani hekaluni.

16Matawi yangu nilitandaza kama mwaloni,

nayo yana fahari na yanapendeza.

17Nilichipusha neema kama mzabibu,

maua yangu yakatukuka na kutoa matunda mengi. [

18Mimi ni mama wa upendo mzuri, kicho, uchaji wa Mungu, maarifa na tumaini takatifu. Na kwa kuwa mimi nadumu milele, nimetolewa kwa watoto wangu wote, kwa wale ambao amewataja.]

19Njoni kwangu enyi nyote mnaonitamani,

mkale na kushiba matunda yangu.

20Kunikumbuka mimi ni kutamu kuliko asali,

kunipata mimi ni kutamu kuliko sega la asali.

21Wanilao mimi watataka tena zaidi

waninywao watataka kunywa zaidi.

22Mwenye kunitii hataaibishwa kamwe,

wanaojishughulisha nami hawatatenda dhambi.”

Hekima na sheria

23Yote haya ni kitabu cha agano la Mungu Mkuu,

kitabu cha sheria aliyotuamuru Mose tufuate.

Sehemu waliyopewa watu wa jumuiya ya Yakobo. [

24Usiache kumtegemea Bwana kwa dhati, andamana naye ili akuimarishe; Bwana Mwenye Nguvu peke yake ndiye Mungu, hakuna awezaye kuokoa ila yeye.]

25Sheria huwatiririshia watu hekima kama mto Eufrate,

na kama mto Tigri wakati wa matunda ya mwanzoni.

26Sheria inawajaza maarifa kama mto Eufrate,

na kama mto Yordani wakati wa mavuno.

27Hufanya mafunzo yangae kama mwanga,

kama Gihoni wakati wa kuchuma zabibu.

28Mtu wa kwanza hakuweza kumjua Hekima kamili,

na mtu wa mwisho pia hataweza kumwelewa.

29Maana mawazo yake ni mengi kama maji baharini,

na mashauri yake yana kina kuliko kilindi cha kuzimu.

30Mimi nilijitokeza kama mfereji kutoka kwenye mto,

kama mfereji wa maji kwenda bustanini.

31Nilisema, “Nitainywesha bustani yangu,

na kulowanisha vitalu vyake.”

Na kumbe, mfereji wangu ukageuka mto,

na mto wangu ukageuka bahari.

32Basi, mafunzo yangu nitayangarisha tena kama pambazuko;

nitayangarisha, yaangaze mpaka mbali.

33Nitamimina mafundisho tena kama unabii

na kuviachia vizazi vijavyo.

34Kumbukeni sikufanya kazi kwa ajili yangu mwenyewe,

bali kwa ajili ya wote wanaotafuta kufunzwa.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania