Sira 25

Sira 25

Watu wanaostahili kusifiwa

1Moyo wangu wafurahia mambo matatu;

mambo yaliyo mazuri mbele ya Bwana na wanaadamu:

Ndugu wanaopatana vizuri,

jirani wenye uhusiano mwema,

na mke na mume wanaoishi kwa furaha.

2Moyo wangu wawachukia watu wa aina tatu,

watu ambao nachukizwa sana na maisha yao:

Maskini mwombaji mwenye kiburi,

tajiri ambaye ni mwongo,

na mzee mzinzi asiye na akili.

3Kama hukuokota chochote cha funzo ulipokuwa kijana,

utawezaje, basi, kupata chochote katika uzee wako?

4Ni jambo zuri mno kwa mzee mwenye mvi kuamua vema,

na mwenye umri mkubwa kujua namna ya kushauri!

5Ni jambo la kupendeza mno hekima katika wazee,

na mawaidha yafaayo na mashauri kutoka kwa watu mashuhuri!

6Uzoefu mwingi wa maisha ni taji ya wazee,

kumcha Bwana ndiyo fahari yao.

7Najua mambo tisa ambayo nayathamini sana moyoni;

naam, na jambo la kumi nitawaambieni pia:

Mtu anayefurahi kwa sababu ya watoto wake,

mtu aishiye hata akawaona maadui zake wanaangamia;

8mwanamume aliye na bahati ya kuishi na mke mwenye akili,

ambaye halimi shambani kwa ng'ombe pamoja na punda,

mtu ambaye hajakoseshwa na ulimi wake,

mtu asiyemtumikia mtu ambaye hastahili,

9mtu aliye na bahati ya kupata rafiki amini,

na mtu ambaye watu hufurahia kumsikiliza.

10Jinsi gani alivyo mkuu mtu aliyepata hekima!

Lakini hakuna aliye mkuu kuliko yule amchaye Bwana!

11Kumcha Bwana ni muhimu kuliko mambo yote.

Mtu amchaye Bwana hana kifani! [

12Kumcha Bwana ni mwanzo wa kuandamana naye.]

Mke mwema na mke mbaya

13Hakuna jeraha baya kama jeraha la moyoni!

Hakuna ubaya mbaya kuliko ubaya wa mwanamke!

14Hakuna pigo baya kama la mtu mwenye chuki.

Hakuna kisasi kibaya kama kisasi cha adui.

15Hakuna sumu mbaya kama sumu ya nyoka,

na hakuna hasira mbaya kama hasira ya adui.

16Afadhali kuishi na simba na nyoka

kuliko kuishi na mwanamke mwovu.

17Uovu wa mwanamke humbadilisha sura,

uso wake ukawa kama uso wa dubu.

18Mumewe akila chakula kwa jirani

hawezi kujizuia kupiga kite kwa uchungu.

19Hakuna uovu mbaya kuliko uovu wa mke wa mtu;

huyo atapatwa na balaa la wenye dhambi.

20Kama vile ilivyo shida kwa miguu ya mzee kupanda mlima uliojaa mchanga,

ndivyo ilivyo kwa mume mpole kuishi na mke mwenye makelele.

21Usinaswe na uzuri wa mwanamke,

wala usimtamani mwanamke kwa mali yake.

22Ni ghadhabu, aibu na fedheha

mume kulishwa na mkewe.

23Moyo wa huzuni, kukosa raha na kuvunjika moyo,

husababishwa na mke mwovu.

Mikono na magoti hafifu ya mumewe

husababishwa na mke asiyemfurahisha mumewe.

24Dhambi ilianza kwa mwanamke,

na kwa sababu yake sote lazima tufe.

25Kama vile huachi maji yavuje,

vivyo hivyo usikubali mke mwovu aseme apendavyo.

26Kama hapendi kufuata kama unavyomwagiza,

basi mtenganishe nawe.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania