The chat will start when you send the first message.
1Anayelipiza kisasi naye atalipizwa na Bwana,
na Bwana atathibitisha kuwa mtu huyo ana dhambi.
2Msamehe jirani yako maovu aliyokutendea,
nawe unapoomba, utasamehewa dhambi zako.
3Kama mtu akidumisha hasira dhidi ya mtu mwingine,
atawezaje kumtaka Bwana amwonee huruma?
4Kama hamwonei huruma binadamu mwenzake,
je, ni sawa kumwomba Bwana amsamehe dhambi zake?
5Kama yeye ambaye ni kiumbe tu anashikilia hasira,
nani atamsamehe yeye dhambi zake?
6Kumbuka mwisho wa maisha yako uache uadui;
kumbuka maangamizi na kifo, uzingatie amri.
7Kumbuka amri, na usimkasirishe jirani yako.
Likumbuke agano la Mungu Mkuu, uache ujinga.
8Epa ugomvi, nawe utapunguza kutenda dhambi.
Maana mtu mwenye hasira huchochea ugomvi.
9Mwenye dhambi huwasumbua marafiki
na kuweka uadui kati ya watu waishio kwa amani.
10Kadiri ulivyo na kiasi cha kuni,
ndivyo na moto utakavyowaka.
Kadiri ubishi unavyozidi,
ndivyo na ugomvi utakavyowaka.
Kadiri mtu alivyo na nguvu
ndivyo atakavyozidi kuwaka hasira.
Kadiri mtu anavyozidi kuwa tajiri,
ndivyo anavyozidi kuwa na ghadhabu.
11Kugombana kwa ghafla huwasha moto,
na ugomvi wa ghafla humwaga damu.
12Ukipuliza kaa la moto litawaka zaidi,
ukilitemea mate litazimika;
hayo yote mawili ni matokeo ya kinywa chako.
13Alaaniwe mtu mchongezi na mdanganyifu,
maana amewaangamiza wengi wanaoishi kwa amani.
14Uchongezi umevunja amani ya wengi,
na kuwatawanya kutoka taifa hata taifa lingine;
uchongezi umeangamiza miji yenye nguvu,
na kuangusha nyumba za wakuu.
15Uchongezi umewafanya wake waaminifu wawakimbie waume zao,
na kuwanyanganya matunda ya jasho lao.
16Yeyote anayemsikiliza mchongezi hatatulia moyoni,
wala hataishi kwa amani.
17Pigo la mjeledi hubakiza kovu,
lakini pigo la ulimi huvunjavunja mifupa.
18Watu wengi wameuawa kwa upanga,
lakini ni wengi zaidi waliouawa kwa ulimi.
19Heri mtu ambaye amekingwa mbali na ulimi,
mtu ambaye hajakabiliwa na hasira yake.
Mtu ambaye hajabeba nira yake,
na kufungwa kwa pingu zake.
20Maana nira yake ni nira ya chuma,
na pingu zake ni pingu za shaba.
21Kifo kiletwacho na uchongezi ni kifo kibaya,
kuzimu ni afadhali kuliko uchongezi.
22Lakini uchongezi hauwezi kuwatawala wamchao Mungu,
hao hawatachomwa na miali yake.
23Makuchani mwake wataanguka wale wanaomwacha Bwana;
watakuwa chini ya mamlaka yake.
Uchongezi utawaka ndani yao, wala hautazimishwa.
Utawavamia hao kama simba,
utawararuararua kama chui.
24Hakikisha umeweka ua wa miiba kuzunguka mali zako,
umefungia ndani fedha na dhahabu yako.
25Hakikisha umeizungushia mali yako ua wa miiba,
pima maneno yako kama vile kwa mizani,
na kinywa chako ukiwekee mlango na kufuli.
26Jihadhari usije ukakosa kwa kinywa chako,
la sivyo utaanguka mbele ya huyo anayekuotea.