Sira 29

Sira 29

Kukopa na kulipa

1Mwenye huruma humkopesha jirani yake;

kumsaidia jirani ni kutimiza amri.

2Mkopeshe jirani yako anapohitaji msaada,

na ukimkopa jirani yako, mlipe mara.

3Tekeleza neno lako na kuwa na imani naye,

nawe utapata mahitaji yako kila wakati.

4Wengi hudhani mikopo ni zawadi,

na kuwaaibisha hao waliowasaidia.

5Mtu atabusu mkono wa mtu mwingine mpaka amkopeshe,

na kunongoneza juu ya mali ya jirani yake.

Lakini wakati wa kulipa mkopo atachelewa,

atalipa kwa maneno mengi matupu

na kudai kukosekana kwa wakati.

6Kama anaweza kulipa, atamlipa labda nusu,

kwani mkopaji anadhani mkopo si wa kulipa.

Kama hawezi kulipa, mkopaji amemwibia,

na hivyo amemfanya kuwa adui yake bure.

Atamlipa laana na matukano;

badala ya kumheshimu atamlipa madharau.

7Kwa sababu hiyo, wengi hukataa kukopesha,

wanaogopa kudhulumiwa bure.

Ukarimu

8Hata hivyo, uwe na uvumilivu kwa mtu aliye maskini,

wala usimfanye angoje mno kupata msaada wako.

9Msaidie maskini kwani hiyo ni amri,

kama anahitaji, usimwache aende mikono mitupu.

10Tumia fedha yako kumsaidia ndugu au rafiki,

wala usiiache ipate kutu mafichoni na kupotea.

11Tumia utajiri wako kama alivyoamuru Mungu Mkuu

nawe utapata faida kubwa kuliko dhahabu.

12Jaza hazina yako misaada kwa maskini,

hiyo itakuokoa wakati wa maafa.

13Hiyo itakupigania dhidi ya adui yako,

vizuri kuliko kwa ngao kubwa na mkuki mzito.

Dhamana

14Mtu mwema atamwekea jirani yake dhamana,

lakini mtu asiye na aibu atamwacha.

15Usisahau wema wa mdhamini wako,

maana ameyahatarisha maisha yake kwa ajili yako.

16Lakini mtu mwenye dhambi ataharibu mali ya mdhamini wake,

mtu asiye na shukrani atamwacha yule aliyemwokoa.

17Kutoa dhamana kumewaangamiza matajiri wengi,

na kuwatikisa kama kwa mawimbi makubwa.

18Kutoa dhamana kumewafanya watu wengi maarufu kuwa wakimbizi,

wakatangatanga miongoni mwa mataifa mengine.

19Mwenye dhambi anayekubali kuwa mdhamini atajuta,

atatafuta faida na kujikuta amekabiliwa na sheria.

20Msaidie jirani yako kadiri unavyoweza,

lakini uchukue hadhari usije ukaanguka katika maafa.

Nyumba na ukarimu

21Mahitaji ya maisha ni maji, chakula na mavazi,

na nyumba unakoweza kujificha.

22Afadhali maisha ya maskini mwenye nyumba yake mwenyewe,

kuliko chakula cha fahari nyumbani kwa wengine.

23Ridhika na kidogo ulicho nacho,

nawe hutakemewa kuwa unaishi kwa jasho la wengine.

24Ni fedheha kutangatanga nyumba moja hata nyingine,

popote ulipo mgeni huwezi kufungua kinywa chako;

25wewe utakuwa mgeni na kuonja kunyenyekeshwa,

tena utasikia maneno yatakayokuumiza:

26“Mgeni, njoo hapa na kuandaa meza!

Na kama una chochote, nipe nile.

27Mgeni, nenda zako umwachie nafasi mtu maarufu.

Ndugu yangu anakuja kwangu, nahitaji nyumba yangu.”

28Mambo ya kutukanwa kuhusu malazi na mkopo,

hayavumiliki kwa mtu mwenye akili zake.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania