Sira 3

Sira 3

Wajibu wa watoto kwa wazazi

1Wanangu sikilizeni mawaidha ya baba yenu.

Fanyeni ninayowaambia,

nanyi mtawekwa salama,

2maana Bwana amewapa kina baba mamlaka juu ya watoto wao,

na kuimarisha uwezo wa kina mama juu ya watoto wao.

3Anayemheshimu baba yake anajipatia msamaha wa dhambi zake.

4Anayemheshimu mama yake anajiwekea hazina kubwa.

5Anayemheshimu baba yake atafurahishwa na watoto wake mwenyewe,

na atakapomwomba Bwana, atasikilizwa.

6Anayemheshimu baba yake atapata maisha marefu,

anayempendeza mama yake anamtii Bwana.

7Mtoto huyo, huwatumikia wazazi wake kama Bwana wake.[#3:7 mwanzoni mwa mstari huu hati nyingine zina: Amchaye Bwana atamheshimu baba yake.]

8Mheshimu baba yako kwa maneno na matendo,

ili upate baraka kutoka kwake.

9Maana baraka za baba huimarisha nyumba za watoto,

hali laana ya mama huingoa misingi ya nyumba zao.

10Usijikuze mwenyewe kwa kumdharau baba yako.

Maana kumdharau baba yako hakutakuletea faida.

11Maana fahari ya baba mtu ni fahari ya huyo mtoto,

na watoto wasiomheshimu mama yao ni balaa.

12Mwanangu, mtunze baba yako alipo mzee

wala usimhuzunishe muda wote aishipo.

13Hata akipungukiwa akili, umvumilie.

Usimdharau kwa vile wewe una afya na nguvu.

14Bwana hatasahau wema wako kwa baba yako,

utakusaidia kukupatia msamaha wa dhambi zako.

15Wakati wa taabu Bwana atakumbuka wema wako.

Kama umande kwenye jua, dhambi zako zitatoweka.

16Anayemtupa baba yake anamkufuru Mungu;

anayemkasirisha mama yake analaaniwa na Bwana.

Unyenyekevu

17Mwanangu, uwe mpole katika shughuli zako,

nawe utapendwa na wale wanaokubaliwa na Mungu.

18Kadiri ulivyo mkuu, ndivyo unavyotakiwa kunyenyekea;

na hapo utapata kibali cha Bwana. [

19Wengi hujitukuza na kujiona bora, lakini siri za Mungu hufunuliwa kwa wanyenyekevu. Makala ya Kiebrania: Huruma za Mungu ni kubwa, naye huwafunulia wanyenyekevu siri zake.]

20Nguvu ya Bwana ni kuu

lakini hutukuzwa na wanyenyekevu.

21Usitafute yaliyo magumu mno kwako,

wala kuchunguza yaliyo nje ya uwezo wako.

22Zingatia yale uliyopangiwa kufanya,

huhitaji kujihangaisha juu ya mambo yaliyofichika

23Usiingilie mambo yanayopita nguvu zako

maana hata hayo uliyooneshwa yanapita akili ya binadamu.

24Maana wengi wamepotoshwa kwa kujiona kuwa wajuzi sana,

maoni yao ya utundu yamepotosha akili zao. [

25Kama huna macho huwezi kuona; usijitakie kuwa na akili kama hunayo.]

26Mwenye kiburi ataishia vibaya mwishoni;

na apendaye hatari ataangamia huko.

27Mwenye kiburi atalemewa taabu;

mwenye dhambi hujirundikia dhambi mfululizo.

28Mateso ya mwenye kiburi hayana matibabu.

Maana uovu umeota na kutia mzizi ndani yake.

29Mwenye akili atazitafakari methali moyoni mwake;

kuwa mtu msikivu ndicho atakacho mwenye busara.

Kuwasaidia maskini

30Kama vile maji yazimavyo moto mkali

ndivyo na sadaka kwa maskini iletavyo msamaha wa dhambi.

31Amwoneaye huruma mwenzake hufikiria mbele,

wakati atakapopata taabu atasaidiwa.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania