The chat will start when you send the first message.
1Hakuna baa lolote litakalompata mtu amchaye Bwana;
wakati wa majaribu Bwana atamwokoa tena na tena.
2Mwenye hekima hataichukia sheria,
lakini mnafiki juu ya sheria ni kama mashua kwenye mawimbi.
3Mwenye busara atakuwa na imani na sheria,
kwake sheria ni ya kutegemewa kama kauli ya Mungu.
4Tayarisha utakachosema nawe utasikilizwa;
panga pamoja unayoyajua kisha ujibu.
5Moyo wa mpumbavu ni kama gurudumu la mkokoteni,
na mawazo yake kama kizungukio.
6Rafiki mwenye mizaha ni kama farasi;
kila anayempanda farasi hutoa sauti.
7Kwa nini siku moja ni bora kuliko nyingine
hali zote zinapata mwanga wake kutoka kwa jua?
8Bwana ndiye aliyeamua kuzitofautisha,
na kuweka majira mbalimbali na sikukuu.
9Siku nyingine alizikuza na kuzitakasa,
na nyingine alizifanya ziwe za kawaida tu.
10Binadamu wote wametoka udongoni,
naye Adamu aliumbwa kutoka mavumbini.
11Lakini, Bwana kwa hekima yake kamili aliwatofautisha,
na kila mmoja wao akampa jukumu tofauti.
12Baadhi yao aliwabariki na kuwakuza,
baadhi aliwafanya watakatifu na kuwaweka karibu naye.
Lakini wengine aliwalaani na kuwashusha,
akawaondoa kutoka mahali pao.
13Kama udongo mikononi mwa mfinyanzi ambaye huufinyanga atakavyo,
ndivyo walivyo binadamu mikononi mwake aliyewaumba:
Yeye huwafanya kama anavyoamua.
14Wema ni kinyume cha uovu,
na uhai ni kinyume cha kifo,
ndivyo na mwenye dhambi ni kinyume cha mcha Mungu.
15Angalia kazi zote za Mungu Mkuu:
Ziko mbilimbili, kimoja kinyume cha kingine.
16Mimi, nimekuwa wa mwisho kuyaangalia hayo,
kama mtu anayeokota zabibu baada ya wavunaji kupita.
17Lakini Bwana amenibariki sana, nikawazidi wote;
kama vile mvunazabibu nimejaza kinu cha kusindikia.
18Kumbuka sikufanya kazi kwa ajili yangu tu,
bali kwa ajili ya wote wanaotaka kujifunza.
19Nisikilizeni enyi wakuu kati ya watu;
nanyi viongozi wa jumuiya, nisikilizeni.
20Muda wote uishipo usimwachie mtoto, mke, ndugu au rafiki akutawale;
usimpe mtu mwingine mali yako,
usije ukabadili nia na kuomba urudishiwe.
21Ungali bado hai, unapumua,
usikubali mtu mwingine achukue nafasi yako.
22Maana ni afadhali watoto wako wakutegemee,
kuliko wewe kuwategemea wao.
23Fanya kila kitu ufanyacho vizuri kabisa,
usiitie dosari heshima yako.
24Mwisho wa maisha yako,
wakati wa saa yako ya mwisho,
gawa mali yako.
25Nyasi, mzigo na kiboko kwa punda,
chakula, nidhamu na kazi kwa mtumwa.
26Mpe mtumwa wako kazi nawe utapata pumziko,
mwache bila kazi naye atataka uhuru.
27Mtiishe mnyama kwa nira na lijamu,
na mtumwa mwovu kwa mateso.
28Mpe kazi ili asiwe mvivu,
maana uvivu huwafunza watu uovu mwingi.
29Mpe kazi kama inavyostahili kwako,
na kama hakutii, mfunge minyororo.
30Usimtendee mtu yeyote bila kiasi,
wala usifanye chochote bila busara.
31Ukiwa na mtumwa na awe kama wewe,
kwa sababu umemnunua kwa jasho lako.
32Ukiwa na mtumwa, mtendee kama ndugu yako,
maana utamhitaji kama unavyohitaji roho yako.
33Ukimtendea vibaya akakukimbia,
utafuata njia ipi kumtafuta?