Sira 37

Sira 37

1Kila mtu anaweza kudai,

“Mimi pia ni rafiki yako.”

Lakini rafiki wengine ni rafiki kwa jina tu.

2Je, si pigo la kifo ndugu au rafiki akiwa adui?

3Ee mwelekeo wa uovu, kwa nini umeumbwa

hata ukaijaza dunia kwa udanganyifu?

4Baadhi ya ndugu hufurahia furaha ya rafiki,

lakini, wakati wa taabu humwacha.

5Wengine humsaidia rafiki kwa ajili ya chakula,

lakini vita vikitokea, hujikinga wao wenyewe.

6Usimsahau rafiki yako wa kweli;

na unapokuwa tajiri usimfute moyoni mwako.

Washauri

7Kila mshauri atatoa ushauri,

lakini wengine hutoa ushauri kwa faida yao.

8Uwe mwangalifu juu ya mshauri,

ukachunguze kwanza anachotaka,

maana huenda anajifikiria yeye mwenyewe tu.

Huenda amekwisha fanya mpango dhidi yako.

9Huweza kusema: “Mambo yote ni sawa”,

halafu akasimama mbali kuona yatakayokupata.

10Usiombe ushauri kwa mtu unayemwonea mashaka,

na usimpe ushauri mtu anayekuonea wivu.

11Usiombe ushauri kwa mwanamke kuhusu mpinzani wake,

usiombe ushauri kwa mwoga kuhusu vita,

kwa mfanyabiashara kuhusu biashara,

kwa mnunuzi kuhusu uuzaji wa mali,

kwa mtu bahili kuhusu ukarimu,

kwa mtu mkatili kuhusu upole;

kwa mtu mvivu kuhusu kazi,

kwa kibarua kuhusu kumaliza kazi,

au kwa mtumwa mvivu kuhusu kazi ngumu.

Usiwajali watu wa namna hiyo,

kuhusu jambo la kupata ushauri.

12Lakini uwe na uhusiano daima na mcha Mungu,

ambaye unajua anatii amri,

yeye nawe mnapatana,

naye atahuzunika nawe ukishindwa.

13Utegemee sana shauri la moyo wako;

maana hakuna aliye mwaminifu kuliko moyo wako.

14Moyo wa mtu mara nyingi humpa mawaidha mema

kuliko yale ya walinzi saba wanaolinda zamu mnarani.

15Zaidi ya hayo, mwombe Mungu Mkuu

ili aiongoze njia yako katika ukweli.

Hekima ya kweli na ya uongo

16Busara iwe ndio msingi wa kila tendo,

na shauri hutangulia shughuli yoyote.

17Mawazo yote yamo moyoni,

na kutoka humo namna nne huonekana:

18Wema na uovu, uhai na kifo;

na mtawala wa hayo daima ni ulimi.

19Mtu aweza kuwa na busara na mwalimu wa wengi,

lakini asiwe na faida kwake mwenyewe.

20Mtu aliye hodari wa kusema aweza kuchukiwa,

hata akakosa chakula kabisa,

21maana hakupewa neema na Bwana,

kwa vile hana hekima yoyote.

22Mwingine ana hekima kwa faida yake mwenyewe,

na maneno yake akayaona yeye mwenyewe kuwa hakika.

23Mwenye hekima atawafunza watu wake,

na matokeo ya maarifa yake yatakuwa hakika.

24Mwenye hekima atapewa sifa kwa wingi,

na wote watakaomwona watamwita mwenye bahati.

25Siku za maisha ya mtu zimehesabiwa,

lakini siku za Israeli hazihesabiki.

26Mwenye hekima atajipatia heshima kwa watu wake,

na jina lake litadumu milele.

Kuwa na kiasi

27Mwanangu, jipime nafsi yako ungali hai;

ona ni kitu gani kibaya kwako, ukiepe.

28Maana si kila kitu kinafaa kwa kila mtu,

wala si kila mtu anafurahia kila kitu.

29Usiwe mwenye uchu wa kila anasa,

wala usiwe mtumwa wa chakula.

30Maana kula mno huleta ugonjwa,

ulafi huleta kichefuchefu.

31Wengi wamekufa kwa sababu ya ulafi,

anayekwepa ulafi, atarefusha maisha yake.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania