Sira 38

Sira 38

Dawa na ugonjwa

1Mpe daktari heshima anayostahili,

kwa sababu ya huduma zake kwako,

kwa vile naye aliumbwa na Bwana.

2Maana kipaji chake cha kuponya chatoka kwa Mungu Mkuu;

naye hupata zawadi kutoka kwa mfalme.

3Ujuzi wa daktari humfanya maarufu,

naye huheshimiwa miongoni mwa wakuu.

4Bwana aliumba dawa zote kutoka ardhini,

na mtu mwenye busara hawezi kuzidharau.

5Je si kwa kijiti maji yaligeuzwa kuwa mazuri

ili Mungu awaoneshe watu nguvu yake?

6Bwana aliwapa watu maarifa na ujuzi,

ili atukuzwe katika kazi zake za ajabu!

7Kwa dawa huwaponya watu na kuondoa maumivu;

8mchanganya dawa hutengeneza mchanganyiko wake.

Kazi za Bwana hazina mwisho;

afya yote duniani hutoka kwake.

9Mwanangu, ukiugua usiwe mzembe juu ya ugonjwa,

bali mwombe Bwana naye atakuponya.

10Acha makosa yako, uamue kutenda mema,

na kutakasa moyo wako dhambi zote.

11Mtolee Bwana tambiko ya harufu nzuri,

na tambiko ya ukumbusho ya unga safi.

Umiminie tambiko zako mafuta,

kadiri unavyoweza kupata.

12Kisha mengine mwachie daktari;

maana Bwana ndiye aliyemuumba;

usikubali akuache maana unamhitaji.

13Kuna wakati ambapo kupona kwawategemea madaktari.

14Maana nao pia wanamwomba Bwana

ili awape mafanikio katika uchunguzi wao,

na katika kuponya ili kuokoa maisha.

15Mtu anayetenda dhambi dhidi ya Muumba wake,

mwache aanguke mikononi mwa daktari.

Matanga

16Mwanangu, mlilie mtu aliyekufa;

lia kwa uchungu, kuonesha huzuni yako.

Uuzike mwili wake kwa heshima ipasavyo,

wala usipuuze mazishi yake.

17Lia kwa uchungu na kwa moyo,

hudhuria matanga kama anavyostahili marehemu,

omboleza siku mbili tatu usije ukasemwa;

kisha ufarijike kutokana na huzuni yako.

18Maana huzuni huweza kusababisha kifo,

na huzuni ya moyo hunyonya nguvu za mtu.

19Mtu akiondolewa duniani huzuni imekwisha,

lakini maisha ya maskini, huulemesha moyo.

20Usiruhusu moyo wako kutawaliwa na huzuni;

ifukuze huzuni, ukifikiria mwisho wako.

21Usisahau kwamba hakuna kurudi nyuma,

humsaidii marehemu chochote na unajidhuru mwenyewe.

22Kumbuka, utakufa kama alivyokufa,

jana yeye, kesho wewe.

23Marehemu anapowekwa kupumzika kaburini,

nako kumkumbuka kuachwe;

nawe usiendelee kumlilia roho yake ikisha ondoka.

Shughuli

24Nafasi humwezesha msomi kujifunza hekima,

aliye na shughuli chache aweza kupata hekima.

25Atakuwaje na hekima mtu anayeshughulika tu na jembe?

Fahari yake ni kuongoza ng'ombe,

kuwafanya wakokote plau,

na mazungumzo yake yote ni juu ya mifugo!

26Mawazo yake ni kupiga mifuo shambani,

na kuwalisha ndama wake.

27Kadhalika na kila mfanyakazi na fundi,

ambaye hufanya kazi usiku na mchana;

na wanaonakshi mihuri wakibuni daima mbinu mpya;

hufanya bidii kunakshi mifano mizuri,

na kukesha wakiikamilisha kazi yao.

28Kadhalika na mfuachuma kwenye fuawe yake;

hufikiria cha kufanya na chuma chake,

miali ya moto hudhoofisha mwili wake,

akilivumilia joto la tanuri;

sauti ya nyundo yake huziba masikio yake,

macho yake hukodolea chombo afuacho.

Moyo wake umepania kuikamilisha kazi yake

na huwa mwangalifu kukamilisha nakshi yake.

29Kadhalika na mfinyanzi kazini mwake,

hulizungusha gurudumu kwa mguu wake,

kila siku yu macho juu ya kazi yake

na hukesha kutimiza idadi itakiwayo.

30Huupondaponda udongo kwa mkono wake

huufinyanga kwa miguu yake,

hutia maanani sana kumaliza kazi yake,

na huwa mwangalifu kusafisha kinu chake.

31Wote hao huitegemea mikono yao,

na kila mmoja ana ujuzi wa kazi yake.

32Bila wao mji haujengeki;

na watu hawawezi kuutembelea wala kuishi huko.

33Hata hivyo, hawafikii hali ya kuwa halmashauri ya watu,

wala hawapewi hadhi katika kikao cha hadhara.

Hawawi mahakimu wala kuelewa hukumu zinazotolewa.

34Hawawezi kueleza mafunzo au maamuzi ya sheria,

wala hawajaonekana wakitumia methali.

Lakini huufanya ulimwengu ulioumbwa utengemae,

na dua lao lahusu mambo ya shughuli zao!

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania