The chat will start when you send the first message.
1Majukumu magumu yaliumbwa kwa ajili ya binadamu wote,
mzigo mzito uko juu ya wanaadamu tangu walipozaliwa
mpaka watakaporudi kwao mavumbini,
ambayo ni mama wa watu wote.
2Wasiwasi wao, hofu ya moyoni,
na woga wao ni juu ya siku ya kufa.
3Hayo huwapata wote: Tangu mfalme katika fahari yake,
mpaka mnyonge anayeketi mavumbini na katika majivu;
4tangu tajiri na mavazi yake ya zambarau na taji kichwani,
mpaka yule maskini avaaye magunia.
5Kila kitu ni hasira na wivu, shida na wasiwasi,
hofu ya kifo, uadui na ugomvi.
Hata mtu anapolala kitandani mwake
usingizi wake huvuruga mawazo yake.
6Hulala usingizi kidogo au halali kabisa;
na akiwa amelala, huwa kama yu macho.
Husumbuliwa na maono akilini mwake,
kama mtu aliyetoroka mstari wa mbele vitani.
7Wakati wa kuokolewa, huamka,
akashangaa kwamba hofu zake hazikuwa kweli.
8Ndivyo ilivyo kwa viumbe wote, binadamu na wanyama,
na kwa wenye dhambi ni mara saba:
9Kila mara kifo, umwagaji damu, mapigano na vita,
maafa, njaa, mateso na tauni.
10Hayo yote yaliumbwa kwa ajili ya wenye dhambi,
na kwa sababu ya waovu gharika ilikuja.
11Vitu vyote vilivyotoka ardhini vitarudi ardhini,
kama vile maji yote hurudi baharini.
12Kila rushwa na udhalimu, vitafutwa,
lakini imani njema itadumu milele.
13Mali ya waovu itakauka kama kijito,
itapondeka kwa kishindo kama ngurumo wakati wa mvua nyingi.
14Mtu mkarimu atapata furaha,
lakini wakosefu wataangamia kabisa.
15Watoto wa wasiomcha Mungu hawatakuwa na chipukizi,
wao ni kama mizizi dhaifu kwenye mwamba mtupu.
16Matete yaliyo kando ya maji au mto,
hayo ndiyo yatakayongolewa kabla ya nyasi nyingine.
17Wema ni kama bustani iliyojaa baraka,
na sadaka kwa maskini hudumu milele.
18Kwa anayejitegemea na mfanyakazi maisha ni mazuri;
lakini bora kuliko hiyo ni mtu anayegundua hazina.
19Kuwa na watoto na kujenga mji humpatia mtu jina,
lakini mke asiye na hatia ni bora kuliko hivyo viwili.
20Pombe na muziki hufurahisha moyo,
lakini kuipenda hekima ni bora kuliko hivyo viwili.
21Filimbi na kinanda hutoa muziki mtamu,
lakini sauti ya kupendeza ni bora zaidi.
22Macho hufurahia urembo na uzuri wa mtu,
lakini uzuri wa chipukizi za mbegu ni bora zaidi.
23Rafiki na ndugu hufaa sana,
lakini kupatana kwa mke na mumewe ni bora zaidi.
24Kuwa na ndugu na msaada wakati wa shida ni vizuri,
lakini kuwasaidia maskini huokoa kuliko hivyo.
25Dhahabu na fedha humfanya mtu imara,
lakini shauri jema lathaminiwa kuliko hivyo viwili.
26Mali na nguvu humfanya mtu kuwa thabiti,
lakini kumcha Bwana ni bora zaidi.
Hakuna dosari katika kumcha Bwana,
na ukiwa na kipaji hicho huhitaji msaada.
27Kumcha Bwana ni kama bustani ya baraka,
nayo humlinda mtu kuliko fahari yoyote.
28Mwanangu usiishi maisha ya kuombaomba,
ni afadhali kufa kuliko kuombaomba.
29Mtu anapomtegemea mwingine ampe chakula,
anaishi maisha ambayo hayastahili utu.
Kutegemea chakula cha mwingine ni kujiaibisha;
mtu mwenye akili, aliyefunzwa vema ataepa kuishi hivyo.
30Kwa mtu asiye na aibu kuombaomba ni kutamu,
lakini ndani yake kuna moto unaomchoma.