The chat will start when you send the first message.
1Fahari ya huko juu ni uangavu wa anga lake;
anga laonekana kumetameta kwa fahari yake.
2Jua litokezapo linatangaza likingaa.
Hilo ni kitu cha ajabu alichoumba Mungu Mkuu.
3Mchana laikausha ardhi,
nani awezaye kustahimili joto lake?
4Mtu huchochea tanuri na kusikia joto lake,
lakini jua huichoma milima mara tatu zaidi.
Jua hupuliza mionzi yake ya moto,
na miali yake mikali hupofusha macho.
5Jinsi gani alivyo mkuu Bwana aliyeliumba,
na ambaye kwa amri yake laendelea na mkondo wake.
6Vilevile mwezi huangaza kwa wakati wake,
nao ni alama ya milele;
huongoza nyakati na majira.
7Nyakati za sikukuu hutambuliwa kwa mwezi;
mwanga wake huwa mkubwa halafu hupungua.
8“Mwezi” wa kalenda jina lake latokana na mwezi,
hukua kwa namna ya ajabu katika vipindi vyake;
wenyewe ni ishara ya majeshi ya angani
ukingaa katika anga la mbinguni.
9Mngao wa nyota unaonesha uzuri wa anga
mapambo mazuri sana katika mbingu za juu za Bwana.
10Kwa amri yake yeye Mtakatifu
zinasimama mahali zilipopangiwa;
kamwe hazikiuki jukumu lao la ulinzi.
11Tazama upinde wa mvua, umsifu yeye aliyeuumba!
Upinde wa mvua ni mzuri mno kwa mngao wake!
12Hulizingira anga kwa nusu mzingo wake mzuri,
mikono ya Mungu Mkuu imeutandaza.
13Kwa amri yake Bwana hupeleka theluji,
na umeme humulika anapoamuru.
14Kadhalika ghala zake hufunguka,
mawingu yakaruka kutoka humo kama ndege.
15Kwa ukuu wake huyakusanya mawingu,
na kuipasua barafu ikawa mvua ya mawe.
16Atokeapo, milima hutetemeshwa,
kwa kutaka kwake upepo wa kusi huvuma.
17Sauti yake ya ngurumo huikemea nchi,
kadhalika na upepo wa kaskazi na kimbunga.
Huitawanya theluji ikashuka chini kama ndege,
kama vile nzige wanaotua.
18Tunashangaa kuona uzuri wa weupe wake,
na kustaajabia kuanguka kwake.
19Hutawanya ukungu juu ya nchi kama chumvi,
na unapoganda huweko vitu vilivyochongoka kama miiba.
20Huvumisha upepo baridi wa kaskazi,
barafu ikaganda juu ya maji,
ikafunika madimbwi yote ya maji,
ikiwa kama ngao ya kujikingia.
21Huiteketeza milima na kuchoma nyika,
akazinyausha nyasi changa kama kwa moto.
22Lakini ukungu hurekebisha tena kila kitu,
umande unapotokea na kuburudisha.
23Kwa hekima yake aliituliza bahari kuu,
na kuweka huko visiwa.
24Wanaosafiri baharini husimulia hatari zake,
nasi tunashangaa juu ya hayo tunayosikia.
25Baharini mna viumbe vya ajabu na vya kushangaza,
viumbe vikubwa mno na aina zote za viumbe hai.
26Bwana humwezesha kila mjumbe wake kufaulu,
kwa neno lake kila kiumbe hushikishwa pamoja.
27Ingawa tunasema mengi, hatuwezi kufikia mwisho wao,
kwa kifupi: “Bwana ni kila kitu.”
28Tupate wapi nguvu ya kumsifu?
Maana yeye ni mkuu kuliko kazi zake zote.
29Bwana ni wa kutisha na mkuu sana,
nguvu zake ni za ajabu mno.
30Unapomsifu Bwana, msifu kadiri uwezavyo,
maana yeye, anastahili zaidi ya hayo yote.
Unapomtukuza, mtukuze kwa nguvu zako zote.
Wala usichoke maana huwezi kumsifu yeye ipasavyo.
31Nani aliyemwona, akaweza kueleza alivyo?
Au, nani awezaye kumtukuza ipasavyo?
32Maajabu mengi makuu kuliko haya, yamefichika,
maana tumeziona tu kazi zake chache.
33Maana Bwana amefanya vitu vyote,
akawapa heshima wale wamchao.