Sira 47

Sira 47

Nathani

1Baada yake alitokea Nathani;

yeye alikuwa nabii siku za Daudi.

Daudi

2Kama vile mafuta ya tambiko ya amani yanavyochaguliwa na kutengwa kwa ajili ya Bwana,

ndivyo na Daudi alivyoteuliwa miongoni mwa watu wa Israeli.

3Alicheza na simba kana kwamba ni wanambuzi

na dubu kana kwamba ni wanakondoo.

4Wakati wa ujana wake aliliua jitu,

akawaondolea watu wake matukano yake.

Alirusha jiwe kwa kombeo lake,

likamwangusha Goliathi, mwenye majivuno.

5Maana alimsihi Bwana, Mungu Mkuu

naye akauimarisha mkono wake wa kulia,

apate kumuua adui mwenye nguvu vitani,

na kukuza nguvu za watu wake.

6Watu walimsifu kwa kuua maadui 10,000,

na kumshangilia kwa baraka za Bwana

wakati alipovikwa taji la kifalme.

7Aliwafagilia mbali maadui zake pande zote,

na kuwatokomeza kabisa Wafilisti;

alizivunjavunja nguvu zao mpaka leo.

8Katika yote aliyoyatenda Daudi,

alimshukuru na kumtukuza yule Mtakatifu Mungu Mkuu.

Alimpenda Muumba wake

na kumwimbia sifa kwa moyo wake wote.

9Aliwaweka waimbaji mbele ya madhabahu,

ili kwa sauti zao waimbe nyimbo tamu.

10Sikukuu alizifanya ziwe nzuri,

na kuzipangia nyakati zake mwaka mzima,

wakati watu waliposifu jina takatifu la Mungu,

na hekalu kujaa nyimbo nzuri tangu asubuhi.

11Bwana alimwondolea Daudi dhambi zake,

na kuikuza nguvu yake milele;

alimjalia haki ya kuwa mfalme,

akaweka kiti cha enzi kitukufu katika Israeli.

Solomoni

12Baada ya Daudi alifuata mwanawe mwenye hekima

ambaye aliishi kwa amani kwa sababu yake.

13Solomoni alitawala wakati wa amani.

Mungu alimjalia amani pande zote,

ajenge nyumba kwa heshima ya jina lake,

na kutayarisha hekalu la kudumu milele.

14Kweli ulikuwa na hekima ewe Solomoni ulipokuwa kijana!

Ulitiririka busara kama mto!

15Ulijulikana duniani kwa maarifa yako,

na kuijaza methali na vitendawili.

16Jina lako lilijulikana mpaka visiwa vya mbali,

watu wakakupenda kwa kuwaletea amani.

17Kwa nyimbo, methali, mifano na maelezo yake,

nchi zilishikwa na mshangao.

18Kwa heshima ya jina la Bwana Mungu

ambaye anaitwa Mungu wa Israeli,

ulikusanya dhahabu kama bati, na fedha kama madini ya risasi.

19Lakini ukautoa mwili wako kwa wanawake,

ukawa mtumwa wa tamaa zako.

20Uliitia doa heshima yako,

na kuutia unajisi ukoo wako,

hata ukawaletea wazawa wako adhabu,

wakahuzunishwa kwa sababu ya upumbavu wako.

21Hata ufalme ukagawanyika sehemu mbili,

ufalme pinzani ukatokea huko Efraimu.

22Lakini Bwana hataacha kuwa na huruma,

wala kuruhusu kazi yake yoyote iharibike;

hatawafutilia mbali wazawa wa Daudi, mteule wake,

wala kuangamiza ukoo wa huyo aliyempenda.

Kwa hiyo alimwachia Yakobo mabaki,

na Daudi mzizi wa jamaa yake.

Rehoboamu na Yeroboamu

23Solomoni akafariki kama wazee wake,

akamwacha mmoja wa watoto wake kuwa mtawala.

Huyo alikuwa Rehoboamu, mwingi wa upumbavu na mtovu wa busara,

ambaye maongozi yake yaliwafanya watu wakaasi.

Kulikuwa pia na Yeroboamu mwana wa Nebati,

aliyewasababisha Waisraeli kutenda dhambi,

na kuwaongoza Waefraimu katika njia ya dhambi.

24Dhambi zao zilizidi kuwa nyingi mno,

hata zikasababisha waondolewe nchini mwao.

25Maana walijaribu kutenda kila aina ya uovu,

mpaka Bwana alipowalipiza kisasi.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania