The chat will start when you send the first message.
1Usimwonee wivu mke umpendaye;
utakuwa umemfundisha namna ya kukudhuru.
2Usimwachie mwanamke ukuu wako,
la sivyo atakutawala kabisa.
3Usifuatane na mwanamke wa tabia mbaya,[#9:3 Kigiriki: Mwanamke mwenye tabia mbaya.]
la sivyo utanaswa katika mitego yake.
4Usishirikiane na mwanamke mwanamuziki,
la sivyo, utanaswa kwa werevu wake.
5Usimtazame kijana msichana mzuri;
la sivyo, wewe na yeye mtapata adhabu ileile.
6Usimpe malaya moyo wako,
la sivyo utapoteza nchi yako yote.
7Usipepesepepese macho mitaani mjini,
wala kuzururazurura kwenye maeneo yake ya pekee.
8Usimtazame mwanamke mzuri,
usimkodolee macho mwanamke mrembo asiye wako.
Maana wengi wameangushwa kwa uzuri wa mwanamke,
maana jambo hilo hufanya tamaa kuwaka kama moto.
9Kamwe usiketi na mke wa mtu,
wala kuketi naye kunywa pombe;
la sivyo moyo wako utampenda
nawe utakosa kujizuia ukaangamia.
10Usimtupe rafiki wa miaka mingi,
maana rafiki mpya hatalingana naye.
Rafiki mpya ni kama divai mpya;
divai ya miaka mingi hunywewa kwa furaha.
11Usimwonee kijicho mwenye dhambi akifanikiwa,
maana hujui mwisho wake utakuwaje.
12Usifurahie yanayowapendeza wasiomcha Mungu.
Kumbuka hawataepa kuadhibiwa hapahapa duniani.
13Kaa mbali na mtu anayeweza kukuua,
nawe hutakuwa na wasiwasi wa kuuawa.
Kama ukimkaribia, uwe na tahadhari;
la sivyo, utayaangamiza maisha yako.
Ujue kuwa unatembea kwenye mtego hatari,
na kwamba unatembea kwenye uwanja wa vita.
14Wafahamu jirani zako kadiri uwezavyo
na kuwaomba ushauri watu wenye hekima.
15Mazungumzo yako yawe na wenye akili,
na mazungumzo yako yote yahusu sheria ya Mungu Mkuu.
16Watu wanyofu wawe wenzako katika kula,
majivuno yako yawe katika kumcha Bwana.
17Kazi ya mtu mwenye juhudi itapata sifa;
kiongozi wa watu sharti awe hodari katika maneno yake.
18Mtu aropokaye ni kitisho mjini kwake;
mtu wa maneno ya ovyo huchukiwa.