Tobiti 10

Tobiti 10

Mahangaiko ya Tobiti na Ana

1Huko nyuma, kila siku Tobiti alikuwa akihesabu siku zilizohitajiwa kwenda Rage na kurudi. Siku hizo zikapita na mwanawe Tobia akawa bado hajarudi. Basi, Tobiti akafikiri:

2“Je, labda amecheleweshwa huko? Huenda Gabaeli alikwisha kufa na hakuna mtu wa kumpa mwanangu ile fedha!”

3Tobiti akaanza kuwa na wasiwasi.

4Naye Ana, mkewe akawa anasema, “Mwanangu amekufa! Hayuko tena duniani!” Akaanza kulia na kumwombolezea mwanawe.

5Akaendelea kusema, “Ole wangu mwanangu! Kwa nini nilikuacha uondoke ewe mwanangu uliye mwanga wa macho yangu?”

6Naye Tobiti akamwambia, “Tulia, dada, usihangaike. Hajambo; bila shaka kuna kitu kinachowachelewesha huko. Yule mwenzake ni mtu wa kuaminika tena ni jamaa yetu. Usife moyo mpenzi wangu; atarudi upesi.”

7Lakini Ana akamjibu, “Niache usijaribu kunidanganya! Mwanangu amekufa!”

Ikawa kila siku Ana alikuwa akitoka haraka nyumbani na kushinda kwenye barabara aliyoichukua Tobia wakati alipoanza safari yake, maana hakumwamini mtu mwingine. Jua lilipotua alirudi nyumbani akaomboleza na kulia usiku kucha bila kupata usingizi.

Kuondoka Ekbatana

Basi, yale majuma mawili ya sherehe ambayo Ragueli alikuwa ameapa kumfanyia binti yake yakaisha. Kwa hiyo Tobia akamwendea Ragueli akamwambia, “Tafadhali, uniache nirudi nyumbani, maana najua kwamba wazazi wangu hawana tena matumaini ya kuniona tena. Basi, nakuomba baba uniache niende nyumbani kwa baba yangu. Nimekwisha kukueleza hali niliyomwacha nayo nilipoondoka.”

8Lakini Ragueli akamwambia Tobia, “Kaa kidogo, kaa nami, mwanangu. Nitawatuma wajumbe wampelekee habari zako.”

9Lakini Tobia akasisitiza, “La! Tafadhali uniache nirudi nyumbani kwa baba yangu.”

10Basi, Ragueli akamkabidhi Tobia mke wake yaani Sara, bila kukawia, akampa pia nusu ya mali yake yote: Watumwa wa kike na wa kiume, ng'ombe, kondoo, fedha na vyombo kadha wa kadha.

11Basi, akawaacha waende kwa furaha halafu akamkumbatia Tobia na kumwaga akisema, “Kwa heri mwanangu. Safiri salama. Bwana Mungu wa mbinguni, akuongoze wewe na mkeo nami nijaliwe kuwaona watoto wenu kabla sijafa.”

12Kisha akambusu binti yake Sara na kusema, “Nenda sasa nyumbani kwa baba mkwe wako, kwani tangu sasa wazazi wa mumeo ni wazazi wako kama sisi tulivyo wazazi wako. Nenda kwa amani, binti yangu. Natumaini kusikia mema juu yako kadiri niishivyo.” Kisha akawaaga na kuwaacha waende zao. Naye Edna akamwambia Tobia, “Mwanangu mpendwa na ndugu Tobia, Bwana wa mbinguni akurudishe tena salama! Nami natumaini kuishi hata niwaone watoto wako na binti yangu Sara kabla sijafa. Mbele ya Bwana namkabidhi binti yangu mikononi mwako. Kamwe usimhuzunishe maishani mwako. Nenda kwa amani mwanangu. Tangu sasa mimi ni mama yako na Sara ni dada yako mpendwa. Na sote tuishi kwa amani siku zote za maisha yetu!” Basi akawabusu wote wawili na kuwaacha kwa furaha.

13Tobia aliondoka kwa Ragueli amejaa furaha, akimtukuza Mungu wa mbingu na dunia, Mfalme wa vyote, kwa kuifanikisha safari yake. Kisha aliwatakia Ragueli na mkewe Edna baraka akisema, “Furaha yangu na iwe kuwaheshimu nyinyi siku zote za maisha yangu!”

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania