Tobiti 14

Tobiti 14

1Hapa yaishia maneno ya shukrani ya Tobiti.

Mawaidha ya mwisho ya Tobiti

2Tobiti alikufa kwa amani mwenye umri wa miaka 112, akazikwa kwa heshima huko Ninewi. Alikuwa na miaka 62 alipopofuka macho. Baada ya kuponywa kwake aliishi kwa fanaka akawasaidia maskini na kuendelea kumsifu Mungu na kuadhimisha ukuu wake.

3Alipokuwa karibu kufa alimwita mwanawe Tobia akampa mawaidha haya:

4“Mwanangu, wachukue watoto wako na uende nao kwa haraka kule Media, maana naamini neno la Mungu lililotamkwa na nabii Nahumu dhidi ya Ninewi litatimia. Kila kitu wajumbe wa Mungu, yaani manabii wa Israeli, walichosema dhidi ya Ninewi na Ashuru kitatokea kwa wakati wake. Hakuna walichosema kitakachobatilika. Nyinyi mtakuwa salama zaidi huko Media kuliko kukaa Ashuru au Babuloni. Mimi najua na kusadiki kwamba kila kitu alichosema Mungu kitatimia, na hakuna hata neno moja kati ya hayo yote yaliyotabiriwa litabatilika.

“Ndugu zetu waishio nchini Israeli watahesabiwa wote na kuchukuliwa mbali na nchi hiyo nzuri. Nchi yote ya Israeli itakuwa mahame; miji ya Samaria na Yerusalemu itaachwa mitupu, nayo nyumba ya Mungu itachomwa moto na kubaki gofu kwa kitambo.

5Kisha Mungu atawahurumia tena watu wake na kuwarudisha tena nchini Israeli. Watajenga upya nyumba yake ingawa haitakuwa nzuri kama ile ya kwanza mpaka wakati wake utakapotimia. Lakini baada ya hayo watu wote wa Israeli watarudi kutoka uhamishoni, watajenga upya mji wa Yerusalemu katika fahari yake yote nayo nyumba ya Mungu itajengwa humo upya kama manabii wa Israeli walivyotabiri.

6“Watu wote wa dunia nzima wataongoka na kumcha Mungu kwa ukweli wote. Wote watatupilia mbali miungu yao ya uongo iliyowapotosha na watamtukuza Mungu wa nyakati zote kwa uadilifu.

7Watu wote wa Israeli waliosalimishwa siku hizo watamkumbuka Mungu kwa moyo wote. Watakuja na kukutanika pamoja huko Yerusalemu na baadaye wataishi kwa usalama katika nchi ya Abrahamu ambayo itakuwa yao. Wote wanaompenda Mungu kwa kweli watafurahi, lakini wale wanaotenda dhambi na uovu watatoweka duniani.

8Na sasa, wanangu nawapeni mwongozo wangu. Mtumikieni Mungu kwa moyo wote na kufanya yale yanayompendeza.

9Wapeni watoto wenu jukumu la kuishi kwa unyofu, kuwasaidia maskini, kumkumbuka Mungu na kulitukuza jina lake daima, kwa moyo wote na kwa nguvu zao zote.

10“Basi, mwanangu ondoka Ninewi, usikae hapa. Mara tu utakapomaliza kumzika mama yako kaburini kando yangu, ondoka siku hiyohiyo ikiwezekana, wala usingojengoje nchini humu ambamo naona uovu na kufuru vinatawala bila aibu. Kumbuka mambo yote Nadabu aliyomtendea Ahika, mjomba wake, na mlezi wake. Je, si alimfanya ashukie kaburini akiwa mzima. Lakini Mungu alimfanya huyo mhalifu Nadabu apate adhabu ya uovu wake mbele ya Ahika, kwani Ahika alirudi katika mwanga wa mchana bali Nadabu alitumbukizwa kwenye giza la milele kama adhabu ya kupanga kumwua Ahika. Kwa sababu ya matendo yake mema Ahika hakunaswa na mtego aliotegewa na Nadabu bali Nadabu alinaswa humo na kuangamia.

11Basi, wanangu mnaona faida ya kuwasaidia maskini na jinsi mauti yanavyowangojea watu wanaowatendea wengine maovu. Lakini sasa roho inanitoka!”

Basi, wakamlaza Tobiti kitandani mwake. Tobiti alikufa, akazikwa kwa heshima.

12Baadaye kidogo naye mke wa Tobiti akaaga dunia, naye Tobia akamzika karibu na baba yake. Kisha Tobia, mkewe na watoto wao wakaondoka kwenda Media. Tobia aliishi huko Ekbatana pamoja na Ragueli, baba mkwe wake.

13Tobia aliwatunza Edna na Ragueli katika uzee wao, akawapa heshima kubwa. Na walipofariki, aliwazika huko Ekbatana nchini Media. Tobia akarithi mali ya Ragueli licha ya ile ya Tobiti, baba yake.

14Alipofikia umri wa miaka 127, Tobia alifariki kule Ekbatana.

15Kabla ya kufa alishuhudia kuangamizwa kwa Ninewi. Aliwaona Waninewi wanachukuliwa mateka na kupelekwa uhamishoni Media na mfalme Ahasuero wa Media. Tobia alimsifu Mungu kwa jinsi alivyokuwa amewaadhibu watu wa Ninewi na Ashuru. Alimtukuza Bwana Mungu milele na milele, Amina.

Biblia Habari Njema kwa Watu Wote (Yenye Vitabu vya Deuterokanoni): Tafsiri ya Ushirikiano wa Makanisa (BHN): Hakimiliki -1995, 2001: kwa Chama cha Biblia cha Tanzania na Chama cha Biblia cha Kenya. Haki zote zimehifadhiwa.
Published by: Bible Society of Tanzania