The chat will start when you send the first message.
1Adamu alimzaa Sethi, Sethi akamzaa Enoshi, Enoshi akamzaa Kenani,[#1:1—9:44 Sura nane za kwanza za 1 Nyakati zinatumia orodha za nasaba ambazo zinampeleka msomaji tangu yule binadamu wa kwanza (Adamu) ambaye Mungu alimbariki, kisha Noa ambaye Mungu alifanya naye agano lingine, mpaka Abrahamu, mpaka Daudi. Lengo ni kuonesha kwamba taifa la Israeli liliteuliwa miongoni mwa mataifa yote ya dunia. Orodha hiyo inamweka Daudi katika nafasi maalumu kwa vile Mungu alifanya agano naye, na kabila la Lawi kwa kuwa lilihusika na ibada kwa Mwenyezi-Mungu. Wakati wa mwandishi, yapata wakati ule Wayahudi waliporuhusiwa kurudi makwao kutoka Babuloni, mwandishi anaona jumuiya hiyo iliyorudi kutoka uhamishoni na kuanza kutengeneza upya maishi ya kidini ya watu wa Mungu, inaendelea na mpango wa Mungu: Adamu … Noa … Abrahamu … Israeli (Yakobo)… Daudi, hekalu.]
2Kenani akamzaa Mahalaleli, Mahalaleli akamzaa Yaredi,
3Yaredi akamzaa Henoki, Henoki akamzaa Methusela. Methusela alimzaa Lameki,
4Lameki akamzaa Noa. Noa alikuwa na wana watatu: Shemu, Hamu na Yafethi.[#1:1-23 Taz Mwa 5:1-32. Hapa orodha hiyo au nasaba inatolewa bila vitu vidogovidogo (kadiri ya mwandishi wa Nyakati) ambavyo si vya lazima kwa lengo lake. Ni kana kwamba mwandishi anaharakisha kumfikia Noa na kisha kuanza orodha ya wanawe ambayo itakuwa na matawi yake.]
5Wana wa Yafethi walikuwa Gomeri, Magogu, Madai, Yavani, Tubali, Mesheki na Tirasi.[#1:5-7 Taz Mwa 10:2-4. Maeneo ya wazawa wa Yafethi, kwa wingi, yalikuwa Asia Ndogo na sehemu za juu za Mto Eufrate.]
6Wana wa Gomeri walikuwa Ashkenazi, Difathi na Togama.
7Wana wa Yavani walikuwa Elisha, Tarshishi, Kitimu na Rodanimu.[#1:7 Tafsiri kulingana na baadhi ya hati za kale za Kiebrania. Pengine ni “Dodanimu” kwa kuwa herufi “d” na “r” katika Kiebrania zinafanana sana.]
8Wana wa Hamu walikuwa Kushi, Misri, Puti na Kanaani.[#1:8-16 Taz Mwa 10:6-7. Wazawa wa Hamu walimiliki maeneo ya mwambao wa kaskazini-mashariki ya bahari ya Mediteranea, Kanaani na kuenea mashariki mpaka miji ya Babuloni, Ninewi (Ashuru), ambao ulikuwa pia karibu na Mto Eufrate. Kulingana na Mwa 10:8-11 Nimrodi, mmoja wa wazawa wa Hamu, alikuwa mwanzilishi wa dola la Ashuru. Nabii Mika anataja nchi ya Ashuru kama nchi ya Nimrodi (Mika 5:5). Wayebusi, Waamori n.k. walikuwa kule Kanaani kabla ya Waisraeli kuingia humo (Hes 21:21-35). Inajulikana kwamba nchi ya Kanaani ni ile nchi ambayo inasemwa Mungu alimwahidi Abrahamu kuwa yake na ya wazawa wake (Mwa 15:7; 17:7-8).]
9Wana wa Kushi walikuwa Seba, Havila, Sabta, Raama na Sabteka. Wana wa Raama walikuwa Sheba na Dedani.
10Kushi alimzaa Nimrodi, aliyekuwa mtu shujaa wa kwanza duniani.
11Wazawa wa Misri ni Waludi, Waanamu, Walehabi, Wanaftuhi,
12Wapathrusi Wakaftori na Wakasluhi (hao ndio asili ya Wafilisti).
13Wana wa Kanaani walikuwa Sidoni, mzaliwa wake wa kwanza, na Hethi.
14Kanaani pia ndiye babu yao Wayebusi, Waamori, Wagirgashi,
15Wahivi, Waarki, Wasini,
16Waarvadi, Wasemari na Wahamathi.
17Wana wa Shemu walikuwa Elamu, Ashuri, Arpaksadi, Ludi, Aramu, Usi, Huli, Getheri na Mesheki.
18Arpaksadi alimzaa Shela, Shela akamzaa Eberi.
19Eberi alikuwa na wana wawili; mmoja wao aliitwa Pelegi, (kwa maana wakati wake watu walikuwa wametawanyika duniani), na ndugu yake aliitwa Yoktani.[#1:19 Jina hili “Pelegi” kwa Kiebrania linafanana na neno lenye maana ya “waligawanyika”. Taz Mwa 10:25. Na pia simulizi la 11:1-9 jinsi Mungu alivyowatawanya makabila yale kila mahali duniani kwa kuvuruga lugha zao.]
20Wana wa Yoktani walikuwa Almodadi, Shelefu, Hasarmawethi, Yera,
21Hadoramu, Uzali, Dikla,
22Obali, Abimaeli, Sheba,
23Ofiri, Havila na Yobabu. Hao watu ni wana wa Yoktani.
24Ukoo wa Abrahamu kutokea Shemu ni kama ifuatavyo: Shemu alimzaa Arpaksadi, naye Arpaksadi akamzaa Shela.
25Shela akamzaa Eberi, Eberi akamzaa Pelegi, Pelegi akamzaa Reu;
26Reu akamzaa Serugi, Serugi akamzaa Nahori, Nahori akamzaa Tera,
27na Tera akamzaa Abramu, ambaye ndiye Abrahamu.
28Abrahamu alikuwa na watoto wawili wa kiume: Isaka na Ishmaeli.
29Hivi ndivyo vizazi vyao: mzaliwa wa kwanza wa Ishmaeli alikuwa Nebayothi na wengine ni Kedari, Adbeeli, Mibsamu,
30Mishma, Duma, Masa, Hadadi, Tema,
31Yeturi, Nafishi na Kedema. Hao ndio wana wa Ishmaeli.
32Abrahamu alikuwa na suria aliyeitwa Ketura. Ketura alimzalia Abrahamu: Zimrani, Yokshani, Medani, Midiani, Ishbaki na Shua. Wana wa Yokshani walikuwa Sheba na Dedani.[#1:28-33 Taz Mwa 25:1-4. Wazawa wa Abrahamu na Ketura walikuwa wazee wa kwanza wa baadhi ya makabila ya Waarabu pamoja na Wamidiani ambao walikuwa kabila la mkewe Mose na baba yake aitwaye Yethro (Kut 2:15-22; 18:1).]
33Wana wa Midiani walikuwa: Efa, Eferi, Henoki, Abida na Eldaa. Wote hao walikuwa wazawa wa Ketura.
34Isaka, mwana wa Abrahamu, alikuwa na wana wawili: Esau na Israeli.[#1:17-34 Taz Mwa 10:21-29. Mwandishi anachukua kwamba Shemu alikuwa babu wa Waebrania (Eberi) aya 18,19 (Mwa 10:21) na kumtaja “Abramu ambaye ndiye Abrahamu” ni jambo mwafaka katika mpango wa mwandishi wa Mambo ya Nyakati. Mwandishi atataja wazi katika aya 34 “Abrahamu alikuwa na wana wawili: Esau na Israeli”. Abrahamu ni kiungo maalumu cha ile jumuiya ya wateule wa Mungu.]
35Wana wa Esau walikuwa Elifazi, Reueli, Yeushi, Yalamu na Kora.
36Wana wa Elifazi walikuwa Temani, Omari, Sefo, Gatamu, Kenazi, Timna na Amaleki.
37Wana wa Reueli walikuwa Nahathi, Zera, Shama na Miza.
38Wana wa Seiri walikuwa Lotani, Shobali, Sibeoni, Ana, Dishoni, Eseri na Dishani.
39Wana wa Lotani walikuwa wawili: Hori na Homamu. Lotani alikuwa na dada yake aliyeitwa Timna.
40Wana wa Shobali walikuwa Alvani, Manahathi, Ebali, Shefi na Onamu. Wana wa Sibeoni walikuwa Aya na Ana.
41Mwana wa Ana alikuwa Dishoni; na wana wa Dishoni walikuwa Hamrani, Eshbani, Ithrani na Kerani.[#1:41 Kulingana na hati kadhaa za kale. Katika Mwa 36:26 ni “Hemdani”.]
42Wana wa Eseri walikuwa Bilhani, Zaawani na Akani; na wana wa Dishoni walikuwa Usi na Arani.[#1:42 Katika Mwa 36:28 ni “Dishani”.]
43Wafuatao ndio wafalme waliotawala nchi ya Edomu kabla mfalme yeyote hajatawala Waisraeli: Bela mwana wa Beori alitawala nchi ya Edomu, akiwa na makao yake makuu katika mji wa Dinhaba.[#1:35-54 Nchi ya “Edomu” au “Seiri” ilikuwa kusini-mashariki mwa Bahari ya Chumvi. Waedomu walikuwa wazawa wa Esau (Mwa 36:1-43). Wazawa wa Yakobo (Waisraeli) walipigana mara kwa mara na Waedomu (Hes 20:14-21; Oba 9-10).]
44Bela alipofariki, Yobabu mwana wa Zera kutoka Bosra alitawala badala yake.
45Yobabu alipofariki, Hushamu wa nchi ya Watemi alitawala badala yake.
46Hushamu alipofariki, Hadadi mwana wa Bedadi alitawala badala yake, makao yake makuu yakiwa katika mji wa Avithi. Huyu ndiye aliyewapiga na kuwashinda Wamidiani katika nchi ya Moabu.
47Hadadi alipofariki, Samla kutoka Masreka alitawala badala yake.
48Samla alipofariki, Shauli kutoka Rehobothi ulio karibu na mto Eufrate, alitawala badala yake.
49Shauli alipofariki, Baal-hanani mwana wa Akbori alitawala badala yake.
50Baal-hanani alipofariki, Hadadi kutoka Pai alitawala badala yake na jina la mkewe Akbori lilikuwa Mehetabeli, binti Matredi, binti Mezahabu.
51Naye Hadadi akafariki.
Wakuu wa makabila ya Edomu walikuwa Timna, Alva, Yethethi,
52Oholibama, Ela, Pinoni,
53Kenazi, Temani, Mibsari,
54Magdieli na Iramu. Hao ndio wakuu wa makabila ya Edomu.