The chat will start when you send the first message.
1Basi Daudi akasema, “Hapa ndipo mahali ambapo nyumba ya Mwenyezi-Mungu itakuwa, na hii ndiyo madhabahu ambapo watu wa Israeli watatolea sadaka ya kuteketezwa.”
2Daudi akatoa amri wageni waliokuwa wanaishi katika nchi ya Israeli wakusanyike, naye akawapangia kazi. Akaweka waashi wachonge vizuri mawe ya kujenga nyumba ya Mungu.[#22:2 Hawa walikuwa watu wasio Waisraeli ikiwa ni pamoja na wazawa wa Wakanaani au watumwa waliotekwa vitani. Kushiriki kwa wageni katika ujenzi wa hekalu la kwanza (ingawaje kwa kulazimishwa) kunafanana na kushiriki kwa wageni wakati wa ujenzi mpya wa hekalu wakati wa Ezra na Nehemia baada ya Waisraeli kurudi kutoka uhamishoni kule Babuloni (Isa 60:10-12).]
3Daudi pia akaweka akiba tele ya chuma cha kutengenezea misumari na mafungo ya malango ya nyumba, na akiba tele ya shaba isiyopimika.
4Mbao za mierezi ambazo Daudi aliletewa na Wasidoni na Watiro zilikuwa hazihesabiki.[#22:4 Au, “mikangazi”. Neno “mwerezi” katika tafsiri hii linajaribu kutaja aina ya mti unaohusika katika Biblia ambao ni kama mti wa mkangazi, mgumu na mzuri wa kujengea na pia wenye harufu nzuri kidogo. Miti hiyo ilipatikana kwa wingi kule Lebanoni (rejea Ezra 3:7).]
5Daudi akajisemea, “Nyumba ambayo mwanangu Solomoni atamjengea Mwenyezi-Mungu itakuwa ya fahari sana, ya kusifika na tukufu duniani kote. Lakini kwa vile yeye bado angali kijana na bado hana uzoefu mwingi, afadhali nimfanyie matayarisho.” Hivyo basi, Daudi akaweka akiba kubwa sana ya vitu vya ujenzi kabla hajafariki.
6Ndipo Daudi akamwita Solomoni mwanawe, akamwagiza amjengee Mwenyezi-Mungu, Mungu wa Israeli nyumba.
7Daudi akamwambia Solomoni, “Mwanangu, nilikusudia moyoni mwangu kumjengea Mwenyezi-Mungu, Mungu wangu nyumba ili kumtukuza.
8Lakini Mwenyezi-Mungu aliniambia, ‘Wewe umemwaga damu nyingi kwa kupigana vita vikubwa. Kwa sababu ya damu nyingi ambayo umemwaga mbele yangu hapa duniani, hutanijengea nyumba.
9Hata hivyo, utapata mwana, ambaye atatawala kwa amani kwa sababu nitampa amani na maadui zake wote wa jirani. Jina lake litakuwa Solomoni, kwa maana katika siku za utawala wake, atailetea Israeli amani na utulivu.[#22:9 Jina Solomoni katika Kiebrania linasikika kama neno “Shalom” ambalo maana yake ni “amani”. Solomoni alitawala wakati wa amani hali Daudi daima alitumia wakati wake mwingi zaidi kupigana vita na umwagaji wa damu kwa upande wake ulimfanya asifae kumjengea Mungu hekalu (1Fal 5:3-4).]
10Hivyo, yeye ndiye atakayenijengea nyumba. Atakuwa mwanangu nami nitakuwa baba yake, na wazawa wake wataitawala Israeli milele.’
11Sasa mwanangu, Mwenyezi-Mungu, Mungu wako na awe pamoja nawe ili ufaulu kumjengea nyumba kama alivyosema.
12Mwenyezi-Mungu akupe busara na akili ili atakapokupa uongozi juu ya Israeli, uzishike sheria zake Mwenyezi-Mungu, Mungu wako.[#22:12-13 Solomoni alijaliwa na Mungu busara na akili, vipaji ambavyo vinaendana na hekima. Katika Biblia hekima hiyo anapewa mtu ambaye anazishika sheria na maagizo ya Mwenyezi-Mungu (taz Meth 1:7; 2:4-7). Ni hivyo pia katika tamaduni za makabila mengi ya Kiafrika: wazee wenye hekima ni wale wanaojali maagizo ya Mungu.]
13Ukiwa mwangalifu, na ukizitii amri ambazo Mwenyezi-Mungu alimwagiza Mose juu ya Israeli, utastawi. Jipe moyo, uwe imara. Usiogope wala usifadhaike.[#22:13 Maneno ya Daudi kwa Solomoni yanafanana na yale Mungu aliyomwambia Yoshua, katika Yos 1:6-9.]
14Kwa juhudi kubwa, nimeiwekea akiba nyumba ya Mwenyezi-Mungu, talanta 100,000 za dhahabu, talanta 1,000,000 za fedha na idadi isiyopimika ya shaba na chuma, kwani ni nyingi sana. Nimeandaa mbao na mawe tayari. Lakini huna budi kuongezea.
15Unao wafanyakazi wengi: kuna wachonga mawe, waashi, maseremala na mafundi wa kila aina wenye ujuzi mwingi;
16wa kufua dhahabu, fedha, shaba na chuma. Haya! Anza kazi! Mwenyezi-Mungu na awe pamoja nawe!”
17Zaidi ya hayo, Daudi aliwaamuru viongozi wote wa Waisraeli wamsaidie Solomoni mwanawe, akisema,
18“Je, Mwenyezi-Mungu Mungu wenu hayuko pamoja nanyi? Je, hajawapa amani katika pande zote? Yeye aliwatia wakazi wa nchi hii mikononi mwangu na sasa wako chini ya Mwenyezi-Mungu na watu wake.
19Sasa, mtumikieni Mwenyezi-Mungu, Mungu wenu, kwa nia na moyo wote. Shime basi! Mjengeeni Mwenyezi-Mungu mahali patakatifu ili sanduku la agano la Mwenyezi-Mungu pamoja na vyombo vyote vitakatifu vitumiwavyo katika ibada, viwekwe ndani ya nyumba iliyojengwa kwa ajili ya Mwenyezi-Mungu.”