1 Mambo ya Nyakati 4

1 Mambo ya Nyakati 4

Wazawa wa Yuda

1Wana wa Yuda walikuwa Peresi, Hesroni, Karmi, Huri na Shobali.[#4:1-23 Sehemu hii ambayo inaweza kugawanyika katika visehemu vitatu (4:1-10; 4:11-20 na 4:21-23) ni orodha nyingine ya wazawa wa Yuda ambayo ni ziada ya ile ya 2:1-8. Majina mengi yanayotajwa hapa hayajulikani pengine katika A.K. Tena majina mengine ya watu yamechanganyika na majina ya kijiografia.]

2Reaya, mwana wa Shobali, alimzaa Yahathi, aliyekuwa baba yake Ahumai na Lahadi, hizo ndizo jamaa za Wasorathi.

3Wana wa Etamu walikuwa Yezreeli, Ishma na Idbashi. Walikuwa na dada mmoja aliyeitwa Haselelponi.[#4:3 Hapa tu katika Biblia yote na sababu ya kutajwa kwake si dhahiri.]

4Penueli aliwazaa Gedori na Ezeri, na Ezeri akamzaa Husha. Hao ndio wazawa wa Huri mzaliwa wa kwanza wa Efratha, baba yake Bethlehemu.

5Ashuru, mwanzilishi wa mji wa Tekoa, alikuwa na wake wawili: Hela na Naara.[#4:3-5 Kuhusu “Bethlehemu” taz 2:51 maelezo. Kuhusu “Tekoa” itakumbukwa kwamba hicho kilikuwa kijiji alimotoka nabii Amosi (Amo 1:1).]

6Naara alimzalia wana wanne: Ahuzamu, Heferi, Temeni na Haahashtari.

7Hela alimzalia wana watatu: Serethi, Ishari na Ethnani.

8Hakosi aliwazaa Anubi na Sobeba, na ndiye aliyekuwa baba wa jamaa za wazawa wa Aharheli, mwana wa Harumu.

9Kulikuwa na mtu mmoja jina lake Yabesi, aliyeheshimiwa kuliko ndugu zake wote. Mama yake alimpa jina la Yabesi kwa sababu alimzaa kwa maumivu.[#4:9 Katika Kiebrania jina hili linasikika kama neno lenye maana ya “maumivu” ila hapa si dhahiri kwamba mwandishi alikusudia maana hiyo. Katika aya inayofuata (aya 10) tuna habari fupi inayoonesha dhahiri kwamba huyu Yabesi alikuwa mcha Mungu: “alimwomba Mungu wa Israeli …”.]

10Lakini Yabesi alimwomba Mungu wa Israeli akisema, “Ee Mungu, nakusihi unibariki na kuipanua mipaka yangu. Mkono wako uwe pamoja nami na unilinde kutokana na jambo lolote ovu, lisiniumize.” Naye Mungu akamjalia yale aliyoomba.

Jamaa nyingine

11Kelubu, nduguye Shuha, alimzaa Mehiri na Mehiri akamzaa Eshtoni.

12Eshtoni alikuwa na wana watatu: Beth-rafa, Pasea na Tehina. Tehina alikuwa mwanzilishi wa mji wa Ir-nahashi. Wazawa wa watu hawa waliishi Reka.

13Wana wa Kenazi walikuwa: Othnieli na Seraya; na wana wa Othnieli walikuwa Hathathi na Meonothai.[#4:13 “Othnieli” lilikuwa jina la Mwamuzi mmoja kabla Waisraeli hawajatawaliwa na wafalme (Amu 3:7-11). Na jina “Meonothai” linatajwa katika tafsiri mbili za kale lakini hayumo katika makala ya Kiebrania.]

14Meonothai alimzaa Ofra. Seraya alimzaa Yoabu, mwanzilishi wa Bonde la Mafundi, lililopewa jina hilo kwa sababu wote waliokuwa humo walikuwa mafundi stadi.

15Kalebu mwana wa Yefune alikuwa na wana watatu: Iru, Ela na Naamu. Na mwana wa Ela alikuwa Kenazi.[#4:15 Ni huyu aliyewakilisha kabila la Yuda wakati Mose alipotuma wajumbe wa kila kabila kupeleleza nchi ya Kanaani (Hes 13:6). Wakati huo alikuwa na miaka arubaini (Yos 14:7). Wakati wa kugawanyana nchi ya ahadi aliomba apate Hebroni na nchi iliyokuwa karibu na Hebroni, akapewa. Ndiye baba mkwe wa Othnieli, Mwamuzi wa kwanza wa Waisraeli (rejea Amu 1:12-15,20).]

16Wana wa Yehaleli walikuwa Zifu, Zifa, Tiria na Asareli.

17Wana wa Ezra walikuwa Yetheri, Meredi, Eferi na Yaloni. Meredi alimwoa Bithia, bintiye Farao, na hawa ndio wana aliomzalia Meredi: Miriamu, Shamai na Ishba, mwanzilishi wa mji wa Eshtemoa.[#4:17 Huyu Meredi bila shaka alikuwa mtu maarufu kufaulu kumwoa binti wa mfalme (Farao) wa Misri.]

18Meredi alikuwa na mke mwingine Myahudi. Huyu alimzalia Yeredi, mwanzilishi wa Mji wa Gedori, Heberi, mwanzilishi wa mji wa Soko, na Yekuthieli, mwanzilishi wa Mji wa Zanoa.

19Hodia alimwoa dada yake Nahamu ambaye wazawa wake ndio waanzilishi wa kabila la Garmi, lililoishi katika mji wa Keila, na kabila la Maakathi, lililoishi katika mji wa Eshtemoa.

20Wana wa Shimoni walikuwa Amnoni, Rina, Ben-hanani na Tiloni. Ishi alikuwa na wana wawili: Zohethi na Ben-zohethi.

Wazawa wa Shela

21Wana wa Shela, mwana wa Yuda, walikuwa Eri, mwanzilishi wa mji wa Leka, Laada, mwanzilishi wa mji Maresha; ukoo wa wafuma nguo za kitani waliokuwa wakiishi katika mji wa Beth-ashbea;

22Yokimu na watu walioishi katika mji wa Kozeba; na Yoashi na Sarafi waliotawala huko Moabu na wakarejea Lehemu. (Taarifa hizi ni za zamani sana.)

23Hawa ndio wafinyanzi walioishi katika miji ya Netaimu na Gedera, wakimhudumia mfalme.

Wazawa wa Simeoni

24Simeoni alikuwa na wana watano: Nemueli, Yamini, Yaribu, Zera na Shauli.[#4:24-33 Kabila la Simeoni, muda si muda, lilimezwa na kabila la Yuda na kuacha kuwa kabila lililosimama peke yake. Kadiri ya Neh 11:25-30, Waisraeli waliporudi kutoka uhamishoni Babuloni, miji iliyokuwa pale awali mali ya kabila la Simeoni ilikaliwa na watu wa kabila la Yuda.]

25Mwana wa Shauli alikuwa Shalumu; Shalumu alimzaa Mibsamu na Mibsamu akamzaa Mishma.

26Mishma alimzaa Hamueli, aliyemzaa Zakuri, na Zakuri akamzaa Shimei.

27Shimei alikuwa na wana kumi na sita na binti sita, lakini ndugu zake hawakuwa na wana wengi, na jamii yake pia haikuongezeka kama kabila la Yuda.

28Miji walimokuwa wakiishi ilikuwa Beer-sheba, Molada, Hasar-shuali,

29Bilha, Ezemu, Toladi;

30Bethueli, Horma, Siklagi,

31Beth-markabothi, Hazar-susimu, Beth-biri na Shaaraimu. Hiyo ndiyo miji yao mpaka wakati wa utawala wa mfalme Daudi.

32Pia, waliishi katika miji mingine mitano: Etamu, Aini, Rimoni, Tokeni na Ashani,

33pamoja na vijiji kandokando ya miji hiyo huko Baali. Hayo ndiyo yaliyokuwa makao yao, nao waliweka kumbukumbu ya nasaba yao.

34Watu wafuatao walikuwa wakuu wa koo zao: Meshobabu, Yamleki, Yosha mwana wa Amazia,

35Yoeli, Yehu (mwana wa Yoshibia, mwana wa Seraya, mwana wa Asieli.)

36Eliehonai, Yaakoba, Yeshohaya, Asaya, Adieli, Yesimieli, Benaya,

37Ziza (mwana wa Shifi, mwana wa Aloni, mwana wa Yedaya, mwana wa Shimri na mwana wa Shemaya).

38Jamaa zao waliendelea kuongezeka kwa wingi sana. Hawa waliotajwa majina ni wakuu katika jamaa zao na koo zao ziliongezeka sana.

39Walienea hadi kwenye lango la mji wa Gedori, upande wa mashariki wa bonde, ili kuwatafutia kondoo wao malisho.

40Hapo, walipata malisho tele, tena mazuri sana na pia nchi ilikuwa wazi, tulivu na yenye amani, kwani wenyeji wa nchi hiyo wa hapo awali walikuwa Wahamu.

41Katika siku za mfalme Hezekia wa Yuda, watu hao waliotajwa majina yao walikwenda huko Gedori, wakaharibu hema za Wameuni waliokuwa wakiishi huko na kuwafukuza kabisa mpaka leo. Walifanya makao yao ya kudumu huko kwa sababu kulikuwa na malisho tele kwa ajili ya kondoo wao.[#4:41 Taz 2Fal 18—20; alitawala mwaka 716-687 K.K.]

42Watu wengine wa kabila la Simeoni wapatao 500 walikwenda mpaka kwenye mlima Seiri. Waliongozwa na Pelatia, Nearia, Refaya na Uzieli, wana wa Ishi.

43Hapo waliwaua Waamaleki waliosalia baada ya kunusurika, na wakaishi huko mpaka leo.[#4:43 Yaani mpaka wakati habari hizi zilipoandikwa.]

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania