The chat will start when you send the first message.
1Niigeni mimi kama nami ninavyomwiga Kristo.
2Nawapeni hongera kwa sababu mnanikumbuka na kwa sababu mnayashikilia yale maagizo niliyowapeni.[#11:2-16 Katika sehemu hii Paulo anawafundisha Wakorintho namna akina mama wanavyopaswa kujistahi wakati wa ibada. Nyakati zile wanawake hawakuchukuliwa kuwa katika ngazi moja na wanaume. Hata hivyo, tangu mwanzo wa Kanisa wanawake walikuwa na nafasi katika shughuli za kanisa (Rom 16:1,6,12; Fil 4:2-3). Paulo anatambua usawa wa wanawake na wanaume (Gal 3:28) na kuruhusu kwamba wote, wanaume kwa wanawake, wasali na kusema ujumbe wa Mungu kama manabii katika ibada ya hadhara (aya ya 5). Lakini pia anatumia hoja ambayo anaiona ina msingi katika Mwa 1:26-27 (taz 1Kor 11:7 maelezo), kwamba mwanamke yuko chini ya mamlaka ya mwanamume na kuagiza mwanamke afunike kichwa kama ishara ya jambo hilo (taz 1Kor 11:5 maelezo). Bila shaka mila, desturi na tamaduni za wakati huo zilichangia mtazamo huo. Inafaa kuelewa maagizo ya Paulo kulingana na mazingira ya wakati huo.]
3Lakini napenda pia mjue kwamba Kristo ni kichwa cha kila mwanamume, na mwanamume ni kichwa cha mkewe, na Mungu ni kichwa cha Kristo.
4Basi, kila mwanamume anayesali au anayetangaza ujumbe wa Mungu huku amefunika kichwa chake, huyo anamdharau Kristo.[#11:4-5 Katika aya hizi mbili, neno la Kigiriki “kefale” (Kiswahili: “kichwa”) linatumika kwa maana mbili: a) Kichwa yaani sehemu ya juu ya mwili wa mtu, na b) Kichwa, (kwa matumizi ya mfano “mtangulizi”), yaani kiongozi, mtawala, n.k. Tafsiri hii mpya imetilia maanani tofauti hizo, aghalabu kutokana na yaliyosemwa katika aya ya 3 ambapo ni dhahiri kwamba haihusu kichwa cha mwili wa mtu.; #11:4 Tafsiri ya neno kwa neno hapa ingepaswa kuwa “kichwa chake”, lakini ni dhahiri kwamba yahusu Kristo.]
5Na mwanamke akisali au kutangaza ujumbe wa Mungu bila kufunika kichwa chake, anamdharau mumewe; anayefanya hivyo ni sawa tu na mwanamke aliyenyoa kichwa chake.[#11:5 Neno kwa neno ni “kichwa chake”, lakini yahusu mumewe ambaye ndiye aliyesemwa kuwa kichwa (matumizi ya mfano) chake (aya ya 3).]
6Mwanamke asiyefunika kichwa chake, afadhali anyoe nywele zake. Lakini ni aibu kwa mwanamke kukatwa nywele zake au kunyolewa; basi, afadhali afunike kichwa chake.
7Haifai mwanamume kufunika kichwa chake, kwa kuwa yeye ni mfano wa Mungu na kioo cha utukufu wake Mungu; lakini mwanamke ni kioo cha utukufu wa mwanamume.[#11:7 Paulo anarudi tena katika Mwa 1:26-27. Lakini hapo, neno la Kiebrania linalotafsiriwa “mtu” sio mwanamume bali ni binadamu, yaani wote wawili waliumbwa kwa mfano wa Mungu.]
8Mwanamume hakutoka kwa mwanamke, ila mwanamke alitoka kwa mwanamume.
9Mwanamume hakuumbwa kwa ajili ya mwanamke, ila mwanamke aliumbwa kwa ajili ya mwanamume.
10Ndiyo maana mwanamke hufunika kichwa chake, iwe ishara ya mamlaka yaliyo juu yake, na pia kwa sababu ya malaika.[#11:10 Yamkini hiyo nguo anayojifunikia nayo kichwani sasa inakuwa mfano wa kinga na ulinzi ambao mumewe anampatia mkewe (1Kor 11:5 maelezo).; #11:10 Matumizi ya malaika hapa si dhahiri; wengine wanafikiri wanatajwa kwa vile walichukuliwa kama walinzi wa utaratibu duniani na katika ibada (1Tim 5:21).]
11Hata hivyo, mbele ya Bwana mwanamke si kitu bila mwanamume, naye mwanamume si kitu bila mwanamke.[#11:11-12 Rejea Gal 3:28. Paulo anatambua uwiano kati ya mwanamume na mwanamke. Inaonekana kana kwamba hapa Paulo anaeleza zaidi alichosema katika aya 8-9.]
12Kama vile mwanamke alivyotokana na mwanamume, vivyo hivyo mwanamume huzaliwa na mwanamke; kila kitu hutoka kwa Mungu.
13Amueni wenyewe: Je, inafaa mwanamke kumwomba Mungu bila kuvaa kitu kichwani?
14Hata maumbile yenyewe huonesha wazi kwamba kwa mwanamume kuwa na nywele ndefu ni aibu kwake mwenyewe;[#11:14-15 Kwa mara nyingine tena inaonesha kwamba sehemu hii yote imechangiwa sana na mila na desturi au tamaduni za huko Korintho. Aya ya 5 kwa wazi kabisa inaonesha pia jambo hilo maana wanawake wengi zaidi hawana nywele ndefu.]
15lakini kwa mwanamke kuwa na nywele ni heshima kwake; nywele zake ndefu amepewa ili zimfunike.
16Kama mtu anataka kuleta ubishi juu ya jambo hili, basi, na ajue kwamba sisi hatuna desturi nyingine, wala makanisa ya Mungu hayana desturi nyingine.
17Nikiwa bado nawapeni maagizo haya, siwezi hata kidogo kuwapa nyinyi hongera kuhusu haya yafuatayo: mikutano yenu nyinyi waumini yaleta hasara zaidi kuliko faida.[#11:17-34 Paulo anawakosoa Wakorintho kuhusu migawanyiko iliyozuka miongoni mwao na ambayo ilidhihirika katika kuadhimisha Karamu ya Bwana. Kisha anawapa maana ya kweli ya Karamu ya Bwana.]
18Awali ya yote, nasikia kwamba mnapokutana pamoja hutokea mafarakano kati yenu. Nami naamini kiasi,[#11:18 Au, “migawanyiko” kwa maana ya isiyo ya kufaa.]
19maana ni lazima fikira tofauti ziweko miongoni mwenu, ili wale walio thabiti wapate kutambulikana.
20Kweli mnakutana, lakini si kwa ajili ya kula Karamu ya Bwana![#11:20-22 waumini walikutana kula pamoja kwa upendo. Kuadhimisha Karamu ya Bwana ilikuwa sehemu ya mikutano hiyo ya kula pamoja kwa upendo (Mate 2:46 maelezo).]
21Maana mnapokula kila mmoja hukikalia chakula chake mwenyewe, hata hutokea kwamba baadhi yenu wana njaa, na wengine wamelewa![#11:21 Kwa kawaida walipokutana, kila mmoja alileta chakula ambacho kilikuwa kigawanyiwe walioshiriki; lakini huko Korintho wengine walichukua chakula chao chote wao wenyewe bila kugawana na wale waliokuwa maskini ambao bila shaka hawakuleta kitu au walileta kidogo sana (rejea aya 33-34).]
22Je, hamwezi kula na kunywa nyumbani kwenu! Au je, mnalidharau kanisa la Mungu na kuwaaibisha hao wasio na kitu? Niwaambie nini? Niwasifu? La hasha! Si kuhusu jambo hili.
23Maana mimi nilipokea kwa Bwana yale maagizo niliyowaachieni: kwamba, usiku ule Bwana Yesu alipotolewa, alitwaa mkate,
24akamshukuru Mungu, akaumega, akasema: “Huu ndio mwili wangu ulio kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa kunikumbuka.”
25Vivyo hivyo, baada ya kula, akatwaa kikombe cha divai, akasema: “Hiki ni kikombe cha agano jipya linalothibitishwa kwa damu yangu. Fanyeni hivi, kila mnapokunywa, kwa kunikumbuka.”[#11:25 Yer 31:31-34.; #11:25 Kut 24:6-8; taz Mat 26:28 maelezo.]
26Maana kila mnapokula mkate huu na kukinywa kikombe hiki, mwatangaza kifo cha Bwana, mpaka atakapokuja.[#11:26 Kwa kuadhimisha Karamu ya Bwana Kanisa lilitangaza kifo cha Yesu Kristo kuwa ni kitendo cha wokovu ambacho kilele chake kitafikia wakati atakaporudi.]
27Kwa hiyo, kila aulaye mkate huo au kunywa kikombe cha Bwana bila kustahili, atakuwa na hatia dhidi ya mwili na damu ya Bwana.
28Basi, kila mtu ajichunguze mwenyewe kwanza, ndipo ale mkate huo na anywe kikombe hicho;
29maana anayekula na kunywa bila kutambua maana ya mwili wa Bwana, anakula na kunywa hukumu yake yeye mwenyewe.
30Ndiyo maana wengi kati yenu ni dhaifu na wagonjwa, na wengine kadhaa wamekufa.
31Kama tungejichunguza wenyewe vizuri hatungeadhibiwa hivyo.
32Lakini tunapohukumiwa na Bwana, tunafunzwa tuwe na nidhamu, ili tusije tukahukumiwa pamoja na ulimwengu.
33Kwa hiyo, ndugu zangu, mnapokutana kula Karamu ya Bwana, kila mmoja amngoje mwenzake.
34Na kama kuna yeyote aliye na njaa, na ale nyumbani kwake, ili kukutana kwenu kusisababishe hukumu. Lakini, kuhusu yale mambo mengine, nitawapeni maelezo nitakapokuja.