1 Wakorintho 15

1 Wakorintho 15

Ufufuo wa Kristo

1Sasa, ndugu, napenda kuwakumbusha ile Habari Njema niliyowahubirieni, nanyi mkaipokea na kusimama imara ndani yake.[#15:1-58 Baadhi ya Wakristo wa Korintho walifikiri kwamba wafu hawatafufuliwa. Yamkini waliona kwamba Wakristo walikwisha pata uhai wa milele na kwamba miili yao haikuwa na nafasi katika jambo hilo (taz 6:12-20). Katika sura hii ya 15 Paulo anakanusha mtazamo huo na kusisitiza ufufuo wa Yesu Kristo na ufufuo wa waumini. Katika aya 1-7 tunapewa kwa kifupi kiini cha Habari Njema (taz 15:4 maelezo).; #15:1 Katika 15:1,3 na 11, Paulo anatilia mkazo hali ya fundisho hilo kuhusu ufufuo kama lilivyopokelewa na wote. Anakumbusha hapa katika aya 1-7 matukio ya kimsingi ya historia ya ukombozi.]

2Kwa njia yake mnaokolewa, ikiwa mnayazingatia maneno niliyowahubirieni, na kama kuamini kwenu hakukuwa bure.[#15:2 Rejea 15:16-17.]

3Mimi niliwakabidhi nyinyi mambo muhimu sana ambayo mimi niliyapokea: kwamba Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu kufuatana na Maandiko Matakatifu;[#15:3 Rejea Isa 53:5-12. Hapa na katika 15:4 maneno: “Maandiko Matakatifu” yanaweza kuhusu ujumbe wote kwa jumla katika A.K. na sio tu kuhusu sehemu fulani pekee; rejea Luka 24:25-27,44-46 na taz Yoh 20:9.]

4kwamba alizikwa, akafufuka siku ya tatu kufuatana na Maandiko Matakatifu;[#15:4 Rejea Zab 16:10; Mat 12:40; Mate 2:24-32. Na kuhusu “siku ya tatu” taz Mat 16:21; Marko 8:31; Luka 9:22. Matukio yanayotajwa katika 15:3-4 yanawakilisha kiini cha Habari Njema ya Kristo kama ilivyotangazwa tangu mwanzo wa kanisa (taz Mate 2:14-40 maelezo).]

5kwamba alimtokea Kefa, na baadaye aliwatokea wale kumi na wawili.

6Kisha aliwatokea ndugu zaidi ya 500 kwa mara moja; wengi wao wanaishi bado, lakini baadhi yao wamekwisha kufa.[#15:6 Hakuna mahali pengine katika A.J. ambapo inasemwa kwamba Yesu aliwatokea watu wengi kiasi hicho. Lakini kwa vile tunaambiwa pia “wengi wao wanaishi bado”, Paulo anawaambia kwamba wanaweza kuhakikisha kutoka kwao.]

7Baadaye alimtokea Yakobo kisha akawatokea mitume wote.[#15:7 Yamkini ni yule ambaye anaitwa pia “ndugu yake Bwana” (Gal 1:19; taz Mate 12:17 maelezo).]

8Baada ya wote, akanitokea hata mimi, mimi niliyekuwa kama mtu aliyezaliwa kabla ya wakati.[#15:8 Mate 9:3-6; 1Kor 9:1.; #15:8 Yamkini yahusu namna Paulo alivyozaliwa kwa namna ya pekee katika imani ya Kikristo, au kuhusu kuongoka kwake kulikotukia wakati tofauti na ule wa mitume.]

9Maana mimi ni mdogo kabisa miongoni mwa mitume, na wala sistahili kuitwa mtume, kwa sababu nililidhulumu kanisa la Mungu.

10Lakini, kwa neema yake Mungu, nimekuwa kama nilivyo, na neema yake kwangu haikuwa bure. Mimi nimefanya kazi kuliko wote; si mimi hasa, ila ni neema ya Mungu ifanyayo kazi pamoja nami.

11Lakini hata hivyo, iwe wao ndio wahubirio au mimi nihubiriye, haidhuru, hiki ndicho tunachohubiri, na hiki ndicho mnachoamini.

Ufufuo wetu

12Sasa, maadamu inahubiriwa kwamba Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu, baadhi yenu wanawezaje kusema kwamba hakuna ufufuo wa wafu?

13Kama hakuna ufufuo wa wafu, basi, Kristo naye hakufufuka;

14na kama Kristo hakufufuka, basi mahubiri yetu hayana maana na imani yenu haina maana.

15Zaidi ya hayo sisi tungekuwa mashahidi wa uongo mbele ya Mungu, maana tulisema kwamba Mungu alimfufua Kristo kutoka kwa wafu na kumbe yeye hakumfufua — kama ni kweli kwamba wafu hawafufuliwi.

16Maana, ikiwa ni kweli kwamba wafu hawafufuki, basi naye Kristo hakufufuka.

17Na kama Kristo hakufufuliwa, basi, imani yenu ni ya bure; mngali bado katika dhambi zenu.[#15:17 Ufufuo wa Yesu ni sehemu muhimu isiyoweza kutenganishwa na kitendo chake cha kuwakomboa binadamu, na ambao bila huo haingewezekana kuwaondolea dhambi.]

18Zaidi ya hayo, wale wote waliokufa wakiwa wameungana na Kristo wamepotea kabisa.

19Kama matumaini yetu katika Kristo yanahusu tu maisha haya ya sasa, basi, sisi ni watu wa kusikitikiwa zaidi kuliko wengine wote duniani.

20Lakini ukweli ni kwamba Kristo amefufuliwa kutoka kwa wafu, wa kwanza wa wale waliolala katika kifo.[#15:20 Kol 1:18. Kristo akiwa wa kwanza amekuwa pia kwa ufufuo wake dhamana kwa ajili ya wale wanaomwamini.]

21Maana kama vile kifo kilivyoletwa duniani na mtu mmoja, vivyo hivyo nako kufufuka kutoka kwa wafu kumesababishwa na mtu mmoja.

22Kama vile watu wote wanavyokufa kwa kujiunga na Adamu, vivyo hivyo wote watafufuliwa kwa kuungana na Kristo.

23Lakini kila mmoja kwa mpango wake: Kristo kwanza; halafu wale walio wake Kristo wakati Kristo atakapokuja.

24Baada ya hayo, mwisho utafika wakati ambapo Kristo atamkabidhi Mungu Baba ufalme, baada ya kufutilia mbali kila tawala na mamlaka na nguvu.[#15:24 Maneno matatu ambayo yanataja nguvu (hasa nguvu za kiroho) ambazo ni adui wa Mungu (Kol 2:15).]

25Maana Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda maadui zake wote na kuwaweka chini ya miguu yake.[#15:25 Zab 110:1; taz Mat 22:44 maelezo.]

26Adui wa mwisho atakayeangamizwa ni kifo.

27Maana, Maandiko yasema: “Mungu ameweka vitu vyote chini ya miguu yake.” Lakini, Maandiko yanaposema: “Vitu vyote vimewekwa chini ya miguu yake avitawale” ni dhahiri kwamba Mungu haingii katika kundi hilo la vitu, maana yeye ndiye anayeviweka vitu hivyo chini ya Kristo.

28Lakini vitu vyote vitakapowekwa chini ya utawala wa Kristo, ndipo naye Mwana atakapojiweka chini ya Mungu, aliyeweka vyote chini ya utawala wake; ili Mungu atawale juu ya vyote.

29Kama hakuna ufufuo, je watu wale wanaobatizwa kwa ajili ya wafu wanatumainia kupata nini? Kama wafu hawafufuliwi, ya nini kubatizwa kwa ajili yao?[#15:29 Hatuna habari yoyote juu ya desturi hii. Hoja ya Paulo hapa ni kwamba kufanya hivyo kunamaanisha kwamba kuna matumaini ya ufufuo wa wafu.]

30Na sisi, ya nini kujitia hatarini kila saa?

31Ndugu, mimi nakikabili kifo kila siku! Fahari niliyo nayo juu yenu katika kuungana na Kristo Yesu Bwana wetu inanifanya nitangaze jambo hili.

32Kama kusudi langu lingalikuwa la kibinadamu tu, kule kupigana kwangu na wanyama wakali hapa Efeso kungalinifaa kitu gani? Kama wafu hawafufuki, basi, “Tule na tunywe, maana kesho tutakufa.”[#15:32 Yamkini Paulo anagusia hapa desturi ya tamasha za Waroma za kupigana na wanyama wakali; anatumia kisa hicho kwa mfano wa hatari fulani alizokabiliana nazo katika kuhubiri Habari Njema (rejea Mate 19:23-41; 2Kor 1:8).; #15:32 Huu ni msemo au methali walioutumia watu wengi (Isa 22:13; taz Luka 12:19 maelezo).]

33Msidanganyike! Urafiki mbaya huharibu tabia njema.[#15:33 Msemo ambao yasemekana mtu wa kwanza kuutumia ni Mgiriki mmoja aitwaye Meneanderi (Karne ya 4 K.K.)]

34Amkeni! Anzeni kuishi vema, na acheni kutenda dhambi. Baadhi yenu hawamjui Mungu kabisa. Hii nawaambieni, ni aibu kubwa kwenu!

Mwili wa ufufuo

35Lakini mtu anaweza kuuliza: “Wafu watafufuliwaje? Watakuwa na mwili wa namna gani?”[#15:35 Wagiriki waliamini kwamba roho ya binadamu haifi lakini hawakuamini kwamba kuna ufufuo wa wafu.]

36Hayo ni maswali ya kijinga! Ukipanda mbegu, isipokufa kwanza haitaota.

37Unachopanda ni mbegu tu, labda ya ngano au nafaka nyingine, na si mmea mzima ambao hutokea baadaye.

38Mungu huipa hiyo mbegu mwili anaoutaka mwenyewe; kila mbegu hupata mwili wake wa pekee.

39Miili ya viumbe vyote si sawa. Miili ya binadamu ni ya namna moja, ya wanyama ni ya namna nyingine, ya ndege ni ya namna nyingine na miili ya samaki pia ni ya namna nyingine.

40Iko miili ya mbinguni na miili ya duniani; uzuri wa miili ya mbinguni ni mwingine, na na uzuri wa miili ya duniani ni mwingine.[#15:40 Si rahisi kuelewa Paulo anataka kusema nini hasa; lakini miili ya mbinguni ni miili au viumbe ambao kimaumbile makazi yao ni mbinguni, na miili ya duniani ni miili au viumbe ambao kimaumbile makazi yao ni duniani (aya 47-49). Yawezekana pia kwamba kutaja miili ya mbinguni kumesaidiwa na kule kutaja sayari za angani katika aya ya 41.]

41Uko uzuri wa jua, wa mwezi na wa nyota; hata nyota nazo huhitilafiana kwa uzuri.

42Ndivyo ilivyo kuhusu ufufuo wa wafu. Kama vile mbegu, mwili huzikwa ardhini ukiwa katika hali ya kuharibika, lakini hufufuliwa katika hali ya kutoharibika.

43Huzikwa katika hali duni, hufufuliwa katika hali tukufu; huzikwa katika hali dhaifu, hufufuliwa ukiwa wenye nguvu.

44Unapozikwa ni mwili wa kawaida, unapofufuliwa ni mwili wa kiroho. Kuna mwili wa kawaida na kutakuwa na mwili wa kiroho.

45Maana Maandiko yasema: “Mtu wa kwanza, Adamu, alikuwa kiumbe mwenye uhai;” lakini Adamu wa mwisho ni Roho awapaye watu uhai.

46Lakini unaotangulia kuwako si ule mwili wa kiroho, ila ule mwili wa kawaida, kisha ule mwili wa kiroho.

47Adamu wa kwanza aliumbwa kwa udongo, alitoka ardhini; mtu wa pili alitoka mbinguni.

48Wote walio wa dunia wako kama huyo mtu aliyeumbwa kwa udongo; wale walio wa mbinguni wako kama yule aliyetoka mbinguni.

49Kama vile tulivyofanana na yule aliyeumbwa kwa udongo, vivyo hivyo tutafanana na huyo aliyetoka mbinguni.

50Basi, ndugu, nasema hivi: kile kilichofanywa kwa mwili na damu hakiwezi kuushiriki ufalme wa Mungu; na chenye kuharibika hakiwezi kuwa na hali ya kutoharibika.

51Sikilizeni, nawaambieni siri: sisi hatutakufa sote, ila sote tutageuzwa,[#15:51-52 1Thes 4:13-17. Paulo anaandika haya akifikiri kwamba yeye na wasomaji wake wangekuwa hai wakati wa kurudi kwake Yesu Kristo.]

52wakati wa mbiu ya mwisho, kwa nukta moja, kufumba na kufumbua. Maana tarumbeta ya mwisho itakapolia, wafu watafufuliwa katika hali ya kutoweza kufa tena, na sisi tutageuzwa.

53Maana ni lazima kila kiharibikacho kijivalie hali ya kutoharibika, mwili uwezao kufa ujivalie hali ya kutokufa.

54Basi, mwili huu wenye kuharibika utakapojivalia hali ya kutoharibika, na kile chenye kufa kitakapojivalia hali ya kutokufa, hapo ndipo litakapotimia lile neno lililoandikwa: “Kifo kimeangamizwa; ushindi umekamilika!”

55“Kifo, ushindi wako uko wapi?

Uwezo wako wa kuumiza uko wapi?”

56Kifo hupata sumu yake katika dhambi, nayo dhambi hupata nguvu yake katika sheria.[#15:56-57 Wazo hili limeendelezwa zaidi katika Rom 5—7 na huko katika Rom 7:25, kama vile hapa, Paulo anamalizia pia kwa maneno ya shukrani kwa Mungu.]

57Lakini tumshukuru Mungu anayetupatia ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo.

58Basi, ndugu zangu wapenzi, simameni imara na thabiti. Endeleeni daima kuwa na bidii katika kazi ya Bwana, mkijua kwamba kazi mnayofanya katika utumishi wa Bwana haitapotea bure.

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania