The chat will start when you send the first message.
1Sasa, yahusu ule mchango kwa ajili ya watu wa Mungu: fanyeni kama nilivyoyaagiza makanisa ya Galatia.[#16:1 “Watu wa Mungu”, neno kwa neno “watakatifu”. Kuhusu mchango huu na hao walengwa taz Mate 20:1-6 maelezo na Rom 15:25,26,27,28, 29 maelezo. Yawezekana, kutokana na jinsi ya kusema hapa, kwamba Wakorintho walikuwa wamemuuliza Paulo kuhusu mchango huo katika ile barua yao (1Kor 7:1) naye Paulo sasa anawajibu lakini anatoa maagizo mengine zaidi katika barua nyingine (2Kor 8—9).]
2Kila Jumapili kila mmoja wenu atenge kiasi cha fedha kadiri ya mapato yake, ili kusiwe na haja ya kufanya mchango wakati nitakapokuja.
3Wakati nitakapokuja kwenu, nitawatuma wale mtakaowachagua miongoni mwenu wapeleke barua na zawadi zenu Yerusalemu.[#16:3-4 Taz Mate 20:4 maelezo.]
4Kama itafaa nami niende, basi, watakwenda pamoja nami.
5Nitakuja kwenu baada ya kupitia Makedonia — maana nataraji kupitia Makedonia.[#16:5-6 Rejea Mate 19:21 na taz Mate 20:1-6 maelezo.]
6Labda nitakaa kwenu kwa muda fulani, au huenda nitakaa pamoja nanyi wakati wote wa baridi, ili mpate kunisaidia niendelee na safari yangu kokote nitakakokwenda.
7Sipendi kupita kwenu harakaharaka na kuendelea na safari. Natumaini kukaa kwenu kwa kitambo fulani, Bwana akiniruhusu.
8Lakini nitabaki hapa Efeso mpaka siku ya Pentekoste.[#16:8 Mate 19:8-41; taz Mate 19:10 maelezo.]
9Mlango uko wazi kabisa kwa ajili ya kazi yangu muhimu hapa, ingawa wapinzani nao ni wengi.
10Timotheo akija, angalieni asiwe na hofu yoyote wakati yupo kati yenu, kwani anafanya kazi ya Bwana kama mimi.[#16:10 1Kor 4:17.]
11Kwa hiyo mtu yeyote asimdharau, ila msaidieni aendelee na safari yake kwa amani ili aweze kurudi kwangu, maana mimi namngojea pamoja na ndugu zetu.
12Kuhusu ndugu Apolo, nimemsihi sana aje kwenu pamoja na ndugu wengine, lakini hapendelei kabisa kuja sasa ila atakuja mara itakapowezekana.[#16:12 1Kor 1:12]
13Kesheni, simameni imara katika imani, muwe hodari na wenye nguvu.
14Kila mfanyacho kifanyike kwa upendo.[#16:14 Anachosema Paulo hapa amekiendeleza katika sura ya 13.]
15Ndugu, mnaifahamu jamaa ya Stefana; wao ni watu wa kwanza kabisa kuipokea imani ya Kikristo katika Akaya, na wamejitolea kuwatumikia watu wa Mungu. Ninawasihi nyinyi ndugu zangu,[#16:15 1Kor 1:16.]
16muufuate uongozi wa watu kama hao, na uongozi wa kila mtu afanyaye kazi na kutumika pamoja nao.
17Nafurahi sana kwamba Stefana, Fortunato na Akaiko wamefika; wamelijaza pengo lililokuwako kwa kutokuwako kwenu.[#16:17 Ni dhahiri kwamba hao waumini walifika kutoka Korintho kumtembelea Paulo.]
18Wameiburudisha roho yangu na yenu pia. Kwa hiyo inafaa kuwakumbuka watu wa namna hii.
19Makanisa yote ya Asia yanawasalimuni. Akula na Priska pamoja na watu wote wa Mungu walio nyumbani mwao wanawasalimuni sana katika kuungana na Bwana.[#16:19 Mkoa wa Kiroma wakati huo, mji wake mkuu ukiwa ni Efeso. Eneo hilo sasa ni nchi ya Uturuki.; #16:19 Hawa walikuwa hapo kwanza huko Korintho (Mate 18:2-3) halafu huko Efeso (Mate 18:18—19:26). Priska anatajwa pia kama “Priskila”.]
20Ndugu wote wanawasalimuni. Nanyi salimianeni kwa ishara ya mapendo ya Mungu.[#16:20 Neno kwa neno “busu takatifu”. Taz Rom 16:16 maelezo.]
21Mimi Paulo nawasalimuni, nikiandika kwa mkono wangu mwenyewe.[#16:21 Baada ya Paulo kutoa imla, alitia sahihi kwa mkono wake mwenyewe na kujazia maneno ya mwisho (rejea Gal 6:11; Kol 4:18; 2Thes 3:17; File 19).]
22Yeyote asiyempenda Bwana, na alaaniwe. MARANATHA — BWANA, NJOO![#16:22 Gal 1:8-9; maneno yaliyotumika ilipohitajika kwa maana ya “atengwe” yaani, mbali na jumuiya.; #16:22 Neno la Kiaramu lenye maana hiyo. Yamkini neno hilo lilikuwa limechukuliwa lilivyo katika lugha ya Kiaramu na kuingizwa katika sala ya Wakristo.]
23Neema ya Bwana Yesu iwe nanyi.[#16:23 Paulo anamalizia barua yake kwa maneno kanuni (Rom 16:24; 2Kor 13:13, n.k.) ambayo yanatumika pia katika Ufu 22:20-21 yakiunganishwa na ombi: “Njoo Bwana Yesu!” kama hapa pia.]
24Upendo wangu uwe kwenu katika kuungana na Kristo Yesu.[#16:24 Hati nyingine za kale zinajazia hapa neno “Amina”.]