1 Wakorintho 5

1 Wakorintho 5

Ukosefu wa uadilifu katika kanisa

1Ziko habari za kuaminika kwamba kuna uzinzi miongoni mwenu; tena ni uzinzi mbaya ambao haujapata kuwako hata kati ya watu wasiomjua Mungu. Nimeambiwa eti mmoja wenu anaishi na mke wa baba yake![#5:1—6:20 Katika sehemu hii ya pili ya hii barua kwa Wakorintho, Paulo anakabili matatizo matatu ya ukiukaji wa maadili: kisa cha mwanamume mmoja kuwa na uhusiano wa kimwili na mama yake wa kambo (5:1-13); kupeleka kesi mahakamani kwa watu wasio waumini (6:1-11); na pia kuhusu maana ya uhuru wa kweli (6:12-20).; #5:1 Neno “anaishi” linatumika hapa kama lugha ya picha, yaani anajamiiana na mke wa baba yake. Ni kama amemchukua kuwa mke wake. Na kuhusu “mke wa baba yake” ni dhahiri kwamba si mama yake bali ni mama yake wa kambo. Jambo hili lilikatazwa na sheria ya Mose (Lawi 18:8) na hata sheria ya Waroma haikuruhusu uhusiano wa aina hiyo.]

2Mnawezaje kujivuna? Ingekuwa afadhali kwenu kuomboleza, na huyo aliyefanya kitu hicho aondolewe miongoni mwenu.[#5:2 Au, “Atengwe”. Lengo la kumtenga huyo mwenye hatia mbali na jumuiya ya waumini, ilikuwa kuweka salama hali takatifu ya kanisa; rejea 1Kor 3:16-17.]

3Nami, kwa upande wangu, ingawa kwa mwili niko mbali nanyi, hata hivyo kwa roho niko hapo pamoja nanyi: na hivyo, kama vile nipo hapo, nimekwisha mhukumu huyo aliyefanya jambo hilo la aibu.[#5:3-5 Paulo analitaka kanisa likiwa limekutana liidhinishe hukumu hiyo ya kutengwa kwa huyo aliyekosa ili kumrudi (rejea 1Tim 1:20).]

4Wakati mnapokusanyika pamoja kwa jina la Bwana Yesu, nami nikiwa pamoja nanyi kwa roho, basi, kwa uwezo wa Bwana wetu Yesu,

5mkabidhini mtu huyo kwa Shetani ili mwili wake uharibiwe na roho yake iweze kuokolewa siku ile ya Bwana.

6Majivuno yenu hayafai! Je, hamjui kwamba chachu kidogo huchachusha donge lote la unga?[#5:6 Msemo huu ni kama kitendawili. Kama vile chachu hupenya donge lote la unga uliokandwa kuwa mkate, uovu wa mtu mmoja utaozesha jumuiya yote ya kanisa ambayo inaukubali. Taz pia Gal 5:9.]

7Jitakaseni, mkatupe mbali chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu kama mnavyopaswa kuwa; maana, Kristo, Pasaka yetu, amekwisha tolewa kuwa sadaka.[#5:7 Mwanakondoo aliyetolewa kuwa tambiko ya Pasaka ni mfano wa Kristo, taz maelezo ya Yoh 1:29 na Kut 12:5,21; 1Pet 1:19.]

8Basi, tufanye karamu hiyo si kwa chachu ile ya kale, chachu ya ubaya na uovu, bali kwa mkate usiotiwa chachu, mkate wa usafi na kweli.

9Niliwaandikia katika barua yangu msishirikiane na wazinzi.[#5:9 Hapa tuna dokezo kuhusu barua ya awali ambayo Paulo alikuwa amewaandikia waumini wa Korintho. Wengine wanafikiri sehemu ya barua hiyo kimsingi iko katika 2Kor 6:14—7:1.]

10Ukweli ni kwamba sikuwa na maana ya watu wote duniani walio wazinzi, wachoyo, walaghai na wenye kuabudu sanamu. Maana, ili kuwaepa hao wote ingewalazimu nyinyi kuihama dunia hii kabisa!

11Nilichoandika ni hiki: msishirikiane na ndugu Mkristo aliye mzinzi, mchoyo, mwenye kuabudu sanamu, mchongezi, mlevi na mlaghai. Mtu wa namna hiyo, hata kula msile naye.[#5:11 Yamkini Paulo alimaanisha kwamba mtu au watu wa namna hiyo wasiruhusiwe kushiriki chakula cha jumuiya pamoja na Karamu ya Bwana (1Kor 10:16-21; taz pia 2Thes 3:14).]

12Je, ni shauri langu kuwahukumu watu walio nje? Hao Mungu atawahukumu. Je, nyinyi hampaswi kuwahukumu wale walio katika jamii yenu nyinyi wenyewe?[#5:12-13 Kumb 13:5; 17:7; 22:21. Lengo la kuchukuliwa hatua hiyo lilikuwa kuhifadhi maadili ya jumuiya.]

13Mfukuzeni mbali nanyi huyo mwovu!

Copyright The Bible Society of Tanzania, 1993 The Bible Society of Kenya 1993
Published by: Bible Society of Tanzania