The chat will start when you send the first message.
1Anathubutuje mmoja wenu kumshtaki ndugu mwaamini mbele ya mahakama ya watu wasiomjua Mungu badala ya kumshtaki mbele ya watu wa Mungu?[#6:1-2 Ilikuwa kawaida nyakati hizo, hasa miongoni mwa Wayahudi walioishi mbali na makwao, na pia kwa makundi mengine, kutatua matatizo yao katika vikundi vyao au jumuiya zao na hivyo kuepa kushtakiana mahakamani.]
2Je, hamjui kwamba watu wa Mungu watauhukumu ulimwengu? Ikiwa basi, ulimwengu utahukumiwa nanyi, kwa nini hamstahili kuhukumu hata katika mambo madogo?
3Je, hamjui kwamba, licha ya kuhukumu mambo ya kawaida ya kila siku, tutawahukumu hata malaika?
4Mnapokuwa na mizozo juu ya mambo ya kawaida, je, mnawaita wawe mahakimu watu ambao hata hawalijali kanisa?
5Aibu kwenu! Ndiyo kusema hakuna hata mmoja miongoni mwenu mwenye hekima kiasi cha kuweza kutatua tatizo kati ya ndugu waumini?
6Badala yake, kweli imekuwa mtindo ndugu kumpeleka ndugu yake mahakamani, tena mbele ya mahakimu wasioamini.
7Kwa kweli huko kushtakiana tu wenyewe kwa wenyewe kwabainisha kwamba mmeshindwa kabisa! Je, haingekuwa jambo bora zaidi kwenu kudhulumiwa? Haingekuwa bora zaidi kwenu kunyang'anywa mali yenu?
8Lakini, badala yake, nyinyi ndio mnaodhulumu na kunyang'anya; tena, hayo mnawafanyia ndugu zenu!
9Au je, hamjui kwamba watu wabaya hawataurithi ufalme wa Mungu? Msijidanganye! Watu wanaoishi maisha ya uasherati, wanaoabudu sanamu, wazinzi, au walawiti,
10wezi, wachoyo, walevi, wasengenyaji, wanyang'anyi, hao wote hawatashiriki ufalme wa Mungu.
11Baadhi yenu mlikuwa hivyo; lakini sasa mmeoshwa, mkafanywa watakatifu, na kufanywa waadilifu na kupatanishwa na Mungu kwa jina la Bwana Yesu Kristo na kwa Roho wa Mungu wetu.[#6:11 Rejea Tito 3:5.; #6:11 Taz Rom 1:17 maelezo.; #6:11 Yaani kwa nafsi yake Yesu Kristo.]
12Mtu anaweza kusema: “Kwangu mimi kila kitu ni halali.” Sawa; lakini si kila kitu kinafaa. Nakubali kwamba kila kitu ni halali kwangu lakini sitaki kutawaliwa na kitu chochote.[#6:12 Yaani, “mimi nina uhuru wa kufanya chochote ninachotaka”. Yahusu tamko thabiti la uhuru wa Kikristo ambao yamkini Paulo mwenyewe pia alikuwa nao na kuutumia (rejea Rom 7:6; Gal 5:1,13), lakini Wakorintho wengine walikariri tamko hilo ili kuhalalisha ufisadi wao.; #6:12-16 Baadhi ya waumini wa Korintho walifikiri kwamba walikuwa na uhuru wa kufanya chochote (taz pia 10:33), hata kuwa na uhusiano wa kimwili na kahaba. Tamko la Paulo ni kwamba miili ya waumini ni hekalu la Roho Mtakatifu (aya ya 19) na kwa sababu hiyo isitumiwe kamwe kwa uasherati bali kwa kumtumikia Mungu.]
13Unaweza kusema: “Chakula ni kwa ajili ya tumbo, na tumbo ni kwa ajili ya chakula.” Sawa; lakini Mungu ataviharibu vyote viwili. Mwili wa mtu si kwa ajili ya uzinzi bali ni kwa ajili ya kumtumikia Bwana, naye Bwana ni kwa ajili ya mwili.[#6:13 Namna ya kitendawili ambacho baadhi walikitumia kuhalalisha uhuru wa kutosheleza tamaa zao za mwili.; #6:13 1Kor 3:23. Ndiyo kusema mwenye mamlaka juu ya mwaamini ni Kristo.]
14Basi, Mungu aliyemfufua Bwana kutoka wafu atatufufua nasi pia kwa nguvu yake.
15Je, hamjui kwamba miili yenu ni viungo vya mwili wa Kristo? Je, mnadhani naweza kuchukua sehemu ya mwili wa Kristo na kuifanya kuwa sehemu ya mwili wa kahaba? Hata kidogo!
16Maana, kama mjuavyo, anayeungana na kahaba huwa mwili mmoja naye — kama ilivyoandikwa: “Nao wawili watakuwa mwili mmoja.”
17Lakini aliyejiunga na Bwana huwa roho moja naye.
18Jiepusheni kabisa na uzinzi. Dhambi nyingine zote hutendwa nje ya mwili lakini mzinzi hutenda dhambi dhidi ya mwili wake mwenyewe.
19Je, hamjui kwamba miili yenu ni hekalu la Roho Mtakatifu aliye ndani yenu, ambaye mlimpokea kutoka kwa Mungu? Nyinyi basi, si mali yenu wenyewe.
20Mlinunuliwa kwa bei kubwa. Kwa hiyo, itumieni miili yenu kwa ajili ya kumtukuza Mungu.[#6:20 Yaani Mungu aliwanunua: 1Kor 7:23; Ufu 5:9; taz Rom 3:25 maelezo.]